Elimu ya watoto wetu wamiliki ni sisi wazazi

12Mar 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu ya watoto wetu wamiliki ni sisi wazazi

KATIKA juhudi za kuboresha elimu, serikali ilishatoa maelekezo kuwa kila shule ya msingi, ni lazima iwe na darasa la awali, kwa ajili ya watoto wadogo wanaojiandaa kuanza darasa la kwanza.

Maelekezo hayo yanatokana na ukweli kwamba msingi mkubwa wa elimu, unaazia chini kabisa, kwa maana ya shule ya awali, kwa sababu huko ndiko ambako kunakopatikana mwanafunzi anayefaa au asiyefaa.

Kutokana na ukweli huo, serikali ilitoa maelekezo hayo ili kwamba wanafunzi wanaoingia darasa la kwanza wawe wanajua kusoma na kuandika, kwani hatua hiyo ni utekelezaji wa mpango wa Kukuza Stadi za Kusoma (KKK) kwa ajili ya kuboresha elimu kwa wanafunzi.

Hata hivyo, pamoja na lengo hilo nzuri, bado kumekuwapo changamoto ambazo zinaweza kukwamisha maendeleo ya watoto, iwapo wazazi hawatazivalia njunga na kuzimaliza haraka iwezekavyo.

Ninasema hivyo, kwa sababu baadhi ya changamoto zipo chini ya uwezo wao, hivyo wakiwa kimya zinaweza kuathiriwa zaidi kwa elimu ya awal, hivyo kuendelea kuwapo wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.

Kuna taarifa zilizowahi kuandikwa na vyombo vya habari miaka michache iliyopita, kwamba wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Mkambarani mkoani Morogoro, walikuwa wakisomea jikoni, kwa sababu ya uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo.

Hizo ni taarifa za sehemu moja, lakini inawezekana kuna shule nyingi zenye changamoto za aina hiyo, ambayo kimsingi kama nilivyosema awali, zipo kwenye uwezo wa wazazi.

Wakati baadhi ya shule zikikumbwa na ukosefu wa vyumba vya madarasa, wazazi na walezi wapo, ni kama wameridhika nayo, kwa watoto wao kusoma katika mazingira hayo.

Mchango walionao kuboresha elimu ya watoto wao ni upi? Hapo tunapaswa kujuliza. Hivi, wanasubiri wafanyiwe kila kitu na serikali? Kuna ugumu gani wa kuitisha vikao kwa ajili ya maendeleo ya shule na watoto wao kwa ujumla?

Siyo vizuri kusubiri serikali itufanyie kila kitu, bali jamii sasa ibadilike kwa kutambua wajibu wake katika kuhakikisha watoto wanapata elimu, tena katika mazingira bora kuliko kujiweka pembeni, kana kwamba haihusiki.

Mazingira kama hayo ya kusomea jikoni, yanaweza kusababisha watoto wengi wakahitimu shule ya awali bila ya kujua kusoma na kuandika. Watoto wasaidiwe kwa kila hali, ili kuhakikisha wanakuwa na madarasa yao.

Ikumbukwe, miaka ya nyuma msingi wa ufundishaji watoto elimu ya awali ulikuwa haupewi kipaumbele hasa maeneo ya vijijini na kusababisha baadhi ya wanafunzi kuhitimu hata elimu ya msingi, bila kujua kusoma na kuandika.

Serikali ililibaini hilo na kuamua kila shule ya msingi ni lazima iwe na darasa la awali kwa ajili ya 'kuwanoa' watoto ili wanapoanza darasa la kwanza wawe wanajua kusoma na kuandika.

Kinachotakiwa ni wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao, badala ya kutegemea serikali ifanye kila kitu.

Vilevile, ni muhimu wazazi na walezi kutambua kwamba walimu ni msingi mzuri kwa ajili ya kuwasaidia watoto kupiga hatua, hivyo ni muhimu kushirikiana nao kwa kila hali.

Karne hii ya sayansi na teknolojia siyo tena ya kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika, hivyo wazazi na walezi wasichangie kuwapo kwa wanafunzi wa aina hiyo.

Wambue kwamba elimu ya watoto wao iko mikononi mwao, kwani wanapaswa kushrikiana kwa karibu na walimu ili kutatua changamoto zinazozikabili shule ikiwamo ukosefu wa madarasa ya elimu ya awali.

Bila wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa madarasa hayo, elimu ya awali inaweza kusuasua kwenye baadhi ya shule za serikali.

Serikali ilishaweka wazi kwamba huwa inaunga mkono pale wananchi wanapoonyesha juhudi zao, hivyo ni vyema jamii ikatambua hilo na kulizingatia kuliko kungojea kufanyiwa kila kitu.