Corona itukumbushe malezi ya pembetatu

03Apr 2020
Beatrice Moses
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Corona itukumbushe malezi ya pembetatu

SERIKALI ilitangaza kufunga shule za awali, msingi na sekondari kwa siku 30 kuanzia Machi 17, ikiwa ni sehemu ya kuikabili Corona
Ni hatua ya ghafla, iliyotangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Ni uamuzi ambayo katika mazingira yake, haukuwa na muda wa kujiandaa, hata uongozi wa shule mbalimbali zikiwapo binafsi hawakumudu kutoa kazi za masomo kwa wanafunzi wawapo likizo.

Waziri Mkuu alitangaza hatua, siku moja baada ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutangaza kubainika uwepo wa mgonjwa wa corona nchini hapa.

Ratiba ya kitaifa, ilionyesha wanafunzi wa kidato cha sita walipaswa kuanza mitihani Mei 4, mwaka huu, hivyo wameahidiwa kutangaziwa utaratibu mwingine, kulingana na hali iliyoko nchini.

Kwa kuwa ni hatua ya ghafla, ni wazi uongozi wa shule, wazazi na wanafunzi husika hawakuwa wamejiandaa, hakuna wa kumlaumu, Sote tuna ushuhuda kupitia vyombo vya habari, vikiwano vya kimataifa, corona inavyoathiri hapa kwetu, hadi jana imeshawagusa watu 20, kati yao mmoja kishatangulia mbele ya haki na wawili wamepona.

Nakumbuka siku hiyo, walimu hasa wa shule za bweni, walihaha kuhakikisha wanafunzi wanaondoka kurejea nyumbani kwao wakiwa salama. Wazazi nao walijitahidi kuhakikisha wanatuma nauli kwa watoto wasafiri salama.

Walio hasa katika madarasa ya kujiandaa ana mitihani, kwa maana ya mitihani ya taifa, yaani la nne, saba, kidato cha pili, nne na sita walihitaji kujua hatma ya maandalizi yao.

Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), kwa kushirikiana na asasi ya HakiElimu, walifanya utafiti kati ya Septemba 2003 na Desemba, mwaka 2003 kuhusu maisha na mazingira ya kazi ya walimu katika wilaya saba nchini na walipata mawazo na mtazamo wa walimu kuhusu uhalisia wa maisha yao.

Nikiwa ni miongoni wa wazazi, siku hiyo ya tangazo nilijikuta nakumbuka umuhimu wa malezi ya pembe tatu kwenye sekta ya elimu; mzazi au mlezi, mwalimu na mwanafunzi husika.

Kwani, hayo yote niliyotaja hapo juu yalifanikiwa kwa wazazi walikuwa na ushirikiano mzuri wa walimu, kwa kuwasiliana nao ili kutuma nauli.

Pia, baadhi ya walimu walitambua umuhimu wa kutoa maelekezo kwa wazazi jinsi ya kuwasaidia wanafunzi waliopo kwenye maandalizi ya mitihani ya taifa.

Kutokana na teknolojia ya mawasiliano, baadhi ya shule zina makundi ya mitandao ya kijamii (whatsApp) ilitumika katika kuweka mambo sawa.

Baadhi ya walimu walikumbuka kuhamasisha watoto kujisomea vitabu vya masomo mbalimbali kwa mujibu wa mwongozo wa shule husika, wakizingatia mtaala iliyotolewa na Wizara ya Elimu.

Kuna wazazi au walezi waliopuuza malezi ya pembe tatu, hali inayosababisha usumbufu kwa watoto, kutokana na likizo hiyo ya ghafla.

Wapo ambao hawazingatii maagizo yanayotolewa na walimu, ikiwamo kununua vitabu vinavyohitajika, ambavyo sasa ndiyo vinatumiwa na watoto kujisomea nyumbani.

Wapo ambao wamekuwa na visingizio vya kutokuwa na uwezo (fedha) kununua vitabu hivyo, lakini baadhi yao wakiwafuatilia, ni hodari wa matumizi ya mengine uasiyio na tija.

Wazazi kukwepa malezi ya pembe tatu, ni jambo linalolipigiwa kelele na viongoni wa serikali, hata taasisi binafsi kama CWT na wadau wenza, HakiElimu.

Matokeo ya utafiti yalilenga kuchangia mijadala mbalimbali ya serikali, kuhusu uboreshaji hali ya walimu kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu kinachotolewa nchini.

Utafiti huo, pamoja na mambo mengine uliangalia nyanja zinazochangia ama kuboresha au kudidimiza hali ya maisha na kazi ya walimu, pia mzigo wa kazi ya ufundishaji.

Mengine ni uwiano stahiki wa wanafunzi kwa mwalimu kila mmoja, maendeleo ya walimu kitaalamu katika kufundisha na kujifunza, maisha na walimu maslahi yao,

Ni utafiti huo uliobainisha kuwepo kwa umuhimu wa ushirikiano kati ya shule na wazazi, ni muhimu sana katika kujenga misingi bora ya maendeleo kwa watoto.

Ilibainishwa kuwa, muungano mzuri wa wazazi na walimu, umeweza kukuza maendeleo ya shule kitaaluma katika shule zilizo na ushirikiano wa karibu na wazazi na pale penye wazazi wenye mtazamo tofauti, zimekuwa zikilega kwa miaka mingi.

Kwa hiyo kupitia likizo hii iliyotokana na janga la ugonjwa corona, iwashitue wazazi na walezi waliokuwa mbali na majukumu yao kutoa ushirikiano, wakumbuke majukumu ya msingi, kama vile kununua vitabu vya watoto na kuwasiliana na walimu, wapate taarifa za maendeleo ya watoto zao.