Fadhila za punda mateke!

18May 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Fadhila za punda mateke!

UKIMTUNZA PUNDA vizuri atasahau na (ashaakum) kukujambia au hata kukupiga mateke unapomkaribia!

Methali hii hutumiwa kumpigia mfano mtu anayetendewa wema na badala ya kuurudisha wema aliotendewa akawa anarudisha ubaya. Huweza kutumiwa kwa mtu asiyekuwa na shukrani.

Kuna mtu anayeitwa Jella Mtagwa. Huyu alikuwa mchezaji kabumbu mahiri wa timu ya Yanga jijini Dar es Salaam aliyesajiliwa kutoka ‘mji kasoro bahari’ (Morogoro). Kwa uhodari wake wa kusakata kabumbu, akateuliwa kuwa nahodha wa Yanga na pia Timu ya Taifa (Taifa Stars).

“Mcheza kwao hutuzwa” chambilecho wahenga. Maana yake mtu anayecheza kwao hupewa zawadi au hutunzwa vizuri. Methali hii hutumiwa kutufunza kwamba mtu anayefanya jambo vizuri au inavyopasa, hutuzwa au hupewa zawadi.

Ndivyo alivyofanyiwa Jella Mtagwa kwani Shirika la Posta na Simu (au Serikali?) iliamua kumtuza kwa kuweka picha yake kwenye stempu zilizotumika kwenye barua. Hapana shaka barua zilizotumwa ndani na nje ya nchi zilifanya ajulikane na wengi na kufahamika kwa umaarufu wake.

Ingekuwa ni wakati wa sasa ambapo timu za Ulaya zinatafuta wachezaji kutoka Afrika, hapa shaka leo hii angekuwa mmoja wa wachezaji walionufaika kucheza Ulaya na kuishi maisha mazuri ya uhakika. Si ajabu tungekuwa tunamzungumzia tofauti na alivyo sasa lakini hakubahatika.

Matokeo yake, bidii na fadhila zote alizozitendea nchi yake kupitia Yanga, Shirikisho la Soka Nchini na Serikali, vyote havimkumbuki!

Hii yanikumbusha walivyosema wahenga kuwa “Kuku wa mkata hatagi, akitaga haangui, akiangua hutwaliwa na mwewe.” Maana yake kuku wa maskini hatagi na hata akitaga hafanikiwi kuwatunza wale vifaranga.

Nilipata mshtuko na simanzi nilipoona picha ya Jella Mtagwa akiwa kazungukwa na mkewe na baadhi ya watu waliokwenda kumjulia hali nyumbani kwake. Ilikuwa vigumu kumtambua mara moja kwa jinsi alivyodhoofika kutokana na maradhi yanayomsumbua.

Huyu ni mtu aliyeitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa enzi zake lakini katika watu waliokuwa naye siku ilipotangazwa na runinga, sikumwona kiongozi yeyote wa Yanga. Ingawa hawakuwepo enzi zake walipaswa kumtembelea mara kwa mara na kumpa msaada wakikumbuka juhudi zake alipokuwa mchezaji wa klabu hiyo maarufu nchini.

TFF nalo lipo kimya kuhusu mchezaji huyo wa zamani kama lilivyo Shirika la Posta na Serikali pia! Ni kama kusema “Iliyopita si ndwele (kitumbe cha mongo), tugange yajayo.” ‘Kitumbe cha mongo’ ni usemi wa zamani wenye maana ya kitu cha kutupwa mgongoni.

Jambo lingine la kufanyiwa kazi ni wachezaji kuwa na chama imara kitakachowatetea na kuwasaidia wanapodhulumiwa haki zao au kutopewa mishahara na stahiki zao kwa muda mwafaka. Mara nyingi wachezaji hulipwa  fedha zao za usajili, na mishahara kwa mafungu tena baada ya kudai kwa mbinde na kutishia kuachana na klabu.

Kadhia hii husababisha baadhi ya wachezaji kuzisusa timu zao kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji Obrey Chirwa aliyekuwa Yanga na sasa yupo Azam. Pia Beno Kakolanya aliyekuwa kipa namba moja wa Yanga ambaye mkataba wake umemalizika akisusa kuwa kwenye kikosi cha Yanga kwa kudai malimbikizo ya mishahara yake.

Ucheleweshaji na ubabaishaji wa stahiki za wachezaji huwaogofya hata wanaotaka kujisajili na Yanga kila wanaposikia ubabaishaji wanaofanyiwa wenzao wa klabu hiyo. Siku hizi mchezo wa mpira ni kazi kama zilivyo zingine. Mfanyakazi hufanya kazi kwa uangalifu na bidii akitegemea kulipwa mshahara wake mwisho wa mwezi.

Fedha hizo humsaidia kulipa kodi ya nyumba, ada za shule kwa watoto wake, chakula na mahitaji mengine muhimu. Sasa kama halipwi mshahara wake kila mwezi ataishi vipi? Awe omba omba? Hili ndilo linalowakatisha tamaa wachezaji wengi kusajiliwa na klabu isiyolipa mishahara kwa wakati.

Jambo hili na mengine yaangaliwe kwa makini na viongozi wapya wa Yanga waliochaguliwa hivi karibuni. Wanapaswa kufanya mambo kwa vitendo badala ya maneno matupu.

Nimalizie makala yangu kwa maneno waliyotuachia wahenga kuwa: “Ahadi ni deni (na deni ijuzie).” Maana yake ahadi ni kama deni, mtu akitoa ahadi lazima aitimize. Methali hii yatufunza umuhimu wa kutimiza ahadi tutoazo.

[email protected]

0784  334 096