Enyi waandishi, kazi ni kanzi

15Oct 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Enyi waandishi, kazi ni kanzi

‘KANZI’ ni hazina kubwa au vitu vya thamani. Kanzi ni kama hazina. Twafunzwa umuhimu wa kazi ambayo ni hazina yetu ya siku za shida au zijazo.

Neno ‘kazi’ laweza kuwa na maana mbili au tatu lakini ninalolizungumzia kwenye makala yangu ni shughuli yoyote anayofanya mtu kwa ajili ya kupata riziki ya kuendeshea maisha yake.

Mwandishi ni mtunzi wa makala, kitabu, kazi ya sanaa au habari mbali mbali za matukio. Yasemwa mwandishi wa habari ni masikio, pua na macho ya wasomaji.

Uandishi au uandikaji, ni shughuli inayohusu masuala ya kuandika kama vile habari au kitabu. Kwa hiyo mwandishi husikia, hunusa na huona matukio mbalimbali kisha kuwajuza wananchi kwa njia ya magazeti, redio na runinga.

Kwa hakika uandishi unahitaji utulivu na hekima ili kuwafahamisha wasomaji wa magazeti, watazamaji wa runinga na wasikilizaji wa redio kuhusu matukio yatokeayo nchini na kwingine ulimwenguni.

Mwandishi mzuri huandika kwa maneno yanayotambulika kwa wote badala ya kutumia maneno ya kihuni yatumikayo mitaani! Mwandishi aweza kuwa na habari nzuri lakini akaiharibu au kuipotosha kwa kutumia maneno ya mitaani yaani simo* ambayo si lugha sahihi.

*Simo ni msemo wa muda unaozuka katika jamii na kisha kupotea. Lugha ya aina hiyo kwa Kiingereza yaitwa ‘slang’ ambayo kwa Kiswahili ni simo au misimu, yaani lugha ya mitaani.

Soma hii: “Taifa Stars, Sudan ‘vibe’ kama lote” ni kichwa cha habari inayohusu mchezo wa kandanda kati ya Taifa Stars na Sudan jijini Dar es Salaam. Ni wangapi wanaojua maana ya “‘vibe’ kama lote?”

Aya ya pili ya habari husika iliandikwa: “ Kampeni pacha ya Tunakanyaga Mpaka CHAN, iitwayo Chaji Simu Yako, tukutane Taifa Kuwamulika Wasudan, nayo imepamba moto ikilenga kuchagiza mashabiki kumiminika kwa wingi kuisapoti Stars ikiwakanyaga Sudan kuelekea kwenye fainali hizo Cameroon.”

Yaelekea watazamaji hawakuchaji (nguvu zinazozalishwa na umeme) simu zao na kusababisha kukosa mwanga wa ‘kuwamulika’ wachezaji wa Sudan hata kufanya Taifa Stars wafungwe 1-0 kwenye uwanja wa nyumbani, tena mbele ya umati wa Watanzania! (Haya ni maoni yangu.)

“Kampeni pacha ya Tunakanyaga Mpaka CHAN.” ‘Pacha’ ni neno lenye maana tatu: 1) watoto wawili au zaidi waliozaliwa kwa mimba moja; 2) kitendo cha kuzifunga pamoja nazi ambazo hazijafuliwa; 3) ni –enye kuambatana na kingine (Wazanzibari husema ‘chengine.’) Je, neno ‘pacha’ kwa muktadha ninaoujadili lilistahiki kutumiwa?

“… imepamba moto ikilenga kuchagiza mashabiki kumiminika kwa wingi kuisapoti Stars …” Neno ‘chagiza’ ni kitenzi elekezi na maana yake ni ghasi mtu kwa kumdodosa sana; udhi, sumbua. ‘Chagizi’ ni –enye kusumbua na ‘chagizo’ ni shinikizo; udhia, usumbufu, kero. Je, mwandishi ametumia neno ‘chagiza’ kwa usahihi?

“Bodaboda ya Mchongo wa (jina la gazeti) yatua Morogoro” ni kichwa cha habari inayoeleza washindi wa mchezo wa gazeti ninaloliheshimu.

Maana ya ‘mchongo’ ni mtindo wa utengenezaji wa samani ya mbao unaoitafautisha na nyengine, kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha la Zanzibar.

*Visawe ni maneno yenye maana zinazokaribiana. Kwa mfano, ‘mtoto’ na ‘mwana’ humaanisha kitu kimoja.

Visawe hutumika ili kuwasilisha dhana ileile iliyokusudiwa bila kubadilisha maana. Kwa hiyo visawe hupamba lugha ama katika mazungumzo au katika uandishi wa aina mbalimbali.

Kwa mfano ‘shabihi’ ni fanana, landana. ‘Simanzi’ maana yake ni majonzi, jitimai, ukiwa, huzuni. ‘Taadhima’ ni heshima, adabu, tasfida. ‘Wajihi’ ni sura, uso. ‘Kibahaluli’ maana yake ni kibatari, koroboi.

Maana ya ‘kuwadi’ ni kijumbe, gambera, mtalaleshi, kibirikizi. ‘Laghai’ ni danganya, nyenga, kenga, ongopa. ‘Weweseka’ ni hohosa, babaika, kiakia, hangaika, riyariya. ‘Mvulana’ maana yake ni ghulamu, janadume, barobaro. ‘Mtu’ ni adinasi, mja, mwanadamu, mahuluki.

“Messi vyenga kama ana gundi miguuni vile.” Mwandishi katumia neno ‘vyenga’ akiwa na maana ya chenga nyingi. Hata hivyo ‘chenga’ haina wingi hata iitwe ‘vyenga!’

Baadhi ya maneno yasiyokuwa na wingi ni baba, mama, dada n.k. Ni kupotosha Kiswahili kusema ‘wababa, wamama, wakaka, wadada.’

Upotoshwaji huu hufanywa sana na Wakristo wenzangu! Kama ilivyo mitaani kaka huitwa ‘mkaka’ neno lenye maana ya mti wa porini wenye kiini cheusi na kigumu na majani madogomadogo; mkurungu.

“Wakati mashabiki wengi wa Toto Africans wakijiuliza heshima ya klabu yao itarejea lini, beki wa timu hiyo Robert Magadula amesema tulizeni mzuka mambo mazuri yanakuja watulize mzuka.”

Mwandishi katumia neno ‘mzuka’ mara mbili. Alikuwa na maana gani? ‘Mzuka’ ni pepo; mahali patukufu akhera ambapo mtu mwema duniani ataishi baada ya kufufuliwa.

Pia ni jini, yaani kiumbe dhahania (-enye kutokuwa na umbo linaloshika au uwezo mdogo wa kutokea) asiyeonekana aliyeumbwa kwa moto; mtu habithi/khabithi yaani asiyejali utu wa mwingine. Chembe ya urithisho ya mzazi kwa mtoto wake.

Mwandishi angeandika: “Mashabiki wa Toto Africans wanapojiuliza heshima ya klabu yao itarudi lini, beki wao, Robert Magadula amewatuliza kwa kuwaambia mambo mazuri yanakuja.”

Kichwa kingine cha habari ya gazeti ninalojadili kiliandikwa: “Nyota Gwambina akitaka kiatu FDL.” Badala ya neno ‘akitaka,’ mwandishi angeandika: “Nyota Gwambina ataka kiatu FDL.”

Kichwa kingine cha gazeti hilo kiliandikwa: “Siku 814 bila wenye Simba yao kuwa uraiani.” Wenye Simba ni viongozi au wanachama?

Methali: Ada ya mja, hunena: mwungwana ni kitendo.
[email protected]com
0784 334 096