Elimu zaidi matumizi ya njia za BRT inahitajika

12Jun 2016
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Elimu zaidi matumizi ya njia za BRT inahitajika

HIVI karibuni Kikosi cha Usalama Barabarani kilitoa takwimu zake kuhusu kuongezeka kwa makosa ya usalama barabarani, ikiwamo yanayotokea katika Barabara za Mabasi yaendayo Haraka (BRT), jijini Dar es Salaam.

Kwa muda siku sita pekee, ilielezwa, madereva 54 walikamatwa kutokana na kipita katika njia za BRT na kusababisha ajali, ikiwamo uharibifu wa mabasi na miundombinu yake.

Operesheni iliyoanza Juni Mosi hadi Juni 6 inadhihirisha bado wakazi wa jijini hawazingatii, kuzielewa sheria zinazolinda barabara za BRT lakini wapo wanaozipuuzia, wakidhani watatozwa faini na kuondoka zao.

Kwa hivi sasa jeshi hilo limesema hakuna dereva atakayepita katika njia za BRT na kutozwa faini zaidi ya kupelekwa mahabusu, wakati utaratibu wa kufikishwa mahakamani ukiendelea.

Hii ni baada ya kutokea ajali 14 katika kipindi cha kuanzia Mei 10 hadi Juni 6 na kusababisha majeruhi ya watu watano na uharibifu wa mabasi ya mwendo haraka.

Juhudi zinazoonyeshwa na jeshi hilo zinakwamishwa na madereva wachache ambao wameshaisababishia hasara serikali kwa kuharibu mioundombinu ya BRT na kuharibiwa kwa mabasi ya mwendo haraka.

Kutokana na kuendelea kutokea kwa makosa ya usalama barabarani yanayofanywa na madereva wa bodaboda na magari binafsi, kunahitajika kuongezeka kwa elimu ya usalama barabarani kupitia njia mbalimbali.

Elimu inaweza ikatolewa katika vyombo vya habari, mabango ili kupunguza na kuondoa ajali hizi.

Tayari madereva wawili Hassan Mohamed (30) mkazi wa Tegeta, aliyekuwa akiendesha bodaboda yenye usajili namba MC 299 ABS na Rashid Sheha (45) mkazi wa Kimara aliyekuwa akiendesha bodaboda namba MC 379 ASV wamefungwa miezi sita jela kila mmoja bada ya kukutwa na makosa ya kupita njia za BRT.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga anasema mkakati jeshi hilo wa kuwakamata madereva wa magari, bodaboda wanaopita katika njia hizo na kusababisha uharibifu wa mabasi na miundombinu utaendelea.

Utaratibu wa jeshi hilo hivi sasa ni kuwapiga picha wakiwa wameshikilia ubao wa majina yao, maeneo wanayotoka, kazi wanakofanyia na kosa walilotenda na kisha kuwekwa katika mitandao ya kijamii, ili kuweka kumbukumbu kwa jeshi hilo na jamii kufahamu wale wanaoendelea kukiuka sheria hizo.

Hata hivyo kuna ongezeko kubwa la makosa ya usalama barabarani zaidi ya 290,161 kwa kuwa kuanzia Januari hadi Mei mwaka huu, kulikuwa na makosa 774,195 ikilinganisha na Januari hadi Mei mwaka jana ambako kulikuwa na makosa 484,034.

Wakati umefika kwa watumiaji wa barabara kuzingatia kanuni, sheria, alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali na makosa huku mamlaka zikiendelea kutoa elimu.