Buriani Turky, wapigakura Mpendae watakukumbuka

16Sep 2020
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Buriani Turky, wapigakura Mpendae watakukumbuka

MGOMBEA ubunge aliyetarajia kuwania kiti cha ubunge wa jimbo la Mpendae visiwani Zanzibar, Salim Hassan Turky, amefariki dunia zikiwa zimesalia siku 42 kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu. Wa Oktoba 28.

Kifo chake kilichotangazwa na vyombo mbalimbali vya habari vikimnukuu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole, akielezea masikitiko ya chama kufuatia kifo hicho cha ghafla kilichotokea juzi jioni.

Alifariki dunia katika Hospitali ya Global iliyopo mjini Zanzibar wakati akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla, kwa mujibu wa taarifa za wanafamilia yake.

Kifo cha Turky maarufu kama ‘Mr White’ kutokana na mtindo wake wa kuvalia mavazi meupe akiwa bungeni na kwenye mikusanyiko mbalimbali kinaurejesha tena mchakato wa kutangaza nia, uteuzi na kuanza kampeni upya katika jimbo la Mpandae aliloliongoza tangu mwaka 2010.

Wapigakura wa jimbo la Mpendae pia wamepata pigo wakati hivi sasa kampeni za uchaguzi zikiwa zimeshika kasi nchi nzima kwa wagombea wa udiwani, ubunge, uwakilishi na urais kuendelea kunadi sera zao kwa wapigakura.

Mgombea huyu alikuwa maarufu kwa jina la ‘Mr White’ kutokana na uvaaji wake wa nguo nyeupe, alikuwa, akitetea kiti hicho baada ya kuwa mbunge kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka huu.

Mwanasiasa Turky ni kijana katika uwanja wa siasa aliyezaliwa mwaka 1963 atakumbukwa kwa mchango wake katika sekta nyingi ukiwamo usafirishaji, uzalishaji viwandani na michezo.

Kwenye michezo alikuwa anashiriki wa hali na mali kuinua michezo visiwani Zanzibar kwa kuichangia timu ya taifa.

Katika hilo wadau wa michezo pia wanamlilia wakimkumbuka kwa kujitoa kwake kwa kuwa mwaka 2017 Salim Hassan Turky aliwahi kuzichangia fedha timu ya Zanzibar Heroes, ambayo inashiriki michuano mbalimbali ikiwamo ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Jumatano Oktoba 28 ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshatangaza jumla ya majimbo ya Tanzania Bara na visiwani Zanzibar, Mpendae haitashiriki.

Katika siku za mwisho za maisha yake kisiasa, wengi walishuhudia wiki iliyopita Septemba 12, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, akimnadi mgombea huyo Salim Turky katika uzinduzi wa kampeni za CCM zilizofanyika viwanja vya Demokrasia Kibandamaiti.

Hatua hiyo inaweza kufananishwa na kuwaaga wapiga kura wake na wananchi pia kuagana na kiongozi wao.

Kutoka na kifo cha Turky, kanuni na sheria za uchaguzi zinabainisha kuwa jimbo au kata inapoteza sifa ya kushiriki iwapo mgombea amefariki au kuhama chama.

Kutokana na taratibu hizo Mpendae inapoteza sifa hiyo, na uchaguzi katika jimbo hili utasitishwa na kusubiri mchakato mpya kama ilivyokuwa awali katika kuwapata wagombea kutoka vyama mbalimbali vinavyoshiriki.

Mchakato huo huanzia katika vyama kwa wagombea kutangazania, kuchukua fomu hadi kuteuliwa.

Mchakato huo jimboni Mpendae utasimama hadi Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakapotangaza, ratiba na taratibu nyingine za kisheria.

Ni wazi kuwa washabiki wake wa Mpendae wamepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kiongozi wao huyo ambaye huenda walimtegemea kuwaongoza tena kwa miaka mitano ijayo.
Buriani Turky.