Dk. Mashinji atafuta dhana ya ukanda Chadema?

15Mar 2016
Leonce Zimbandu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Dk. Mashinji atafuta dhana ya ukanda Chadema?

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepata Katibu Mkuu mpya, Dk. Vicent Mashinji, ambaye ameziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Willibrod Slaa, aliyejiuzulu nafasi hiyo Julai 30, mwaka jana.

Dk Slaa alijiuzulu kutokana na kile alichoeleza kuwa ni utaratibu kutofuatwa wa kumkaribisha Edward Lowassa, aliyehamia katika chama hicho kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ingawa kuteuliwa kwake kumepokelewa kwa mtazamo tofauti kwa vile hana jina kubwa katika ulingo wa siasa, lakini inaelezwa kuwa ni miongoni mwa watu waliofanikisha mikakati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupata wabunge wengi kuchaguliwa.

Inalezwa kuwa Dk. Mashinji alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Sera na Wanataaluma wa Ukawa, ambao waliandaa Ilani ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Baada ya kuteuliwa, katibu huyo alitaja vipaumbele vitano ambavyo ataanza navyo atakapotinga ofisini ili kuhakikisha Chadema inafanikiwa kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, ikiwamo kukipeleka chama hadi kwa wananchi wa kawaida.

Zipo vipaumbele vingi ambavyo Dk. Mashinji alikaririwa na vyombo vya habari akivitaja, lakini kipo kimoja ambacho ningemuongezea ili kisaidie kufuta dhana ya ukanda ambayo imejengeka miongoni mwa Watanzania.

Ninasema hivyo kwa sababu baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakidai kuwa Chadema ni chama cha ukanda, hivyo Watanzania wanapaswa kuwa mbali nacho kwa vile hakilengi kuwaunganisha.

Dhana hii ilipata nguvu zaidi kutokana na ukweli kwamba viongozi wakuu kuanzia kwa mwenyekiti wa taifa na katibu wake walikuwa wanatokea ukanda mmoja, hivyo hali hiyo ikawapa upenyo baadhi ya watu kueneza propaganda kwamba ni chama cha ukanda.

Hivyo hii ni nafasi ya pekee kwa katibu mpya kuliona hilo na kulifanyia kazi na kuhakikisha anazika dhana hiyo kwa kuwaunganisha Watanzania wote hasa kutokana na ukweli kwamba yeye hatoki kwenye ukanda uliokuwa ukilalamikiwa.

Kwa maana hiyo anatakiwa kufanya kubwa ili kuwathibitishia Watanzania wote kwamba Chadema hakina itikadi za ukanda.

Ahakikishe anaondoa dhana hiyo na aseme ndio maana akateuliwa kushika nafasi hiyo kubwa ndani ya Chadema akitokea nje ya kanda ya kaskazini.

Akifanya hivyo atakuwa amepiga hatua kubwa ya kukisogeza chama kwenda mbele kwani ndani ya mazingira ya propaganda kama hayo inawezekana wapo baadhi ya wanachama waliokata tamaa.

Hao wanatakiwa kurudishwa katika chama ili waendelee na siasa kama kawaida, kwani dhana iliyokuwa imejengwa vichwani mwao imeondolewa kwa kuteuliwa kiongozi mkubwa asiyetoka kule walikokuwa wakilalamikia.

Ikumbukwe kwamba kwenye siasa hazikosekani siasa za majitaka, ambazo zinaweza kusababisha chama kikasambaratika kwa sababu tu ya uzushi ama namna nyingine ya kukinyima nguvu.

Kwa wale wanaofuatilia siasa za hapa nchini watakuwa wanakumbuka kwamba mbali na tuhuma za ukanda, chama hicho kimekuwa kikidaiwa kuwa cha ukoo, hivyo hayo yote katibu huyo anatakiwa kuyafanyia kazi.

Ni kweli kwamba yapo mambo mengi ya msingi ambayo Dk. Mashinji anajiandaa kuyafanyia kazi, lakini hili la kuwaunganisha wanachama kwa kuwaondolea dhana ya ukanda na ukoo litawasaidia kuwa kitu kimoja.

Akichukua hatua hizo atasaidia kuwafanya wanachama wake watambue kwamba chama ni mali yao na sio cha watu wa ukanda fulani ama ukoo fulani kama ambavyo wamekuwa wakiaminishwa na wanaoeneza siasa za majitaka.

Kwa sasa imekuwa ni jambo la kawaida kuwasikia watu mitaani wakisema kuwa Chadema ni chama cha ukanda fulani, wanasema hivyo kwa sababu walishahakikishiwa kwamba ndivyo ilivyo.

Binafsi sina uhakika hilo, lakini cha msingi ni kwamba katibu mpya afuatilie kwa karibu ili kubaini ukweli kwa jambo hilo mapema na kama lina ukweli ndani yake, basi alifanyie kazi na pia kama ni la uzushi, basi awaunganishe upya wanachama wake.