Elimu ya matumizi sahihi ya mabasi yaendayo haraka Dar ni muhimu sana

12May 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu ya matumizi sahihi ya mabasi yaendayo haraka Dar ni muhimu sana

USAFIRI wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Dart) umeanza wiki hii kwa majaribio ili kuwapa fursa watumiaji wapate uzoefu wa matumizi ya mfumo mpya wa usafiri jijini .Unatarajiwa kuanza rasmi leo.

Yawezekana mfumo huu mpya wa usafiri, unaweza kuwa mwarobaini wa kukabili adha ya usafiri wa umma uliokuwapo awali katika baadhi ya maeneo, hususan kati ya Kimara, mjini kati Posta hadi Kivukoni.

Usafiri huo umeanza na mabasi 50 ya majaribio kwa kusafirisha abiria bure, kutoka maeneo ya Kivukoni-Kimara Mwisho, Kimara Mwisho-Morocco, Kivukoni-Ubungo, Kariakoo-Kimara Mwisho kumewafanya wakazi wa jijini kuwa na matumaini ya kuondokana na adha sugu za usafiri wa awali.

Licha ya kwamba baadhi ya maeneo bado yanahitaji usafiri huo kama vile Mbagala, Tegeta, Gongo la Mboto hata hivyo, hatua iliyopigwa ni mwanzo mzuri.

Pamoja na usafiri huu kuwa wa matumaini, baadhi ya madereva hususan bodaboda wameendelea kusumbua kwa kukatiza katika njia za Dart hata kusababisha mabasi haya yasiende kwa kasi kama inavyotakiwa kuwa.

Kwa mfano, abiria anayepanda mabasi hayo akitokea Kimara Mwisho-Kivukoni hayasimami katika kituo chochote hivyo anatarajiwa kutumia dakika 30 hadi 40 kufika kituo cha mwisho cha safari yake.

Anayepanda mabasi hayo kutoka eneo hilo hilo lakini kwa kutumia basi lisilo katika mfumo huo yaani utaratibu wa kawaida, atatumia karibu saa nzima yaani dakika 60, kwa mujibu wa waendeshaji wa mradi huu.

Hata hivyo, uelewa mdogo wa baadhi ya watembea kwa miguu huku wengi wao wakiendelea kupuuza kwa kuvuka barabarani hata pasipokuwa na alama za pundamilia. Mwenendo unakwamisha muda wa mabasi kusafiri kwa kasi iliyopangwa.

Matokeo yake dereva inampasa kupunguza mwendo ili kuwanusuru watembea kwa miguu pamoja na kupishana na bodaboda ambazo zinaongoza kwa uvunjaji wa sheria za usalama barabarani.

Katika hili, inapaswa wakazi wa jijini kuachana na desturi za kuvuka holela badala yake wazingatia maeneo maalum ya kuvukia , kwa mfano pale katika Ubungo katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani, kumejengwa daraja la kuvukia.

Hata hivyo, baadhi ya abiria wanadai kuwa wanachelewa hadi wazunguke katika daraja badala yake wanapita katika barabara na kuhatarisha maisha yao nay a watumiaji wengineo wa barabara.

Pia watumiaji wa mabasi haya, wanatakiwa kuwa wazalendo watunzaji wa mali, ikiwemo desturi ya kutupa taka ovyo na masuala mengineyo ya usalama .

Ikizingatiwa kwamba,mabasi hayo hayana kondakta, hivyo abiria kusimamiwa na kuelekezwa simama pale, rudi nyuma kaa kushoto kulia hakuna. Ni vyema abiria wajipange kwa kujiongoza na kujisimamia wenyewe.

Wale wanaosubiri kutangaziwa vituo vya kushuka kama ilivyo kwa usafiri wa awali wanahitaji kuwa makini na kujiandaa kituo kimoja kabla, ili anapofika anakuwa tayari kushuka.

Elimu inahitaji kuendelea kutolewa mara kwa mara na mamlaka husika ikwamo Sumatra, Dart wenyewe ili abiria wafahamu namna ya kutumia mfumo huu mpya wa usafiri jijini, ambao ukitunzwa kwa umakini utasaidia kuboresha usafiri wa wakazi wa jiji hilo hata kuwafanya wawahi katika shughuli zao.