Elimu: Mafanikio ni idadi au ufahamu?

19Apr 2016
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Elimu: Mafanikio ni idadi au ufahamu?

INANISHANGAZA zaidi kuwa, siku hizi kigezo kikuu cha mafanikio katika elimu kimeanza, na kubakia kuwa idadi. Tumetengeneza madawati kadhaa, tumedahili wanafunzi kadhaa,

umefelisha na kufaulisha wanafunzi kadhaa, tumesajili walimu kadhaa, tumejenga madawati kadhaa.

Idadi hii imevuka asilimia fulani, imeshindwa kuvuka asilimia fulani. Na kuna wakati najiuliza kwa mfano, kwenye kipengele kimoja, kufaulu maana yake nini haswa? Ukisema wanafunzi kadhaa wamefaulu, sijui maana yake nini? Kufaulu kunatoa ahadi gani kwa jamii na kwa taifa, na hasa tunapoenda kwa namba, namba, namba!

Nafahamu tunapokuwa na mradi mkubwa kama huo wa kusomesha wanafunzi, lazima tuwe na vigezo vya kuingilia na kutokea, na namna hiyo kigezo rahisi sana, na hasa kinapotumika kirahisi rahisi bila kuzipatia namba hizo thamanisho linaloweza kutueleza hakuna kitu.

Lakini katika namba hizo za kufaulu… mwanafunzi anamaliza Chuo kikuu. Hajajua kutumia kompyuta kabisa… na kama anajua ni kwa ajili ya kuandikia insha yake kwa vile mwalimu anataka hivyo.

Mwanafunzi hajui kutafuta matini ya kujisomea au kufanyia utafiti wake kwa kutumia kompyuta. Nilikuwa na rafiki yangu mmoja… anasomea Shahada ya Uzamivu, anashangaa inakuwaje mtu anaweza kuandika kitabu,kurasa mia moja, mia mbili, mia tatu…anaona kama ni muujiza.

Huyu ni msomi wa digrii ya uzamili tayari na aliingizwa katika idadi ya waliofaulu na anapandishwa daraja na ghafla atakuwa katika idadi ya watakaofaulu shahada ya uzamivu.

Na tuna watu wengi waliohitumu shahada ya kwanza, ya pili, ya tatu na kuendelea lakini akikaa na kuongea unashangaa kama kweli aliingia kwenye kundi lile la namba. ya kufaulu.

Mwalimu Julius Nyerere alipoanzisha elimu ya watu wazima kama kampeni, alikuwa na maana kubwa sana. Hii ni tafsiri yangu. Kuwa hapa kuna mtoto aliyesoma hadi darasa fulani. Baba na mama yake na shangazi na ukoo, hawajasoma, lakini mtoto wao amesoma angalau kiwango fulani.

Sasa anawezaje kuleta mabadiliko katika familia katika hali hiyo?. Msomi anaishi katika jamii ambayo hawakusoma na hawajui maana ya kusoma. Na hata akiwaletea maarifa mapya ni kazi bure.

Nyerere aliona ili kuwezesha mtoto huyu akawa chachu ya maendeleo, lazima jamii ijue kusoma na kuandika na iwezeshwe kujitafutia maarifa wao wenyewe bila kumsubiri mtaalamu au mtoto wao.

Na aliona elimu kuna ile ya kujua kusoma na kuandika, na kuna ile ya kumwezesha kufanya mambo yake kwa ufanisi zaidi Kisomo cha Manufaa.

Naona kama hili halizingatiwi tena! Unaweza kujenga sifa juu ya idadi ya walioingia shule au kumaliza na kufaulu, huku huko kwenye jamii wanakwenda idadi ya wasiojua kusoma na kuandika inaongezeka?

Unajenga jamii ipi yenye kujenga matumaini ya kuibadilisha nchi wakati hawajui kusoma kwa ajili ya kujitafutia maarifa mapya? Watoto wanasoma kwa bidii, na wengine wanasemekana wamefaulu, wanapofika nyumbani wanawakuta wazazi wao wamepungua katika uwezo wao wa kujitafutia maarifa.

Hawasomi, haangalii TV za mafunzo au kusikiliza radio angalau. Wamekaa tuu, wakijitahidi zaidi waangalie TV za upako na michezo ya bongo muvi au African Movie Channel. Tunasema kuwa tunataka kuwa na dunia ya viwanda.

Na viwanda na teknolojia maana yake ni kujenga utamaduni wa watu kuwa watafiti, wagunduzi, wenye kutafuta maarifa mapya, yaani wao wanachoona ni kuwa maendeleo maana yake ni kujitafutia maarifa mapya. na sio kuamini kuwa kuna nguvu fulani ya kimungu itaigilia kati, kwa sababu bila hiyo binadamu hata weza, na kuwa akihisi kuwa hajaipata hiyo nguvu atakata tamaa au atashinda nyumba za ibada au kwa matabibu wa kiasili hadi afanikiwe.

Ni lazima tujenga mkakati ambao sio tu watu wanalazimishwa kusoma, pia kuwafanya wapende kusoma, wapende kutafuta maarifa mapya na wapende kuamini kuwa kila kitu kinawezekana kwa kutafuta maarifa na sio kwa kutambika au kwa majaaliwa ya Mungu.

Watoto wanapohitimu shule sio tu kwamba wanakuwa wamefaulu, bali wamefika kwa jamii ambayo tayari imejaa uwezo wa kujitafutia maarifa nje ya shule na wazazi au jamii ina miundo mbinu ya kutosha kwa ajili ya hilo.

Mtoto ndipo atagundua kuwa, kumaliza shule ndio mwanzo mpya wa kujitafutia maarifa, na sio mwisho kama ambavyo sasa inavyoonekana kwa wengi. Kuwa wakishamaliza masomo ndio mwisho wa kusoma na kujitafutia maarifa. Ni kutafuta kazi, na ukiipata kazi na mshahara ukaingia husomi tena ila kama unataka kurudi tena kusoma unaiona hiyo.

Tena mbaya zaidi, hata miongoni mwa wale ambao kazi zao ni kusoma kila siku yaani walimu,madaktari na kadhalika akisha bakia na ile akiba ya maarifa- stock knowledge ya kumuwezesha kufanya kazi kila siku hasomi tena, ila kama kuna semina au warsha.

Hana kitabu na maktaba ni neno gumu sana kwake. Magazeti tu inakuwa shida. Jamii haiwezi kuendelea kwa idadi, inaendelea kwa ubora wa wanaofaulu, na inaendelea kwa kuwa na wananchi ambao wanatumia sehemu ya rasilimali muda na rasilimali fedha kutafuta maarifa mapya.

Kama hiyo halifanyiki, makumi na mamia na maelfu ya wanaofaulu hayatasaidia kuleta maendeleo- watatumbukia kwenye mtego uleule wa kusema nilishamaliza shule, anakung’uta vumbi la viatu harudi tena kusomasoma.