Faida ya kuwekeza kwenye dhamana za serikali

15Apr 2016
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mtazamo kibiashara
Faida ya kuwekeza kwenye dhamana za serikali

WAPENZI wasomaji wa safu hii leo, tunahitimisha safari ndefu tuliyoianza kwa wiki kadhaa, ambayo tuliangalia kwa upana jinsi ya kuwekeza kwenye hati fungani za serikali.

Hati fungani ama dhamana za serikali kwa jina jingine, ziko za aina mbili.

Yaani za muda mfupi na za muda mrefu, kama tulivyoona na kuendelea kukumbushana mfululizo katika safu hii.
Wiki iliyopita, tuliona sababu ya serikali kuuza dhamana zake kwenye minada inayoendeshwa na Benki Kuu (BoT).

Baadhi ya sababu hizo ni pamoja na kuiwezesha serikali kukopa fedha kutoka wa wananchi wake, ili iweze kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo, kama vile ugharimiaji wa miradi yake.

Kwamba dhamana za serikali, ni moja ya njia ambayo serikali huitumia kupata fedha kutoka vyanzo vya ndani.
Sababu nyingine tuliyoiona ya serikali kuuza dhamana zake, ni kuiwezesha kuziba nakisi ya bajeti ya matumizi ya kawaida.

Lakini pia tukasema inafanya hivyo ili kudhibiti ujazo wa fedha unaosababishwa na mfumuko wa bei.

Tumalizie leo kwa kutaja sababu nyingine ya serikali kuuza dhamana zake, kabla hatujaangalia faida kwa mfanyabiashara ya kuwekeza kwenye hati fungani za serikali, ambayo ndiyo eneo litakalohitimisha mada yetu hii.

Sababu nyingine ya serikali kuuza hati fungani zake, ni kuiwezesha kuainisha mwelekeo wa riba zinazotolewa na taasisi zingine za kifedha.

Sasa kuna faida mbalimbali kwa mfanyabiashara na mwananchi mwingine wa kawaida za kuwekeza katika soko la dhamana za serikali.

Kwanza kuwekeza katika dhamana za serikali ni salama, kwani kimsingi serikali haitarajiwi kushindwa kulipa wadai wake wakati dhamana zinapoiva.

Mfanyabiashara anayewekeza katika hati fungani za serikali, anapaswa kuwa na uhakika kuwa kipindi cha kuiva kwa dhamana zake kinapofika, serikali kupitia Benki Kuu (BoT), hulipa mara moja kiasi chote cha fedha iliyowekezwa pamoja na riba ama faida yake.

Kwamba kuna usalama zaidi wa fedha zake, pengine kuliko kuwekeza kwenye taasisi zingine za kifedha.

Faida nyingine ya mfanyabiashara kuwekeza kwenye dhamana za serikali, ni kutokana na ukweli kwamba dhamana hizi zinahamishika, na kwa hali hiyo mfanyabiashara anayewekeza anaweza kuziuza kabla ya muda wake wa kuiva.

Hii ina maana kuwa mfanyabiashara, anaweza kuwa amenunua dhamana za serikali kwa mfano za muda mfupi wa siku 35.

Kwamba kabla ya dhamana hizo hazijaiva katika muda huo kwa maana siku hizo 35, na ikatokea pengine akahitaji fedha kwa ajili ya dharura iliyojitokeza, anaweza akaziuza na kutatua dharura yake ya kibiashara ama ya aina yoyote ile.

Lakini faida nyingine ya kuwekeza kwenye hati fungani za serikali ni kuwa, mfanyabiashara anaweza akazitumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo ya kuendeleza biashara zake.

Kwamba tuseme mfanyabiashara amwekeza kwenye dhamana za muda mrefu, yaani zile za kuanzia miaka miwili, mitano, saba, 10 ama 15, ana weza kabisa kuzitumia kuomba mikopo kwenye taasisi zingine za kifedha wakati akisubiri ziive.

Na faida ya mwisho kwa muktadha wa safu hii, ni kuwa kama tulivyoona huko nyuma dhamana za serikali zina kiwango cha faida inayoridhisha.