CHADEMA igeni mfano wa ACT-Wazalendo

03Jan 2021
Nkwazi Mhango
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
CHADEMA igeni mfano wa ACT-Wazalendo

UCHAGUZI mkuu uliopita ulijaa vimbwanga, visasi, visingizio hata vitisho hasa baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilishinda kwa kishindo kwa aslimia 84 urais na kuzoa viti karibu vyote.

Huku upinzani ukiambulia viti viwili tu upande wa Bara jambo ambalo halijawahi kutokea tangu kuingia mfumo wa vyama vingi.

Japo ni nje ya mada ya leo, washindi wa viti viwili tu vya upinzani Bara ni wanawake mmoja toka CHADEMA na mwingine toka CUF. Hivyo, unaweza kusema kuwa uchaguzi wa mwaka huu umeutia ufa mfumo dume na imani kuwa kinamama hawawezi siasa za ushindani wakati wanaziweza kama walivyodhihirisha. Kwani, kwenye bunge lililoanza hivi karibuni, upinzani kwa upande wa Bara hautakuwa na mwanamume hata mmoja. Ushindi wa kinamama hawa ambapo wanaume wote walishindwa uwahamasishe kinamama wengi kushiriki nafasi za kuchaguliwa na kuachana na kutegemea nafasi za viti maalumu ambazo sasa ziko zinawagombanisha wao kwa wao na vyama vyao kwa baadhi ya vyama. Kimsingi, viti hivi viwili vinakomesha matusi na upuuzi kuwa kinamama siyo thabiti kisiasa kiasi cha kutegemea viti vya dezo. Kama kinamama wameweza kumzaa kila mmoja wa binadamu wote duniani, watashindwa nini kumwongoza? Nayapongeza majimbo yaliyowachagua hawa kinamama wawili waliovunja rekodi ya kuwachakaza wanaume waliotoka kapa kiasi cha sasa kuanza hata kuwawekea mizengo kwenye viti walivyoshinda kihalali na kwa kuvuja jasho.

Hata hivyo, pamoja na upinzani kusimama kidete kupinga matokeo, wapo waliofanya kile ambacho Waingereza huita Road to Damascus kwenye kisa cha Biblia ambapo hasidi mkubwa wa Yesu aliyekuwa akiua wanafunzi wake Paulo au Sauli ‘alitokewa na sauti ya Bwana’ akaamua kuslimu na kujiunga na kumfuata Yesu. Chama cha ACT-Wazalendo tunakipongeza kwa ujasiri wake wa kuachana na msimamo ambao ulikuwa hasi hasa pale kilipokaribishwa kujiunga na SUK Visiwani kikaanza kugoma goma na mwisho wake kikaamua kuingia hasa ikizingatiwa kuwa kama si Katiba ya Zanzibar kukibeba, hapakuwa na namna au stahiki ambapo chama kilichoshindwa kingeingia kwenye serikali.

 Kimsingi, kilichofanyika Zanzibar ni kuheshimu Katiba ambayo inatamka wazi kuwa chama kitakachokuwa cha pili kitapewa nafasi ya umakamu wa kwanza wa Rais na viti kwenye Baraza la Mawaziri kulingana na asilimia ya ushindi wa chama husika. Hivyo, kitendo cha awali cha ACT-Wazalendo kukataa mwaliko wa kujiunga na SUK ilikuwa ni kinyume na Katiba. Sasa ACT-Wazalendo wamo ndani, hakuna tena ubishi kuwa wametekeleza matakwa na maagizo ya Katiba ya Zanzibar. Pamoja na yote, tunawapongeza kwa hili. Maana hakuna mgogoro usio na mwisho hasa muamuzi mwenyewe wanapokuwa ni wananchi walioamua kuichagua CCM.

Hata hivyo, kwa upande wa Bara ambapo Katiba ni tofauti na Visiwani iko wazi kuwa chama kitakachoshinda kitaunda serikali bila kulazimika kikatiba na kisheria kuwashirikisha walioshindwa, hali ni tofauti. Kama tulivyoeleza kwenye utangulizi, upinzani, pamoja na kushindwa wazi wazi, bado haujaitambua serikali ya CCM ambacho kilishinda uchaguzi kihalali.

 Wakati ACT-Wazalendo iliyochukua nafasi ya pili Visiwani ishapeleka wateuliwa na wachaguliwa wake, Bara ambako nafasi ya pili ilishikiliwa na CHADEMA, bado wahusika wanavutana. Hadi tunaandika wabunge 19 wa viti maalum waliochaguliwa na Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), licha ya kuamriwa na chama wasishiriki bunge, walitimuliwa uanachama kwa kukubali kuapishwa na Spika wa Bunge kwa mujibu wa sheria. Hii maana yake ni kwamba CHADEMA wameamua kupinga Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) inayotamka wazi kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu ndiye ataunda serikali bila kulazimika kuwakaribisha wapinzani tena walioshindwa kama ilivyo Visiwani ambako Katiba ilifanya hivyo kutokana na mazingira ya huko na migogoro isiyo na mwisho iliyowahi kuleta maafa kule.

Japo kususa kutuma wawakilishi wake ambao wanaona hawakufuata utaratibu ni haki yao kama chama, ila si haki yao kudharau maagizo ya Katiba kama wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na taasisi ya umma ambayo uhalali wake unatoka kwenye Katiba ile ile wanayopinga maelekezo yake kama watashikilia msimamo wa kutotuma watu wake bungeni. Pamoja na kuwapo wanaoona kama kilichotokea Visiwani ni matokeo ya siasa za sura badala ya sera na mvuto wa ulaji kwa wahusika, bado tunawapongeza kwa kukubali maelekezo ya katiba.  Kwani nani asiyetaka ulaji tena kama ni wa dezo kwa mtu au chama kilichoshindwa vibaya?...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com