Dodoma FC isipande Ligi Kuu Bara kisiasa

13Jul 2020
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Dodoma FC isipande Ligi Kuu Bara kisiasa

HATIMAYE Dodoma Jiji FC ya jijini Dodoma imepanda daraja na msimu ujao wa 2020/21, itashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dodoma Jiji iliyokuwa kwenye Kundi A, sasa inaungana na Gwambina FC ya Misungwi jijini Mwanza moja kwa moja kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Hii si mara ya kwanza kwa mkoa wa Dodoma kupata timu itakayocheza Ligi Kuu, ingawa ni kwa muda mrefu sasa imekuwa haina timu inayocheza kwenye hatua hiyo ya juu.

Katikati ya miaka ya 70, hadi katikati ya miaka ya '80, kulikuwa na timu mbili zilizopishana vipindi zikicheza Ligi Kuu kutoka mkoa huo, nazo ni Waziri Mkuu na CDA.

Timu hizo zilitoa wachezaji wengi wazuri baadhi yao wakiwa ni Justine Simfukwe, Charles Mngodo, Mkala Maulidi, Daniel Poka, Makwa Selemani, Mtemi Ramadhani na Lila Shomari. Kati ya hao, Lila na Mtemi waliwahi pia kuichezea Simba baada ya kutoka hapo.

Ni heshima kubwa kwa Jiji la Dodoma, ambako ndiyo Makao Makuu ya Tanzania kuwa na timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, wakati huo mashabiki wa soka nchini wakisubiri kwa hamu kukamilika kwa uwanja mkubwa wa kisasa.

Siku ya Jumamosi niliwasikia mashabiki wa timu ya Dodoma Jiji wakishangilia kwa nguvu, timu yao kupanda Ligi Kuu baada ya kuichapa Iringa United mabao 2-0.

Baadhi ya wachezaji wake ambao ni wazoefu wa Ligi Kuu ni Emmanuel Mseja ambaye alishawahi kuichezea Mbao FC na Simba. Ni baada ya kutoka Simba ndipo alipokwenda Dodoma Jiji.

Wengine ni Mcha Hamisi aliyekuwa Azam FC, Lipuli na Ruvu Shooting na ndiye aliyefunga bao la kwanza kwenye mechi hiyo.

Wakati shamrashamra za Wanadodoma Jiji ziliendelea, baadhi ya mashabiki wa soka bado wanajiuliza maswali.

Ni kwamba Dodoma Jiji FC imepanda Ligi Kuu kuja kuleta ushindani au kwa sababu za kisiasa tu, kwa sababu tayari jiji hilo limeshatangazwa rasmi kuwa makao makuu na shughuli za kiserikali zimeshahamia huko?

Wana haki ya kujiuliza hivyo. Na hata mimi najiuliza hivyo. Isije kuwa timu inapanda tu kwa sababu za serikali ya jiji hilo ilifanya kila njia ili jiji hilo nalo lipate timu ya Ligi Kuu tu basi na badala ya hapo hakuna chochote kinachoendelea.

Tumeona baadhi ya timu nyingi zikipanda Ligi Kuu kwa sababu kama hizo, tena kwa mbwembwe nyingi, lakini zikifika Ligi Kuu zinatelekezwa na kuanza kulia njaa.

Mashabiki wengi wa soka nchini wanapenda zaidi timu zenye uchumi mzuri ndiyo zipande, ili ziende kuleta chachu na ushindani wa kweli ili ligi iwe ngumu, isiyotabirika na isiyokuwa na timu dhaifu kwa sababu tu ya uchumi.

Ndiyo maana wengi waliitaka Gwambina FC ipande kwa sababu inaonekana kuwa iko vizuri kiuchumi. Ni timu ambayo tangu iko Ligi Daraja la Kwanza ilionekana kabisa haina njaa.

Kwenye Kundi A, mashabiki wengi wa soka walionekana kuipigia debe zaidi Ihefu FC ipande kwa sababu tu imeonekana kuwa na uchumi mzuri kutokana na kumilikiwa na wakulima wakubwa wa mpunga, wakichanganyika na wafanyabiashara wa zao hilo.

Kwa bahati mbaya sana, Ihefu imeangukia kwenye mechi za mchujo na Dodoma Jiji FC imepanda kwa nguvu zake na uwezo wa wachezaji wake.

Sasa ili kuwathibitishia mashabiki kuwa hajaipandisha timu hiyo kisiasa, viongozi wa jiji hilo baada ya kumaliza kushangilia wajue wana jukumu zito la kuitunza timu hiyo, kuingia mifukoni, kusaka wadhamini na kutafuta pesa za kusajili wachezaji wazuri, wazoefu na wenye uwezo wa kupambana katika Ligi Kuu.

Hatutarajii timu ya Dodoma Jiji baada ya kupanda, basi waachiwe tu viongozi wa timu pekee, baadaye waanze kulia njaa na kutembeza bakuli kwa wananchi na wabunge.

Hii itakuwa ni aibu, na baadhi ya mashabiki wa soka wataanza kuhoji nguvu zilizotumika kuipandisha timu hiyo, halafu inaachwa ikiwa hoi.

Tunaitaka Dodoma Jiji FC iwe na makali, uwezo na wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu, pamoja na uchumi usiotetereka kama ilivyokuwa timu za Waziri Mkuu na CDA.