Elimu bado muhimu kuelekea marufuku mifuko ya plastiki

29May 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu bado muhimu kuelekea marufuku mifuko ya plastiki

JULAI Mosi imekaribia ambayo ni tarehe rasmi ya mwisho iliyowekwa na serikali ya kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki nchini.

Wazalishaji na wauzaji wa mifuko hiyo walipewa mwezi mmoja kusambaza mzigo walio nao, kama ilivyo kwa watumiaji wengine kwa maana ya wenye maduka.

Nao wanatakiwa kuhakikisha hawaendelei kutumia wala kusambaza mifuko hiyo baada ya muda wa huruma wa mwezi mmoja uliotolewa kumalizika.

Hatua hii ya serikali ni nzuri kwani inakwenda kuyaokoa mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Hiyo ni kwa sababu kiasi cha mifuko ama plastiki inayokwenda ardhini karibu kila siku itapungua au kwisha kabisa.

Hata hivyo, changamoto anayoiona Muungwana kuelekea siku hiyo ni ile ya kutokuwapo kwa mifuko mbadala ya kutosha kwa ajili ya mahitaji ya wateja wanapokwenda dukani ama sokoni kununua mahitaji mbalimbali.

Hii ni kwa sababu wauzaji wa maduka ya kawaida wanatumia mifuko hii ya plastiki inayopigwa marufuku kwa ajili ya kuwekea wateja wao bidhaa wanazonunua, iwe ni unga, sukari au chochote.

Pamoja na hatua njema zinazoendelea kuchukuliwa, wasiwasi wa Muungwana ni ukweli kwamba bado mifuko mbadala haijasambazwa kwenye maduka ya jumla ili wauzaji wa kawaida waipate.

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, aliwatahadharisha viongozi wa serikali za mitaa dhidi ya matumizi ya nguvu kwa wananchi watakaokutwa wanatumia mifuko ya plastiki.

Ni tahadhari nzuri kwa kuwa ipo mifano ya viongozi wa ngazi hiyo wakiwatumia mgambo wa halmashauri, manispaa na majiji kutumia nguvu dhidi ya wananchi.

Mathalani, ni katika zoezi la kukabili wanaotupa takataka ovyo ambapo zilitumika nguvu kupita kiasi, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kujeruhiwa kutokana na vipigo.

Si mgambo tu kwani hata vijana waliopelekwa kwenye mitaa mbalimbali nao wanadaiwa kujichukulia sheria mkononi pamoja na kuwapo sheria za kushughulikia jambo hilo.

Tahadhari iliyotolewa na waziri ni muhimu kuzingatiwa tukichukulia uzoefu wa matukio ya nyuma.

Kwamba wapo watakaogeuza operesheni hiyo mtaji wa kujipatia kipato.

Sheria imetaja kiwango cha faini atachachotozwa mhusika, lakini upo utaratibu wa kutoza na si kila anayekamata anastahili kutoza faini mfano mgambo.

Muungwana ana rai kwamba wakati jitihada za kutoa elimu na tahadhari kuhusiana na marufuku hii zikiendelea kwa kasi inayotakiwa, ni vyema kwa upande mwingine kasi ya kutengeneza mifuko mbadala nayo ikaendelea.

Lakini pia kuisambaza kwa watumiaji wa jumla na rejareja ili kuondoa mkanganyiko.

Kwa kufuata mfano wa Zanzibar na Kenya, kuwe na utaratibu wa kuwaelimisha wananchi kupitia vikao vya serikali za mitaa na vijiji, au kwenye maeneo yote ya huduma za kijamii kama hospitali na shuleni.

Muungwana anatarajia kuona picha, video fupifupi zikielimisha wananchi juu ya mifuko inayotakiwa ili kunapotokea mwananchi amekamatwa aweze kujitetea.

Vilevile uonevu unaweza kujitokeza kwa wafanyabiashara wenye maduka kwa sababu ya kukutwa tu na bidhaa zilizotoka viwandani ambazo hufungwa nailoni badala ya maboksi.

Katika hali kama hii ni wazi kwamba mtumiaji wa mwisho ambaye ndiye muuzaji anaweza akakutwa na mfuko wa plastiki ambao umeshapigwa marufuku na kukamatwa.

Ndipo panapojitokeza umuhimu wa kukagua viwanda vya kuzalisha plastiki na viwanda vinavyofunga bidhaa kwa plastiki.

Eneo lingine ni kwenye viwanja vya ndege ambapo baadhi ya wasafiri hufunga mizigo yao kwa kutumia nailoni maalum.

Hivyo basi kuna umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kupitia mitandao ya kijamii, kama vile Instagram, Facebook, WhatsApp, Twitter unapojitokeza ili ujumbe usambae kwa haraka.