Elimu kuhusu presha ya macho ni muhimu

19Nov 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu kuhusu presha ya macho ni muhimu

TANZANIA inakadiriwa kuwa na watu milioni 1.7 wenye matatizo ya uoni hafifu,unakosababishwa na changamoto mbalimbali ikiwamo mtoto wa jicho, upeo mdogo wa kuona na presha ya macho.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya. Tena zikiongeza kuwa presha hiyo ni ugonjwa unaotajwa kuathiri zaidi watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40 na kwamba asilimia 4.2 ya Watanzania ambao ni takribani watu 440,000 wana tatizo hilo.

Pamoja na kuwapo kwa idadi hiyo ya watu wenye ugonjwa huo, ambao kitaalam unaitwa ‘glaucoma’, inasemekana asilimia 70 hadi 90 ya watu wenye ugonjwa huo, hawajijui kama wanao, taarifa ya Wizara inaeleza.

Mwaka 2017 ni watu 13,240 tu walikwenda vituo vya tiba kwa tatizo la presha ya macho, idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na walio katika hatari ya kuwa na ugonjwa huo, ambao hawajagunduliwa.

Ugonjwa huo inaelezwa kuwa ni kati ya kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni katika ubongo ili kutafsiri kile kinachoonekana.

Presha ya macho huathiri mishipa ya fahamu inayohusika na kuona 'optic nerves', na kwamba mgonjwa asipopata matibabu kwa wakati anaweza kupata upofu.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile, anayasema hayo mwaka jana kwenye wiki ya maadhimisho ya utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo.

Anasema, 'glaucoma' ndiyo inayoongoza kwa idadi ya watu wasioona, na Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 1.7 wenye matatizo ya kutokuona vizuri.

Kutoona huko kunasababishwa na matatizo mbalimbali ikiwamo kuwa na mtoto wa jicho, na presha ya macho.

Anaeleza kwamba mtu anaweza kupata upofu taratibu siku hadi siku bila dalili yoyote katika hatua ya awali, na ili kuweza kugundua iwapo mtu anao kuna umuhimu wa kupima macho angalau mara moja kila mwaka.

Maelezo ya Naibu Waziri yanatosha kuhamasisha jamii kupata elimu na kujitokeza kwa wingi katika vituo vya afya wapime macho, kuona kama wana ugonjwa huo, ili wapate matibabu haraka kuepuka upofu.

Wito huo wa kupima macho ulirudiwa na mbobezi wa tiba ya macho wa hospitali ya CCBRT ya Dar es Salaam, Dk. Cyprian Ntomoka na kufafanua kuwa siyo kila ugonjwa wa macho ni lazima mtu avae miwani.

Anasema, wapo baadhi ya watu hawapendi kutumia miwani na wanapoumwa macho wanaamini kwamba wakienda hospitali kupima wataambiwa wavae miwani na kumbe sivyo. Ntomoka anasema, presha ya macho inatokana na majimaji yanayozalishwa kubakia zaidi jichoni ikilinganishwa na yale yanayotoka, hivyo wao hufanya kazi ya kuyapunguza kwa kutumia mashine maalum, ili yalingane.

Bingwa huyo anasema, kitaalam macho huwa yana presha ya kiwango kinachoitwa kitaalam 10mmhg hadi 21mmhg, lakini kinapozidi hapo, mtu hutambuliwa kuwa ni mgonjwa wa presha ya macho.

Msisitizo wake ni watu kupata elimu kuhusu ugonjwa huo na pia jamii kuwa na mazoea ya kupima macho, ili wale wenye umri wa miaka 30 wapime angalau mara moja kwa mwaka, lakini wa zaidi ya umri huo, upimaji wa macho ni wa lazima.

Hivyo ni muhimu watu kuchukua hatua mapema za kupima afya ya macho kuliko kusubiri kupata madhara wakati uwezekano wa kuyaepuka upo.

Wataalam wa afya wameshaweka wazi kwamba siyo kila tatizo la macho ni lazima mtu avae miwani, bali yapo mengine ambayo ni kutibiwa tu, kwa hiyo ni muhimu kupima ili kujua chanzo.

Macho ni miongoni mwa milango mitano ya fahamu inayowezesha kujua mazingira, kutambua mambo mbalimbali.

Milango ya fahamu yakiwamo macho, ni muhimu kwa binadamu, kutokana na kwamba yanaona na kufanya shughuli zake za kila siku kwa uhakika, hivyo ni vyema kuyapima kila inapowezekana.