Dhana ya chama kwanza isiingizwe Bungeni

07Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Dhana ya chama kwanza isiingizwe Bungeni

NIANZE kwa kuelezea kidogo maana ya neno uzalendo; kwamba ni hali ya mtu kuipenda na kuithamini nchi yake na kuweka maslahi ya taifa lake hilo mbele. Neno hili ni dogo lakini maana inayobebwa na neno uzalendo ni kubwa.

Kutozingatia ama kutokuwa na elimu ya uzalendo kumekuwa kukisababisha baadhi ya watu kutenda mambo yanayoshangaza wengine na kuwaacha katika mfadhaiko wa kujiuliza kama huyu mtu anaipenda nchi yake ama la. Nina uhakika kwamba wengi mtakuwa mashahidi kwamba hapa nchini baadhi ya masuala yenye manufaa kwa jamii yamekuwa yakienda mrama, lakini wanapojitokeza watu kwa ajili ya kukemea hali hiyo wamekuwa wakipingwa vikali. Mfano mzuri ni yale ambayo tumekuwa tukiyashuhudia bungeni ambako wabunge hunyukana, hasa wanapojadili hoja zenye maslahi kwa umma wa Watanzania. Ni kweli watu hawawezi kukubaliana kila jambo, lakini yapo ambayo ukiyasikia utagundua kuna watu wameweka uzalendo pembeni na kukumbatia maslahi ya vyama vyao. Hali hii imenifanya nikumbe kauli aliyowahi kuitoa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye wakati akihojiwa na gazeti moja mwaka 2008 aliposema siasa ni utumishi kwa umma, na katika hilo anaamini katika uzalendo kwa nchi kwanza kisha chama baadaye. Alisema: "Tunakuwa na nchi kwanza tunayotaka kuijenga, ndipo tunaunda chama cha kujenga nchi tunayoitaka, kwa hiyo uzalendo kwa nchi unapaswa kuvuka mipaka ya itikadi zetu." Wakati anatoa kauli hiyo ambayo binafsi ninaunga mkono, Nape alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), kabla ya kushika nyadhifa alizonazo kwa sasa ndani ya CCM na serikali yake. Kilikuwa ni kipindi ambacho Nape alikuwa ametofautiana na Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya chama hicho (UVCCM) kutokana na kuukosoa hadharani mradi wa jengo la Makao Makuu ya umoja huo. Lengo langu siyo kuzungumzia kadhia hiyo kati ya Nape na vijana wa chama chake, bali ni kujadili dhana ya chama kwanza taifa baadaye ambayo, binafsi, naona haipaswi kupewa nafasi zaidi ya maslahi ya umma. Ni dhana potofu ambayo imesababisha sasa baadhi ya wabunge kugeuka watetezi wa vyama badala ya maslahi ya umma. Tumekuwa tukishuhudia mvutano mkali kwenye baadhi ya vikao vya Bunge wakati wabunge wanapojadili hoja mbalimbali huku kila upande ukivutia kwake na kuacha kutetea maslahi ya wengi. Kuna mifano mingi, lakini mojawapo ni vikao vya Bunge la 11 vilivyomalizika juzi mjini Dodoma, ambapo Watanzania walishuhudia mvutano mkali wenye msingi wa uchama wakati wa uwasilishaji wa 'Mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021'. Wabunge wa upinzani walidai kuwa Kanuni za Bunge na Katiba vilikiukwa kwa serikali kuwasilisha 'Mapendekezo ya Mpango' badala ya 'Mpango' halisi. Lakini wenzao wa CCM walipinga na kusema hakuna kilichokiukwa na hivyo kuwafanya wananchi washindwe kuelewa ukweli uko wapi. Baada ya mvutano mkali, kwa hekima Kamati ya Uendeshaji ya Bunge iligundua kuwa wapizani walikuwa sahihi na kuishauri serikali kutoa hoja ya kutengua kanuni ili kuweka mambo sawa. Nashindwa kuelewa ni kwa nini Wabunge wa CCM waliamua kuvutana wakati wakijua ukweli ulipo kwenye sakata hilo. Mimi ninaamini kuwa kama wabunge wangezingatia kauli ya Nape kwamba siasa ni utumishi kwa umma, na katika hilo uzalendo unatakuwa kuwekwa mbele na vyama vyao baadaye, yasingetokea hayo. Lakini bahati mbaya baadhi yao wametekwa na dhana ya chama kwanza mtu baadaye, hivyo wako tayari kutetea jambo ambalo wanaona lina maslahi kwa chama badala ya wale waliowachagua! Nadhani umefika wakati sasa dhana ya chama kwanza isipewe nafasi Bungeni na badala yake uzingatiwe uzalendo, hasa kwa kuzingatia kwamba wabunge wote bila kujali itikadi za vyama vyao wanataka kujenga nyumba moja ambayo ni Tanzania.