Daladala zisijisahau na ruksa shule katika kukabili corona

02Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Daladala zisijisahau na ruksa shule katika kukabili corona

JUMATATU wiki hii, shule za msingi na sekondari zilifunguliwa ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo, baada ya kukaa nyumbani kwa zaidi ya miezi mitatu, kwa lengo la kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona.

Hiyo ni baada ya serikali kutangaza kwamba, hali ya ugonjwa wa corona imeendelea vizuri na hivyo wameamua kuwaruhusu wanafunzi kurudi shuleni Juni 29, ili vijana na watoto waendelee na masomo.

Pamoja na kuruhusu shule kufunguliwa, msisitizo ukawa ni kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na pia kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wetu wa afya, kwa vile ni muhimu kuzingatia hilo.

Lakini, inaonekana ruhusa hiyo ya serikali imechukuliwa vibaya na baadhi ya makondakta na madereva wa daladala, ambao tangu Juni 29, wamekuwa wakijaza abiria kama zamani kabla ya corona.

Ikumbukwe, Watanzania wanaendelea kusisitiziwa kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa wataalamu wetu wa afya, hasa kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na ukaaji wa 'level seat' katika daladala.

Hatua ya daladala kubeba abiria kwa idadi ya viti 'level seat' ulikuwa ni mkakati wa kupambana na kuenea kwa virusi vya corona. Utaratibu huo ulianza Machi 31 mwaka huu.

Ubebaji huo una changamoto zake, kwani wakati unaanza, kwenye vituo mbalimbali vya daladala, mamia ya abiria walikosa usafiri, daladala nyingi zilifika vituoni, zikiwa zimeshajaa abiria.

Hata hivyo, serikali iliamua kuruhusu magari binafsi kuomba vibali vya muda kwa ajili ya usafirishaji wa abiria na hadi sasa yanaendelea kutoa huduma. Kimsingi, yamesaidia kupunguza mrundakano wa abiria vituoni.

Lakini jambo la kushangaza ni kwamba, tangu shule kufunguliwa, imekuwa kama daladala nazo zimefunguliwa kubeba abiria kupita kiasi kama zamani kabla ya tishio la virusi vya corona.

Yaani wahusika wamejisahau, badala ya kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya yakiwamo ya kukaa umbali wa mita moja, sasa wajazana katika daladala.

Sidhani kama kufunguliwa kwa shule ilikuwa ni ruhusa kwa daladala kuanza kubeba abiria kupita kiasi, kwani pamoja na kuruhusu masomo kuendelea, msisitizo ulikuwa watu kuendelea kuchukua tahadhari.

Hivyo sasa ni vyema wale ambao wamejisahau, wakumbuke kuwa kuna haja ya kuchukua tahadhari na siyo kweli kwamba kufunguliwa shule, kumeenda sambamba na kuruhusu kujaza abiria katika daladala.

Abiria hawana budi kujiongeza na kuacha kujazana, badala yake wachukue tahadhari kwa ajili ya usalama wa afya zao, wakiona daladala imejaa, waachane nayo na kusubiri nyingine.

Ninaamini kwamba wakizingatia utaratibu wa kubeba abiria kulingana na idadi ya viti, huku wakisimamisha wanafunzi wa nne kama, ambavyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliagiza, kutakuwa na usalama.

Kimsingi ni kwamba, jamii isizembee mambo ya msingi kama hayo yanayolenga kulinda afya, vinginevyo ni sawa na kusababisha matatizo na kwamba hakuna tahadhari.

Madereva, makondakta na abiria, kila mmoja azingatie tahadhari iliyotolewa na serikali, kwani itakuwa na faida gani kama watajaza abiria kupita kiasi na mwisho wa siku wakajikuta wameambukizwa corona?

Abiria nao watakuwa na faida gani kutaka kuwahi kwenye shughuli na kulazimika kupanda daladala iliyojaa, halafu mwisho wa siku wajikuta wanaambukizana corona? Chukueni tadhadari!

Ni kweli, maisha lazima yarudi na yaendelee kama yalivyokuwa zamani, lakini kuchukua tahadhari ni jambo la muhimu kwa mustakabali wa afya ya kila mmoja wetu, kuliko kujiendea kienyeji tu.

Kama wahusika watashindwa kujiongeza, ili kuzingatia tahadhari, basi wahusika askari Polisi, Trafiki, waingilie kati kukamata daladala zilizosimamisha abiria na kuwashusha kwa lengo la kuendelea kudhibiti kuenea virusi vya corona.

Wakishushwa huku madereva na makondakta wakichukuliwa hatua zaidi za kisheria, hatua hiyo inaweza kusaidia kuendelea kupunguza kama siyo kumaliza kabisa tishio la virusi, hivyo kwenye usafiri.