Elimu sio kigezo cha kutosheleza kumfanya kila aliyeipata kujiajiri

10Jan 2017
Charles Kayoka
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Elimu sio kigezo cha kutosheleza kumfanya kila aliyeipata kujiajiri

KUFIKIA daraja la juu pekee haitoshelezi kama mfumo wa elimu haumjengi mhitimu kufikiri kwa uyakinifu na kumjengea uwezo wa kujitegemea kimawazo na kuwa mwenye uwezo wa kutatua matatizo.

Kama tunaendelea kufundisha watoto kwa tabia ya kuwakaririsha na kumtegemea mwalimu bila kuwajengea uwezo wa kujitegemea, hawataweza hata kujisomea gazeti.

Kingine katika elimu, ambacho ningetaka kukisitizia ni kuwa na aina ya masomo na kozi zinazoonyesha kupanuka kwa aina ya elimu na mafunzo yetu. Kwa sasa idadi ya kozi na mafunzo tunayotoa bado ni chache na ni zilezile tulizoachiwa na Wakoloni.

Pili wahitimu wa vyuo vikuu na hasa ngazi ya uzamili na uzamivu, hubabaisha katika kusoma kwao na hata wale waliokuwa makini hawapati nafasi ya kuingiza katika mitaala kile walichokisomea. Idara na wakuu wa ndaki (kitivo) wanakuwa wagumu kubadilika ili kuchukua mawazo mapya.

Lakini lazima tukiri kuwa, wataalamu waliobobea katika Nyanja mbalimbali wanaoweza kuzalisha wasomi wa aina aina bado ni wachache. Wasomi wanakuwa ni wale wale.

Kigezo kingine kikubwa ambacho ningetaka kukitaja hapa ni kuwa na wanafunzi ambao wamejengewa uwezo wa kufanya utafiti wao wenyewe bila kutegemea wengine wala kuiga iga.

Kama wanafunzi wanamaliza masomo yao wakiwa na uwezo mkubwa katika utafiti, wana uwezo mkubwa sana wa kujenga uwezo wa kujiajiri, kwa sababu watakuwa wabunifu na wenye uwezo wa kubaini mapengo ambayo wawekezaji wengine katika maeneo waliyosomea wameyaacha.

Huwezi kuwa na mwanafunzi ambaye hajasomea biashara na masoko katika eneo alilosomea, halafu ukategemea kuwa anaweza kuanzisha mradi wa kujiajiri na kuwaajiri wengine. Ni lazima kuwa na wanafunzi wakasoma ujasiriamali, uanzishwaji wa miradi, na namna ya kuitangaza na kuiuza.

Mtu amesoma Kiswahili sarufi au fasihi, hajui namna gani anaweza kujiajiri katika somo hilo, halafu hajafundishwa namna ya kuanzisha na kuusimamia mradi, na hajua namna gani akianzisha mradi anaweza kujitangaza ili kupata wateja, halafu tunataka aweze kujiajiri.

Hapa ni kutaka waende kwenye mwezi huku tukijua kuwa hawajui hata kutengeneza baiskeli. Kutakuwa na wachache wanaoweza lakini wengi watahitaji kuajiriwa kwani ndipo watajisikia amani zaidi.

Nilijaribu mara nyingi kuwashauri wanafunzi wangu pale Chuo Kikuu kuwa, jiungeni katika makundi kisha tafuteni jambo moja mlilolisomea na kulifanya kuwa ajira yenu. Wengi wameshindwa kuthubutu isipokuwa wale wachache waliokuwa makini wakati wa masomo na walipenda walichokisomea, na wale waliokuwa sio waoga kujaribu kitu ambacho wengine wameshindwa au wamekiogopa.

Kwa hiyo, elimu sio kigezo cha kutosheleza kumfanya kila aliyeipata kujiajiri. Na umeona mara nyingi tu kuwa, wale waliofanikiwa katika ujasiriamali na kuanzisha miradi mikubwa sio waliosoma kupindukia.

Lakini je, tuna wanasiasa wanaojua kuwa wanafunzi wanapohitimu wanatakiwa kujiajiri? Wao ndio wakipiga debe juu ya jambo la kujiajiri. Je wana uwezo wa kulifanya hilo linawezekana kwa kuhakikisha kuwa, sera za elimu, za vijana , za jinsia na uchumi inalenga kufanikisha hilo.

Na kuwa wizara husika zi(-i)naanzisha mfumo wa bajeti na kozi zinazolenga kufanikisha hilo. Wanasiasa wanasisitizia kuwa wanafunzi wajiajiri ,wakati hawaweki bajeti ya kutosha katika sekta zinazoweza wanafunzi wahitimu kujiajiri, ni wale wanaotaka tu kusikika kwenye vyombo vya habari na kwa kweli hawajui nini wanachokizungumza.

La mwisho niseme kuwa, wanafunzi wenyewe ni lazima wajenga Imani kuwa wanaweza kujiajiri, kama wanaona wanahitimu na uwezo mdogo wa kujiajiri, wahakikishe kuwa, wanasoma kozi za ziada zinazoweza kuwasaidia kujiajiri.

Wasisubiri kuambiwa, wajaribu kuthubutu, wajaribu kuuliza, na wajifunze kutoka kwa wengine waliowatangulia na wakafanikiwa.

Mtu yeyote anayeweza kufanikiwa ni yule anayefikiria kwa upana na kwa undani na anayejaribu. Kujiajiri kuna kazi kubwa na kunaweza kukatisha tamaa anayetaka kujiajiri kwa sababu ya kupoteapotea njia, lakini ndivyo wengine wote walivyopitapita.