Elimu hii inatibu kutokujua kusoma wala kuandika  

13Jul 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu hii inatibu kutokujua kusoma wala kuandika  

ELIMU ya awali ni hatua ya mwanzo ya kumjengea mtoto uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Ni mwanzo ili hata anapoanza ngazi ya pili awe na msingi wa kumwezesha kufanya vizuri zaidi katika masomo baada ya kujua mazingira.

Umuhimu wa elimu hiyo, unawalazimu wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika hatua hiyo ya awali, kabla ya kuendelea na shule ya msingi.

Kutokana na umuhimu wa elimu ya awali, serikali imeelekeza kila shule ya msingi kuwa na darasa la elimu hiyo, ili watoto wote ambao hawajafikia umri wa kuanza darasa la kwanza, waanzie 'kupikwa' huko.

Hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza idadi ya wasiojua kusoma na kuandika, kwani  watakuwa wamepata msingi bora tangu awali kuliko kujifunza wanapoamza darasa la kwanza.

Serikali imebeba jukumu la kutoa elimu bure tangu shule za awali hadi sekondari, hivyo kama wataendelea kuwapo wazazi na walezi wasioona umuhimu wa elimu, wanaweza kuharibu ndoto za watoto wao.

Ikumbukwe Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) hususani katika lengo namba 4 la elimu, hivyo ni muhimu jamii kusaidiana na serikali kusimamia na kutimiza lengo hilo kwa kishindo.

Malengo hayo yanayofikiwa mwaka 2030, yanagusa mambo mengi ikiwamo ubora wa elimu, ikiwa ni kujenga na kuboresha miundombinu ambayo itachangia mazingira bora ya kujifunza kwa watoto kwa wote.

Inaelezwa kuwa katika nchi maskini duniani, watoto na vijana wenye umri wa kwenda shule, hukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo watoto wa kike kutokwenda shule kwa sababu nyingi ikiwamo ndoa za kulazimishwa.

Vilevile wanaoishi na ulemavu hukwama kwenda shule kwa sababu ya ukosefu wa miundombinu toshelevu kwa mahitaji yao na hata wale wanaokwenda hukabiliwa na mazingira duni ya kusoma.

Ni vyema kila mzazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata elimu ya awali kwa kuwaondolea vikwazo ambavyo husababisha wasipate msingi huo muhimu.

Ikumbukwe kuwapo darasa la elimu ya awali kunasaidia watoto kuanza elimu ya  msingi wakiwa tayari wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu, kuliko kuwaacha walivyo na kujikuta wakiwa 'mbumbumbu' wanapoingia la kwanza.

Mtoto kuhitimu darasa la saba bila kujua kusoma na kuandika, ni matokeo ya kutoanzishwa elimu ya awali ambayo ni msingi bora kwake unaompa uelewa mapema kabla kuanza elimu ya msingi.

Wazazi na walezi wakumbuke kuwa, uhaba wa madarasa katika shule za serikali, unasababisha wanafunzi kurundikana katika chumba kimoja na kuufanya ufundishaji na ujifunzaji kuwa mgumu.

Kwa mazingira kama hayo, si rahisi mwalimu kumfikia kila mwanafunzi ama wanafunzi wote kumuelewa, hivyo wale ambao watakuwa hawajapitia elimu ya awali wanaweza wasijue kusoma na kuandika hadi wanahitimu darasa la saba.

Katika elimu ya awali, mwalimu unapaswa kumwezesha mtoto kujenga umahiri kupitia shughuli zilizobainishwa, mbinu, zana stahiki za kufundishia na kujifunzia na kupima maendeleo ya mtoto hatua kwa hatua.

Hayo ni baadhi ya yaliyomo kwenye mwongozo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambayo imeandaa Mtaala na Muhtasari wa Elimu ya Awali ambao unalenga kuwajengea watoto umahiri uliokusudiwa.

Mwongozo huo unatoa maelezo kuhusu uchambuzi wa mtaala na ujifunzaji na ufundishaji katika elimu ya awali.

Aidha, unahusu upimaji wa maendeleo ya elimu ya mtoto wa awali na pia huwapatia walimu maelezo kuhusu maandalizi ya ufundishaji na namna ya kuwezesha ujenzi wa umahiri ambao mtoto wa elimu ya awali anastahili kuujenga.