Chonde chonde viongozi staha muhimu

17Jan 2021
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
MADONGO YA MGAGAGIGIKOKO
Chonde chonde viongozi staha muhimu

MNAOKUMBUKA simulizi za zamani, hamtanisahihisha nikikumbuka ile ya Kalumekenge aliyekataa kwenda shule, ikabidi aombwe mbwa amng’ate, ili aende shule.

Mbwa alipokataa kumng’ata Kalumekenge, fimbo aliambiwa ampige mbwa ili amng’ate Kalumekenge na Kalumekenge aende shule. Lakini fimbo naye alikataa kutii amri ile.

Hivyo akaambiwa moto amuunguze fimbo, aliyekataa kumpiga mbwa aliyekataa kumng’ata Kalumekenge, aliyekataa kwenda shule.

Moto alipokataa kumuunguza fimbo aliyekataa kumpiga mbwa aliyekataa kumng’ata Kalumekenge aliyekataa kwenda shule, maji aliombwa amzime moto aliyekataa kumuunguza fimbo, aliyekataa kumpiga mbwa, aliyekataa kumng’ata Kalumekenge aliyekataa kwenda shule.

Tofauti na waliomtangulia, maji alikwenda kumzima moto, naye akaenda kumuunguza fimbo, fimbo akampiga mbwa naye akamng’ata Kalumekenge na hatimaye akaenda shule.

Hizi ni baadhi ya simulizi zilizokuwa na mafunzo kwa jamii kupitia kwa wanafunzi waliokuwa wakisoma vitabu jamii ya Someni Kwa Furaha, na vingine vingi kama vya Alfu Lela Ulela, Mashimo ya Mfalme Suleiman na Hadithi za Adili na Nduguze.

Tukirudi kwa simulizi ya Kalumekenge, tunajifunza jinsi lazima inavyoweza kutumika katika kuhakikisha jambo linafanyika. Amri inavyoweza kutumika kufikiwa jambo.

Nenda, ng’ata, piga, unguza, zima! Hizo ni amri zilizotumika katika sakata hilo la Kalumekenge na dhana nzima ya kwenda shule. Maana yake, Kalumekenge hakuwa anataka shule, lakini nguvu zilitumika hatimaye akaenda.

Hata waliosaidia mpaka Kalumekenge akaenda shule, nao walilazimishwa kufanya hivyo tena kwa vitisho. Kifupi hakukuwa na hiari, hakukuwa na kubembelezana, wala hakukuwa na mazungumzo ya kuleta maridhiano. Lakini hatimaye azma ilifikiwa.

Enzi za vitabu hivyo, zilikuwa za muda mfupi baada ya Wakoloni kuziacha nchi zetu za Afrika, hivyo katika kujenga mataifa mapya, kulikuwa na kusukumana hapa na pale. Pengine elimu ya maneno haikutosha bila mabavu kutumika.

Je, baada ya mataifa haya kupata uhuru, bado kuna haja ya kutumiwa mabavu mtu kwenda kupata jambo jema? Hivi kuna kulazimishana kwenda shule? Kina Kalumekenge bado wapo katika jamii zetu? Bila shaka hapana, kila mtu anajua wajibu, nafasi na fursa aliyonayo katika kujikomboa kama yeye na Taifa lake.

Kama ndivyo, inashangaza kuona wapo watu tena viongozi, wanaodhani kuwa kuna wenzao wana fikra kama za kina Kalumekenge, kwamba bila kusukumwa au kutishwa, hawawezi kufanya kazi.

Naamini tunakosea sana kufikiria hivyo, kwani si nadra siku hizi, kushuhudia kiongozi akimkaripia kiongozi mwenzake hadharani tena mbele ya wadogo zake kikazi, kwa sababu tu kuna jambo halikufanyika inavyotarajiwa.

Utashangaa bila hata kuulizia sababu, kiongozi atafokewa kama mtoto mdogo bila staha, na kujiona mtu asiyestahili kuwa na nafsi aliyonayo. Ilipata kushuhudiwa, Disii akimfokea Mkurugenzi wake hadharani, kisa kuchelewa kufika eneo la tukio.

Ilipata kushuhudiwa Waziri akimfokea hadharani, Mkuu wa chombo cha usalama nchini, kisa kuchelewa tena dakika tano, kufika eneo la tukio na hata kumtimua eneo hilo, bila hata kutaka kusikia kilichomsibu kabla!

Tunasikia sasa wakuu mbalimbali wakitishia wadogo zao wa kazi kuwaweka ndani na hata pengine kuamuru wawekwe ndani, kwa sababu tu kuna jambo limeonekana na mushkeli. Yanafanywa haya bila upande wa pili kusikilizwa na hata ukisikilizwa, hauaminiki!

Hii inafanyika, bila hata kujali tofauti za umri wa mtoa amri na mpokea amri, kwamba hata kama kuna makosa, kuna namna ya kumwambia kaka huyu au dada huyu, au baba au mama, au shangazi au mjomba huyu mbele za watu.

Mbona kuna nyakati Mkuu wa Nchi huonesha staha anapokuwa hata akitaka kumrudi mtu anayemzidi umri? Licha ya kuwa hivyo, lakini kuna wakati hujifikiria kuwa kiumri ni mdogo, hivyo hutafuta jinsi ya kufikisha ujumbe wake. Hatumii ng’ata, piga, unguza au zima. Anatumia saikolojia ya ualimu alionao...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com