Damu ni nzito kuliko maji

16Mar 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Damu ni nzito kuliko maji

HATUWEZI kulinganisha damu na maji. Hii ni methali ya kutufunza kuwa uhusiano wa kidamu ni muhimu sana. Aidha, watu wa nchi moja ni ndugu wanaotofautiana kwa silika (mwenendo, tabia na haiba anayozaliwa nayo mtu na kukua nayo) na watu wa nchi zingine.

Leo jioni Yanga inayoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu 20 zinazoshiriki, itapambana na Lipuli FC ya Iringa kwenye Uwanja wa Samora. Lipuli ipo nafasi ya tano kutoka juu. Baadaye usiku wa leo, Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba SC watatoana jasho na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) jijini Dar es Salaam.

Ni mechi ya kufa au kupona kwa timu zote mbili, huku zikisubiri matokeo ya Al Ahly ya Misri dhidi ya JS Saoura ya Algeria ili kujua itakayosonga mbele. Al Ahly kwao iliifunga Simba mabao 5-0 na Simba kulipa kisasi kwa ushindi wa 1-0 jijini. JS Saoura ilifungwa mabao 3-0 na Simba Dar es Salaam lakini kwao wakaifunga Simba magoli 2-0. Ndivyo yalivyo maajabu ya kandanda.

Simba na AS Vita zilipopambana Kinshasa, DRC, Simba iliadhibiwa na wenyeji kwa kufungwa mabao 5-0. Ndo yale yaliyosemwa na wahenga kuwa “Mgeni aje mwenyeji apone.” Maana yake kila mgeni afikapo nyumbani, wenyeji hufaidika kwa kula chakula kizuri.

Kama ndivyo, Simba ambao ndiwo wenyeji, na wenye shauku (hamu kubwa ya ushindi) watatumia fursa hiyo kutufurahisha kwa kuwashinda wageni na kuwanyamazisha wasioitakia mema? Ndio, kwani mcheza kwao hutuzwa.

Simba na Yanga zaitwa ‘watani wa jadi’ ingawa vitendo vyao ni tofauti na maana ya maneno hayo. ‘Watani’ aghalabu ni watu wa makabila tofauti au marafiki wakubwa ambao hufanyiana masihara kwa mujibu wa mila zao pasi na anayetaniwa kukasirika. Mambo wanayofanyiana Simba na Yanga si utani bali ni chuki yaani hisia ya kutopenda maendeleo ya mwengine. Khaa! (tamko la kuonesha kukasirika au dharau).

Watu wa nchi na jiji moja kuchukiana kiasi hicho ni ujuha. Yaonesha jinsi tulivyo na uwezo mdogo wa kufikiri au kuelewa mambo; wapumbavu, wajinga, mabwege! Hali hii itatupeleka wapi zaidi ya timu zetu kuwa ‘jamvi la wageni?’ Kila timu itakayokuja nchini itatushinda na sisi tukishangilia kwa kuchekana na kuzomeana!

Nauliza tu, ingawa wenzangu wa Jangwani watadhani mimi ni mpenzi wa jamaa wa mtaa wenye pilikapilika nyingi kuliko Jangwani penye ukame; na mvua zinyeshapo huwa kwenye hekaheka za kupambana na mafuriko!

Hivi kama Simba au Yanga ikitwaa ubingwa wa Afrika, sifa huwa Msimbazi na Jangwani tu au ni kwa nchi nzima ya Tanzania na pia Afrika Mashariki? Kwa nini tusisaidiane ili nchi yetu ifikie hatua hiyo kama zilivyo nchi za wenzetu? Kwa nini tumekuwa na tabia ya kuzishangilia timu ngeni zinapotushinda? Hatuoni kuwa tunajitukanisha kwa wenzetu?

Twajua timu hizi ziitwazo “watani wa jadi” huhasimiana kila mara, hasa zinaposhiriki mechi za kimataifa. Utani hauwi hivyo ila ni uhasama usiokuwa na sababu. Eti wengine wanasema ni kulipiza kisasi kwa sababu hata wao wakishiriki michezo ya kimataifa, timu ngeni hushangiliwa sana, hasa zinaposhinda. Ebo! Nduguyo anapigwa wewe washangilia? Kinachotufanya tushangilie ni kitu gani kama si kuwaonesha wageni jinsi tunavyotawaliwa na ujinga? Aibu!

‘Bendera’ ni kitambaa chenye rangi au nembo maalumu kinachotambulisha nchi, shirika, chama au jumuiya fulani. Ndo maana timu zinapocheza mechi za kimataifa kama hii ya leo usiku kati ya Simba na AS Vita ya DRC, uwanjani kutakuwa na bendera mbili rasmi zitakazopepea milingotini.

Bendera ya Taifa (Tanzania) ni kwa ajili ya Simba na Bendera ya DRC ni kwa ajili ya AS Vita wanaoiwakilisha nchi hiyo. Ndo maana mashindano ya kimataifa, nyimbo za taifa za nchi zinazoshiriki huimbwa na watu husimama kuonesha heshima. Hata kama wapenzi wa timu hizo watakuwa na bendera za timu zao na kuzipeperusha, hazithaminiwi.

“Ombeni nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtaona, bisheni nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea, naye atafutaye huona, naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki atampa nyoka? Basi kiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je, si zaidi Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

(Mathayo 7:7-11)
[email protected]
0784 334 096