Fahamu likizo ya mfanyakazi, malipo yake

22Jun 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Fahamu likizo ya mfanyakazi, malipo yake

AWALI ya yote, ni vema ikaeleweka mapema kuwa likizo zote anayepaswa kupatiwa/kufaidika ni kila mwajiriwa aliyefanya kazi zaidi ya miezi sita mfululizo, au kama alifanya akatoka halafu akafanya tena basi hizo siku zikizidi miezi sita, atakuwa na haki ya kupata likizo.

Tunapoongelea likizo, tuna maana ile yenye malipo. Siyo mwajiri anampatia mfanyakazi likizo lakini mshahara haumpatii. Hiyo ni kinyume cha Sheria elekezi.

Binadamu kwa kawaida katika maisha na shughuli zetu, tunakutana na mengi sana ikiwa ni pamoja na magonjwa, misiba, msongo wa mawazo na vitu vingine vingi.

Mathalani, katika hali ya kawaida binadamu hatuwezi kufanya kazi miezi yote 12 bila ya kupumzika.

Mfanyakazi anahitaji likizo ili aweze kupumzisha mwili na akili yake; kuachana kwa muda fulani na mizunguko au kazi za ofisini za kila siku.

Kimsingi, makala hii iko kumsaidia mwajiri na mwajiriwa kujua jinsi ya kutoa na kuomba likizo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004, Kila mmoja kwa nafasi yake.

Sheria husika inatoa mwongozo wa jinsi ya kutoa likizo na aina ya likizo ambazo mwajiriwa anapaswa kupatiwa/ kufurahia.

Kwa kutilia mkazo zaidi hapa, kama ambavyo nimetangulia kugusia awali, likizo zote anayepaswa kupatiwa/kufaidi ni mfanyakazi/mwajiriwa aliyefanya kazi kwa zaidi ya miezi sita mfululizo; au kama alifanya akatoka halafu akafanya tena basi hizo siku, zikihesabiwa, zisizidi miezi sita atakuwa na haki ya kupata likizo kama sheria inavyotaka.

Isitoshe, tunapoongelea suala zima la likizo; hii ina maana, likizo yenye malipo. Na siyo kinyume na utaratibu huu.

AINA ZA LIKIZO;

LIKIZO YA MWAKA (Annual Leave), Hii ni likizo ya siku 28; ambazo mfanyakazi/mwajiriwa anapaswa kuipata/kuifaidi kila mwaka.

Haijalishi mhusika yuko sekta gani; binafsi au serikalini. Hali kadhalika, wadhifa wake; mlinzi, dereva au mfanyakazi wa ndani.

Endapo wahusika watakubaliana kuwa badala ya kwenda likizo mfanyakazi/mwajiriwa aendelea kufanya kazi, basi mshahara wake wa mwezi mmoja atatakiwa kulipwa mfanyakazi/mwajiriwa huyo: Kifungu cha 31(1)-(10) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.

LIKIZO YA UGONJWA (Sick Leave),

Hutolewa kwa mgonjwa ambaye ni mfanyakazi/mwajiriwa kwa siku 126; siku 63 ni mshahara wote na siku 63 zinazofuata nusu mshahara.

Hata hivyo, mhusika hatoweza kupatiwa/kufaidi likizo hii endapo atashindwa kutoa uthibitisho rasmi kutoka kwa daktari au endapo inahusisha mafao kutoka kwenye makubaliano ya pamoja au hata kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.

Uthibitisho wa daktari ni uthibitisho wa kutoka kwa daktari aliyesajiliwa na serikali: Kifungu cha 32(1)-(4) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004.

LIKIZO YA KIFO (Compassionate Leave), Ni maalum kwa mfiwa. Endapo mfanyakazi atafiwa na mtu wake wa karibu; baba, mama, dada, mke, mtoto.

Atakuwa na haki ya kupata likizo ya siku nne, hutolewa pia, endapo mfanyakazi/mwajiriwa anauguliwa na mtoto mdogo.

Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 34(1)-(3) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.

LIKIZO YA UZAZI (Maternity Leave),

Likizo ya uzazi kwa mwanamke (Maternity Leave), ni maalumu kwa kinamama. Mama anapaswa kupata likizo ya siku 84 na endapo ikiwa mhusika atajifungua watoto mapacha, basi anapata likizo ya siku miamoja (100).

Sambamba na kupatiwa muda wa saa mbili (2) ya muda wa kazi kila siku kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto/watoto wake.

Muhimu

Mathalani, mtoto akifariki ndani ya mwaka mmoja (1) mhusika atatakiwa kupatiwa likizo ya uzazi tena; endapo atashika mimba nyingine.

Na zaidi sana, taarifa ya likizo husika itatolewa kwa mwajiri ndani ya miezi mitatu (3) kabla, juu ya lini likizo husika inachukuliwa.

Mama anayenyonyesha haruhusiwi kufanya kazi zinazohatarisha afya yake na ya mtoto/watoto wake.

Mama mjamzito anaweza kuchukua likizo yake wakati wowote, wiki nne (4) kabla ya kujifungua; lakini inaweza kuwa mapema zaidi endapo daktari atathibitisha hilo: Kifungu cha 33(1)-(11) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini na. 6 ya mwaka 2004.

LIKIZO YA UZAZI (Paternity Leave)

Hii ni likizo maalumu kwa wanaume ambao wake zao wamejifungua. Ni likizo ya siku tatu na inapaswa kuchukulia ndani ya siku saba kutoka mke ajifungue.

Hatua ya msingi ni mwajiri kutaarifiwa mapema na uthibitisho kuwa aliyejifungua ni mke halali: Kifungu cha 34 (1)-(3) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na.6 ya Mwaka 2004.

Mwisho, haki ya likizo ni ya wafanyakazi/waajiriwa wote (kama sheria inavyoelekeza na kutaka); pia ni marufuku mwajiri kumfukuza/kumfuta kazi mfanyakazi/mwajiriwa wakati wa/yupo likizo. Naomba kuwasilisha.