Fahamu msingi wa wajibu kwa kila raia kujua sheria za nchi

15Jun 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Fahamu msingi wa wajibu kwa kila raia kujua sheria za nchi

HAKUNA jamii duniani isiyo na taratibu au misingi ya namna ya kuishi na kufanya shughuli za kila siku.

Jamii yeyote isiyokuwa na utaratibu, basi migongano itakuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.

 

Hivyo lazima kuwe na utaratibu maalumu ambao jamii hii utaishi kwao, utaratibu huu utaongoza au utaathiri nyanja zote za maisha katika jamii hiyo. Utaathiri nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na hata utamaduni wa eneo hilo. Hivyo tunaweza tukaita utaratibu huu sheria.

Tuangalie basi umuhimu wa mwananchi wa kawaida kufahamu sheria katika jamii, japo chache ni hizi zifuatazo;

Ibara za 12 hadi 29 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inaelezea juu ya Haki na Wajibu wa kila mwananchi.

Hivyo ni jukumu la kila mwananchi kusoma na kuzifahamu (vizuri) Sheria za Nchi: Zaidi sana, *Ibara ya 26(1)-(2)* ya katiba tajwa.

Hapo utafahamu mipaka ya kutumia uhuru na haki yako, hii ni kwa sababu hakuna haki isiyokuwa na wajibu/mipaka.

Kwa mfano, Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi inatoa uhuru wa kujieleza na kutoa maoni, lakini kumewekwa mipaka ya kutumia uhuru huo katika Ibara ya 30 ya katiba ya nchi, kwamba haki na uhuru wowote ule usitumiwe kwa namna ya kuingilia na kuathiri uhuru na haki za watu wengine.

Utatambua kuwa ni wakati gani utahesabiwa kuwa na hatia. Si kila mtu anayefahamu kuwa ni wakati gani atakuwa na hatia.

Ibara ya 13(6)(b), Katiba ya Jamhuri ya Muungano, 1977 (kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara) inaeleza kuwa “mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai hatahesabika kuwa na hatia ya kosa mpaka pale itakapothibitika kuwa ametenda kosa hilo.”

Kwa maana hiyo atakuwa na haki zote anazostahili mtu asiye na hatia mpaka pale itakapothibitika kuwa ana hatia ya kosa hilo.

Haya yote, mtu hatoyafahamu kama hana uelewa wa sheria au hapendi kusoma sheria au hataki kufahamu utaratibu wa kisheria.

Mathalani, kwa mshtakiwa wa kosa la jinai hatofahamu haki zake za msingi, ikiwamo (ile) ya kuwakilishwa na kutetewa na wakili.

Kifungu cha 54(1) cha Sheria ya Mwenendo ya Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (Criminal Procedure Act Cap. 20) inaonyesha kutambua Haki ya Mtuhumiwa kuruhusiwa au kupatiwa Utetezi/Msaada wa Kisheria (Legal Aid); sanjari na 2, 21(1)-(3), 22(a)-(c), 27(a)-(b) na 44(1)-(2) vifungu vyote vya Sheria mpya ya Msaada wa Kisheria, 2017.

Hii imekwenda mbali zaidi kwa kuruhusu fursa husika kwa mashauri yote, jinai na madai!

Kimsingi, mtu asiyejua haya hawezi kudai haki yake pale atakapokuwa chini ya mikono ya sheria. Ndiyo pale atakapolazimika kutoa rushwa au kufanya vitendo vingine visivyofaa kwa kuwa hajui utaratibu wa kufuata kisheria.

Utajua utaratibu wa kupata haki yako pale inapodhulumiwa au inapoonekana kutaka kupokonywa na mamlaka za kiserikali au mamlaka zingine halali au mtu mwingine yeyote.

Utaishi kwa kujiamini, kwani kila jamii ina utaratibu maalumu. Watu wengi wameshindwa kuishi kwa kujiamini kwani kila wakati wanajihisi kuwa ni wenye hatia.

Wengi wanaishi bila kufuata utaratibu na hivyo kujijengea hofu kubwa. Ukifahamu sheria utaishi kwa kujiamini katika jamii yako kwani hutavunja utaratibu bali utafuata utaratibu mahususi wa kisheria. Kwa maana nyingine ukiifahamu sheria, utakuwa huru na jamii yako.

Utaweza kulinda na kuitetea jamii yako, ni jukumu la kila mtu au kila Mtanzania kulinda na kuitetea jamii yake dhidi ya vitendo viovu/ukiukwaji wa haki.

Sheria ndiyo inaelekeza hili ni kosa na lile sio kosa, sasa, je, utatambuaje kuwa hili ni kosa kisheria bila kuifahamu sheria au kuwa na dodoso za kisheria? Hivyo jamii itabaki bila utetezi kwani wanajamii hawana haja ya kufahamu misingi ya kuendeshea jamii zao.

Utakuwa na uwezo wa kutetea maslahi ya watu wengine na kulinda maslahi ya taifa lako, maslahi binafsi ya watu na hata maslahi ya taifa kama yamepokwa (chukuliwa) na watu wenye nia mbaya mbele ya macho ya wananchi, na wananchi hawakuchukua hatua zozote kwasababu hawajui kuwa ni wajibu wao.

Wananchi walio wengi hawajui kuwa wana wajibu wa kulinda na kutetea maslahi ya taifa lao.

Ibara ya 27(1)-(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kwa mara imeweka wajibu wa kila mwananchi kulinda na kutunza mali za umma, mali zinazomilikiwa na watu kwa ujumla wao pia kuheshimu mali binafsi za mtu mwingine.

Haya yote kila Mtanzania atayafahamu pale tu atakapokuwa na desturi ya kusoma makala mbalimbali za kisheria.

Chukua muda wako, soma sheria vizuri (hususan zile zinazoelekeza haki za kiraia na wajibu), ili ufahamu haki na wajibu wako uliowekwa na sheria katika jamii yako.

Ni wazi kuwa sio kila mtu anafahamu au kutambua wajibu wake katika kulinda maslahi na mali za taifa lake.

KUMBUKA: Kutokufahamu sheria hakutakuwa utetezi pale utakapofanya kosa (Kilatini- Ignorancia juris non excusant; Kiingereza-ignorance of the law is not an excuse): Kifungu cha 8, Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.

Tena, ili kupunguza matendo maovu kwenye taasisi za umma na binafsi na jamii kwa ujumla ni vema basi tukafahamu sheria.

Ile kasumba ya kwamba sheria ni ngumu itoke kwenye kamusi na misamiati ya utashi na akili zetu. Jifunze sheria kwa manufaa yako binafsi na taifa kwa ujumla.

“SHERIA NI RAFIKI WA UHURU WAKO/WETU SOTE”. Naomba kuwasilisha! (Soma Gazeti la Nipashe Uk. 21 kila siku ya J'mosi)