Chonde chonde likizo hii isiwe chanzo cha mimba

12May 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Chonde chonde likizo hii isiwe chanzo cha mimba

MIMBA kwa wanafunzi ni tatizo ambalo halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu, kutokana na kuwapo kwa taarifa mbalimbali za kila uchao zinazoonyesha baadhi yao kukatisha masomo kutokana na changamoto hiyo.

Wanafunzi wanaendelea kukumbana na tatizo hilo linalokatisha ndoto zao , huku serikali na wadau wa elimu wakifanya mikakati mbalimbali ya kuwaondoa wasichana kwenye janga hilo.

Lakini imekuwa ikielezwa na wadau wa kutetea haki za watoto na wanawake kuwa mara nyingi mimba hizo hutokea kipindi ambacho wanafunzi wako likizo, hivyo ni wazi kwamba wazazi wanatakiwa kuwa makini.

Imewahi kutokea hata wilayani Liwale mkoani Lindi mwanzoni mwa mwaka huu baada ya wanafunzi kumaliza likizo ya Desemba mwaka jana na kufanyiwa vipimo na kukuta 13 wakiwa na mimba.

Wanafunzi waliopimwa ni kutoka shule 17 za sekondari zilizomo wilayani humo, ambao sasa ni wazi kwamba wamekatisha masomo kutokana na kukutwa na ujauzito.

Kwa hali hiyo, hata wakati huu wa likizo ya corona, wazazi na walezi wa wanafunzi wanatakiwa kuwa makini katika malezi kwa kutowapa uhuru ambao unaweza kusababisha wakajikuta katika mtego wa kupata mimba.

Si kwamba umakini unatakiwa kuwapo kipindi hiki, hapana, bali ni suala la kuzingatiwa wakati wote ili elimu ya makuzi hasa zama hizi ambazo mmomonyoko wa maadili umekuwa mkubwa katika jamii ipewe kipaumbele.

Ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kutambua kwamba jukumu la kuelimisha mtoto wake kuhusu madhara ya mimba hizo ili aweze kuziepuka, kuliko kumpa uhuru ambao mwisho wake ni tatizo.

Kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kutenga muda kwa ajili ya kutoa elimu ya makuzi kwa watoto wake, akitambua kuwa dunia ya leo imebadilika, hivyo ni muhimu kumsaidia mtoto kwa kila njia ili awe salama.

Hivyo wakati wanafunzi wakiendelea na likizo ya corona ambayo bado haijajulikana itaisha lini, kila mzazi na mlezi atimize wajibu, ili watoto waendelee kuwa salama hadi shule zitakapofunguliwa.

Vinginevyo kama ambavyo inaelezwa na wadau mbalimbali kuwa kuwa likizo nazo zinachangia mimba, basi hata likizo hii ya corona inaweza kusababisha baadhi yao wasirudi shule, kutokana na kupata ujauzito.

Wazazi na walezi wakumbue kuwa zama hizi si za kuona aibu tena, kutokana na ukweli kwamba watoto wa kisasa wanajua mambo mengi mapema, hivyo wakae nao na kuwaambia ukweli kuhusu madhara ya mimba.

Ninatambua kuwa kuna changamoto nyingi zinazochangia mimba za utotoni ukiwamo umaskini, ambao unawafanya watoto washawishiwe kwa kupewa chochote na kujikuta wakishiriki vitendo vya ngono na kupata mimba.

Lakini hali hiyo ya maisha haumzuii mzazi kukaa na mtoto wake na kumwambia kila kitu, kwani hata kama atakuwa mgumu kuelewa, ipo siku atakumbuka kwamba alishaonywa.

Mimba bado ni tatizo kwani katika vyombo vya habari huwa kuna taarifa zinaonyesha wanafunzi wamekatisha masomo kwa sababu ya mimba, hivyo ni kila mzazi na mlezi kutimiza wajibu wake katika malezi.

Elimu ni miongoni mwa haki za msingi za mtoto, hivyo anapokatisha masomo kwa sababu ya mimba anakosa haki hiyo, ndiyo ninasisitiza wazazi na walezi kutenga muda angalau wa nusu saa mara moja kwa siku kwa kukaa na watoto.

Si kukaa tu bali kukaa nao kitako na kuwapa elimu kuhusu madhara ya mimba hizo za utotoni na bahati nzuri watoto wao wapo likizo, kwa hiyo hata wale wanaosoma shule za bweni wapo nyumbani.

Walimu wamekuwa wakijitahidi kuelimisha wanafunzi kwa undani kuhusu mimba kwenye masomo ya bailojia ni vyema wazingatie ili iwasaidie kutambua madhara ya kiafya yanayotokana na mimba za utotoni.

Lakini utoaji wa elimu ya afya ya uzazi na makuzi ni ya muhimu kuanzia nyumbani na hata kwenye jamii nzima ili likizo hiyo iwaepushe wanafunzi na tatizo la corona na mimba za utotoni.