Chombo hakiendi ikiwa …

26Nov 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Chombo hakiendi ikiwa …

WAHENGA wetu walituachia utajiri wa methali zenye maana na mafunzo. Kwa mfano, “Chombo hakiendi ikiwa kila mtu anajipigia kasia.”

‘Kasia’ ni ubao wa kuendeshea chombo cha bahari kama vile mashua. Ni vigumu chombo cha majini kwenda, kama kila mtu anajipigia upondo (ujiti/mti mrefu au ufito) unaotumika kuendeshea na kuelekeza chombo majini kama vile mtumbwi.

Aidha ni ufito mrefu unaotumika katika shindano la kurukia juu; kuruka kwa upondo; wenzo.

“Bora kujenga madaraja kuliko kujenga kuta.” Maana yake ni afadhali kujenga madaraja ya kuwaunganishia watu kuliko kuta za kuwatenga.

Methali hii hutumiwa kuwaonya watu wasiwe na tabia ya kusababisha utengano au kutoelewana baina ya wenzao. Ni heri kuwaunganisha watu kuliko kuwatenganisha.

Kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha la Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), Ni kawaida Mswahili anapozungumza na wenzake kuipamba lugha yake kwa kutumia tamathali mbali mbali za usemi kama vile tashbihi, tashihisi, istiara, jazanda, methali, misemo au nahau ambazo humjengea uwezo wa kuwa fasaha wa matumizi ya lugha katika mawasiliano yake.

‘Tashbihi’ ni usemi unaofananisha kitu kimoja na kingine kwa kutumia maneno kama vile kama, mithili au sawa.

‘Istiara’ ni matumizi ya neno kwa maana ile isiyokuwa ya msingi; tamathali ya semi inayofananisha viumbe viwili kwa kutumia sifa wanayoweza kuwa nayo.

‘Jazanda’ ni taswira (picha ya jambo inayomjia mtu akilini mwake anaposoma au anaposikiliza maelezo; umbo linalofanana na kiumbe kingine kilichochongwa, lililochongwa au lililofinyangwa.)

‘Methali’ au ‘mithali’ ni maneno ya kiufundi yaliyorithiwa tangu zama za dahari zilizopita katika jamii, na yanasadikiwa kuwa na ukweli, na hutumika kutolea mfano au kufumbia.

Maneno haya yanabeba ujumbe mpana zaidi kimaana kuliko maneno yenyewe yalivyo. Usemi unaowasilisha dhana mbili wenye dhima ya kufunza maadili.

‘Misemo’ ni kundi la maneno ambalo watu katika jamii huyatumia kwa namna mahsusi ili kupata mafunzo mema. ‘Nahau’ ni maneno yanayotumiwa na jamii, ambayo maana zake hazitokani na maana ya msingi ya maneno hayo.

Sasa tuone maneno yatumiwayo na waandishi wa magazeti, na watangazaji wa redio na runinga: “Mwisho wa siku.” Neno ‘mwisho’ ni hali ya kumalizika; ukomo wa jambo; kikomo, hitimisho.

‘Siku’ ni muda wa saa 24 kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa sita usiku. Baada ya muda huo ni siku ingine. Kwa mfano kusema: “Mwaka jana nilijitahidi sana kulima lakini ‘mwisho wa siku’ sikufanikiwa,” si sahihi.

Tatizo lingine ni matumizi sahihi ya neno ‘kwa’. Magazeti na hata wazungumzaji hutumia neno hilo tofauti na maudhui* yake.

*Maudhui ni neno lenye maana mbili tofauti. Kwanza ni wazo kuu linaloelezwa katika kazi ya fasihi. Kwa muktadha huu, maana ya pili ni wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema.

‘Kwa’ ni neno lenye maana nyingi, tofauti na jinsi litumiwavyo siku hizi. Gazeti liliandika hivi: “Hatua ya kuondoka kwa Aussems huku nyuma ndani ya Simba inataka kutumika kama kumpiga teke chura …”

Inapoandikwa “… kuondoka kwa Aussems …” maana yake ni mtu aliyeondoka nyumbani kwa Aussems. Hata hivyo sentensi haikuandikwa ipasavyo. Ingeandikwa:

“Kutokana na Aussems kuondoka, Simba itatumia mwanya huo kumpata m-badala wake na kufanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi.”

Sentensi ingine ikaandikwa pia kwa kutumia neno ‘kwa’ kimakosa: “Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipoulizwa juu ya kuondoka kwa Ausems alisema kikosi kitakuwa chini ya Kitambi na Abel Zrane …”

Ingeandikwa: “Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alipoulizwa kuhusu Aussems kuondoka, alisema timu itakuwa chini ya Kitambi na Abel Zrane …”

‘Kwa’ ni neno linalounganisha sentensi mbili. Neno linalotumika kuhusisha tendo na kifaa kitakachotumika kutendea: “Amelima kwa jembe,” “alikula kwa kijiko; alikula kwa mkono.” Ni kosa kusema “alikula ‘na’ kijiko” au alikula ‘na’ mkono” kwani maana yake ni kwamba “alikula na kijiko pamoja” au “alikula pamoja na mkono wake!”

Vilevile ‘kwa’ ni neno linalotumika kuunganisha vitu viwili katika kulinganisha; neno linalounganisha kitu kimoja na kingine katika utendaji.

Waandishi hushindwa kuandika sentensi kwa mtiririko mzuri: “Bodi ya Simba na hata wanachama na mashabiki wao hawaridhiki na kiwango cha soka kinachopigwa sasa katika timu hiyo na tayari mpango kamili wa kubadilisha sehemu kubwa ya benchi la ufundi hilo inafanyika kwa siri katika kukamilisha kuborwesha timu hiyo.” (Maneno 40 katika sentensi moja isiyoeleweka!)

Ingeandikwa: “Kwa kuwa Bodi ya Simba, wanachama na mashabiki hawaridhishwi na kiwango cha timu yao, benchi la ufundi linarekebishwa ili kuboresha hali hiyo.” (Maneno 22).

“Shepu yazua utata: Kiungo wa Zanzibar, Hafidja Juma Ali, hakucheza mechi ya jana Jumatatu dhidi ya Sudan Kusini kwa sababu jezi ambazo timu hiyo imezivaa zilikuwa zinambana na kumwonyesha maumbile yake kama alivyo.”

‘Shepu’ si Kiswahili bali limetoholewa kutoka Kiingereza, ‘shape’ na maana yake kwa Kiswahili ni umbo/umbile. Mwandishi aliona neno ‘shepu’ ni zuri zaidi ya neno la Kiswahili, yaani ‘umbo!?’

Chini ya kichwa hicho iliandikwa: “Kiungo wa Zanzibar, Hafidja Juma Ali, hakucheza mechi ya jana Jumatatu dhidi ya Sudan Kusini kwa sababu jezi ambazo timu hiyo imezivaa, zilikuwa zinambana na kumwonyesha maumbile yake kama yalivyo.”

Ingeandikwa: “Kiungo wa Zanzibar Queens, Hafidja Juma Ali hakucheza mechi ya jana dhidi ya Sudan Kusini kutokana na jezi kum-bana na kuonesha umbile lake lilivyo.”

[email protected]
0784 334 096