Elimu ni daraja la uhakika la mafanikio

27May 2016
Veronica Assenga
Nipashe
Mjadala
Elimu ni daraja la uhakika la mafanikio

ELIMU ndio msingi pekee muhimu wa kuweza kuutumia kikamilifu ili kuingia katika maisha na kuyaendesha kwa misingi ya mafanikio ya uhakika.

Naamini mtaungana nami kwa mtazamo huu kwamba, tangu enzi za kale suala la kupata elimu lilipigiwa kampeni na kupewa kipaumbele kutokana na ukweli kuwa, elimu ndio ukombozi katika kupambana na umaskini.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere alihakikisha kuwa Watanganyika wanakuwa na elimu ili waweze kujikomboa kutoka utumwa wa wakoloni na kujiongoza katika maisha yao.

Alisisitiza elimu kwa watu wote, hasa ya misingi iliyotolewa bila gharama ili kila mtu amudu na kusisitiza elimu ya watu wazima iliyolenga stadi tatu za Kujua, Kusoma na Kuandika (KKK) kwa lengo la kufuta ujinga.

Hatua hizo, zilikuwa nzuri na zenye kuleta mafanikio tulionayo leo katika Tanzania na kwingineko duniani .

Mtaungana nami kutoa pongezi hizo kwa walimu ambao wana jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanatoa elimu bora na maarifa ya nyumbani kwa watu mbalimbali.

Mwalimu ni daraja muhimu la kuunganisha ufunguo wa elimu ili kumfikia mtu aweze kufungua maisha yake kwa kutumia ufunguo huo.

Mwalimu ndio anayechonga ufunguo wa maisha.Kila mtu makini, lazima apite kwa mtu huyu muhimu katika maisha ili kuwezeshwa kupata ujuzi na maarifa ya kuendeleza maisha ya kila siku.

Mwalimu ndiye anayezalisha wataalamu wa fani zote na kwa ujumla kila mtu anamtegemea.

Mfano raisi, daktari, mhandisi, mfanyabiashara, mkulima, mvuvi, mwandishi, rubani, nahodha, mtafiti na wengine wengi wote, lazima katika hatua ya awali wapitie kwa mwalimu.

Mwalimu huanza kutoa elimu kuanzia hatua ya mwanzo mtoto anapoandikishwa shule baada ya kupata elimu pekee ya awali kutoka kwa wazazi au walezi.

Mtoto anapoanza elimu ya awali huwa mikononi mwa mwalimu atakayemjenga na kumkuza kifikra,kiakili na kimaadili katika kutambua mambo mazuri na mabaya.

Halikadhalika mtoto mdogo, hasa wa elimu ya awali anahitaji umakini wa hali ya juu, kwani akili yake ni changa na ina uwezo mkubwa wa kunasa vitu, japokuwa polepole lakini akishanasa ni vigumu kumbadilisha.

Mtoto anaamini kile anachoambiwa na mwalimu wake na atakua nacho katika akili na maisha yake siku zote, hivyo kwa kulitambua hili, mtoto huyu anatakiwa kuwa na mwalimu mzuri toka hatua ya awali.

Mwalimu mzuri namaanisha mwenye ubora, ujuzi na maarifa ya kumwelewa na kukaa na mtoto, kucheza na akili na saikolojia ya mtoto, ili kuweza kumjengea uwezo mzuri wa kukua katika maisha ya baadaye.

Aidha Mwalimu huyo anapaswa kutumia mbinu shirikishi za kumkuza mtoto, kwa kumwelekeza mambo mazuri na jinsi ya kuishi na jamii nzima, inayomzunguka hata sehemu yoyote ya dunia.

Mwalimu anabaki kuwa mtu wa muhimu katika kugusa na kutengeneza maisha ya kila mtu kielimu.

Nimezungumzia umuhimu wa mwalimu, kwa sababu ndiye mlengwa mkuu wa elimu kuanzia ngazi ya awali, elimu inapokuwa katika kiwango kizuri anasifiwa na inapokuwa katika kiwango kibaya mwalimu hulaumiwa.

Hivi karibuni sekta ya elimu iliripotiwa kusuasua kutokana na viwango vya ufaulu, kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari. Baadhi ya sababu zilizotajwa ni mabadiliko ya mara kwa mara ya mtaala ya elimu.

Nyingine ni kushuka kwa maadili ya wanafunzi, ujio wa matumizi ya mitandao ya kijamii, pia walimu walitajwa kukosa ujuzi na kuweza kumudu kufundisha masomo vizuri.

Kwa kulitambua hilo, Serikali iliamua kubadili sera ya elimu na kuzindua sera itakayolenga kuboresha elimu na kukuza kiwango cha ufaulu zaidi.

Sera hiyo iliyozinduliwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ilileta faraja na matumaini katika kuchonga ufunguo mzuri wa kufungua maisha bora kwa watanzania wengi siku za usoni.

Lakini Serikali haikuishia hapo, badala yake sasa imegusa mzizi wenyewe kwenye elimu ambao ni walimu kwa kuanza kutoa mafunzo ya walimu 1,800 wa shule ya msingi kutoka mikoa 14 nchini ili kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha mtaala huo mpya wa elimu kwa darasa la kwanza na la pili.