Diplomasia ya uchumi itilie mkazo bidhaa ya mkulima

02Aug 2019
Reubeni Lumbagala
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Diplomasia ya uchumi itilie mkazo bidhaa ya mkulima

WAKULIMA wa mazao ya chakula na biashara na wazalishaji malighafi viwandani, wana nafasi kubwa kuongeza mauzo yao na hatimaye kuwa milionea, kama masoko ya uhakika yatafanyiwa kazi kikamilifu.

Uzalishaji bidhaa za kilimo na viwandani, bila ya kuwapo masoko ya uhakika, ni hasara kwa wazalishaji.

Kilimo ndicho kinawaajiri Watanzania wengi, pia ndio uti wa  mgongo wa uchumi kitaifa. Hivyo, hakuna namna wawekezaji viwandani wanaweza kubadili maisha kwa kupitia faida ya jasho lao, kama masoko ya bidhaa yatasuasua.

Ni vyema kumkwamua mkulima mdogo nchini, jambo linalowezekana kupitia wawekezaji viwandani kuandaa mazingira ya kuuza mazao yao kwa bei nzuri, inayoendana na uhalisia sokoni.

Juhudi za ukuzaji uchumi duniani zinachagizwa na diplomasia ya uchumi, inayokuza ushirikiano baina ya nchi moja na nyingine.

Diplomasia ya uchumi ni ushirikiano kati ya nchi moja na nyingine katika ukuzaji  uchumi kwa maslahi ya wanaoshirikiana. Ni faraja kuona Tanzania haiko nyuma katika maendeleo ya viwanda na ukuzaji uchumi wake.

Zipo juhudi zinazofanywa na serikali kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchini, kuwekeza katika sekta mbalimbali hasa kilimo, viwanda na huduma nyingine za kijamii.

Ni juhudi zilizozaa matunda, kwani wawekezaji wamevutiwa kuwekeza nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi wetu.

Eneo jingine la upatikanaji wa masoko kwa mazao na bidhaa kutoka Tanzania, ambayo juhudi za makusudi zinapaswa kuongezwa kusaidia maendeleo ya kilimo, viwanda na ukuaji uchumi.

Viongozi serikalini na wananchi wanapaswa kutoishia kuonyesha maeneo ya uwekezaji. Ni wakati wa kujikita kutangaza mazao na bidhaa zinazozalishwa, ili kupata soko la uhakika na kuongeza uzalishaji.

Tanzania imebarikiwa ardhi ya kutosha na nzuri, iliyojaa rutuba kwa mazao ya chakula na biashara kuzalishwa kwa wingi.

Nitatoa mifano ya mahindi, ufuta, alizeti, maharage, mbaazi, mawese, matunda, mboga, viazi, chai, katani, kahawa, korosho, pamba  zinazozalishwa kwa wingi.

Viwanda vyetu zinazalisha bidhaa bora zinazomudu vigezo vya ushindani katika masoko kitaifa na kimataifa,  yayohitaji masoko ya uhakika, ili wakulima wafaidi jasho na mitaji waliyowekeza.

Ni wakati sahihi, balozi zetu katika mataifa mbalimbali kutangaza na kutafuta masoko ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mabalozi wajibu wao ni kuwa  viungo wa wakulima na wazalishaji nchini na wanunuzi waliopo katika nchi waliko, ili upatikanaji masoko ya uhakika kwa mazao na bidhaa nchini, liwe jambo halisi.

Kila balozi anapaswa kuwa na deni la kuhakikisha anafanya kila linalowezekana, wakulima na wawekezaji wanazalisha bidhaa kutoka Tanzania, ili kuboresha maisha ya wananchi husika.

Bidhaa na mazao yanayozalishwa nchini, yanahitajika sana katika nchi mbalimbali duniani, lakini tatizo linaodumu ni kushindwa kuyachangamkia masoko.

Ulimwengu wa sasa ni wa ushindani katika kila jambo. Watanzania hatupaswi kujifungia kusubiri masoko yatafute, bali sisi ndio kuyatafuta masoko.

Mkulima kijijini kabisa, ukimwambia changamkia soko la mbaazi lililoko India, ni kumchanganya zaidi, kwani atashindwa kujua aanzie wapi na pa kuishia nako kufanikisha  kuiuza mbaazi yake India.

Serikali kupitia balozi zetu zitakapoandaa taratibu nzuri wa namna ya wakulima watakavyouza mbaazi zao India, itakuwa rahisi wakulima kufanikisha hayo.

Mabalozi wetu wanaandaa mikutano ya kuonana na wafanyabiashara na wanunuzi wa mazao na bidhaa, ili kutangaza fursa za mazao na bidhaa kutoka Tanzania.

Hakuna sababu Tanzania kuwa watazamaji wa masoko ya uhakika yaliyopo nje ya nchi, wakati tuna vigezo vya kuchuana.

Diplomasia ya uchumi inapaswa kutumika kikamilifu, kubadili maisha ya shambani. Jambo muhimu ni kuzingatia wakulima kuzalisha mazao na bidhaa bora zinazokidhi viwango kimataifa.

Tanzania ya Viwanda kusonga katika safari ya uchumi wa kati na ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 inawezekana kama diplomasia ya uchumi itajikita kutafuta masoko kuwasaidia wakulima wasilanguliwe mazao yao.

Bado naamini nchini, mkulima akiinuka, hapana shaka uchumi wa nchi utakuwa kwa kasi.