Faini hizi ni za kukomoa au kurekebishana?

07Jan 2020
Salome Kitomari
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Faini hizi ni za kukomoa au kurekebishana?

HAKUNA ubishi kuwa kwa sasa barabarani, hasa jijini Dar es Salaam, kuna nidhani kubwa kwa madereva kuheshimu alama za barabarani na watembea kwa miguu.

Natamka ni nidhamu, ikilinganishwa na miaka ya nyuma ilikuwa vurugu tupu, kwa kuwa mwenye nguvu ndiye alipita, madereva wa daladala na baadhi ya magari binafsi ambao walitanua na kupita maeneo yasiyotakiwa bila ya kuguswa na yeyote, jambo lililoharibu barabara nyingi.

Ilikuwa kama mashindano ya watu wasio wastaarabu barabarani kiasi cha kuwaweka kwenye hali ngumu watumiaji wengine wa barabara.

Kwa sasa, askari wa usalama barabarani wapo katika maeneo mengi na wengine hujificha, ili kuona utekelezaji wa utii wa sheria bila ya shuruti na inapolazimika sana wanatumia shuruti, kwa kuandika faini kwa madereva.

Kwa sasa, maeneo yenye vibao vya ‘50’ kwa barabara za mikoani, madereva wanaheshimu na hakuna mwendokasi, kwa kuwa wanajua watapigwa picha na kukamatwa mbele kwa kuonyeshwa picha ya gari, mwendo aliozidisha na kibao cha ‘50’ kinavyoelekeza.

Jitihada hizi, operesheni za kila mara mara na ubunifu umesidia kupunguza ajali nyingi za mwisho wa mwaka ambazo zilitokana na mwendo kasi au uzembe wa madereva. Kwa sasa wako makini, kwa kuwa wanajua nini kitafuata iwapo watavunja sheria hizo.

Pamoja na pongezi ya kazi nzuri inayofanywa na askari hao lakini yapo maeneo yanahitaji marekebisho makubwa kwa kuwa sasa imegeuka kuwa adhabu na maumivu kwa madereva kuliko inavyofikiriwa.

Jiji la Dar es Salaam linaoongoza kwa faini ambazo ni za kuumiza au kubambikia madereva na hilo nitalisema nikiwa na mifano halisi ya maeneo ambayo ndiyo la askari kuvizia, jambo linalotoa taswira kwa sasa ni kuviziana zaidi kuliko kuwafanya madereva watii sheria bila shuruti.

Katika barabara ya Bagamoyo nyuma kidogo ya makutano ya barabara ya Goba na Bagamoyo, kwa dereva anayetokea Tegeta upande wa kushoto kuna kituo cha abiria wa daladala na nyuma kidogo kulikuwa na alama ya ‘zebra’ zilizofutika kwa sasa. Mbele kidogo, ndiko askari hujificha na kujitokeza kwa kasi barabarani wanapoona dereva hajasimama eneo hilo.

Kinachonisukuma kuandika haya ni iwapo askari hao wanajua kwamba alama za pundamilia zinaonyesha kuvuka kwa watembea kwa miguu zimechorwa na kuonekana kwa madereva au wanaamini kuwa barabara hiyo inatumiwa na madereva wenyeji kila siku hivyo wamekariri eneo hilo.

Kinachofanyika kwa askari wanapoona kuna mtu amesimama upande wowote wa barabara na gari likapita bila ya kusimama, wanamkamata na kuambiwa hajaheshimu alama za pundamilia na kuandikiwa faini. Lakini, cha kushangaza alama husika hazipo.

Cha kujiuliza hapo, askari wapo pale kukusanya mapato au kuangalia wakosaji ambao hawapo. Ninasema wakosaji hawapo kwa kuwa eneo hilo hakuna kibao wala alama kwenye lami zinazoonyesha dereva anapaswa kusimama kuruhusu watembea kwa miguu kupita.

Eneo lingine ni Majumba Sita, baada ya kutoka Uwanja wa Ndege ukiwa unaelekea Ukonga, jijini Dar es Salaam, katika makutano ya barabara za Kinyerezi na Nyerere ambako kuna taa.

Eneo hilo lina askari wengi na kuna foleni. Kinachoviziwa hapo ni wale wanaoshindwa kukaa kwenye foleni ya mstari mmoja wakati wa kwenda na kurudi kutokana na mabadiliko ya barabara kuwa nyakati za asubuhi ni njia mbili kwenda mjini na njia moja kwenda Ukonga.

Mbaya zaidi hakuna kibao chochote cha kutoa elimu ya jambo hilo bali kinachofanyika ni kuvizia wakoseaji wowote ili watozwe faini, jambo linaloonyesha kuwa hakuna nia njema ya kuwafanya madereva watii sheria bila shuruti bali kukusanya fedha kutoka kwao.

Sehemu nyingine ambazo ni maumivu kwa madereva ni kwenye makutano ya barabara ambako kuna taa, lakini hakuna taa za kuelekeza madereva wa pande nyingine bali wanapaswa kukadiria au kutumia akili za kuzaliwa na kwa dereva mgeni anajikutana kwenye wakati mgumu.

Mfano ukiwa umetokea TMDA unakwenda Ubungo hakuna taa ya kukuelekeza sasa unaruhusiwa kukatiza barabara hiyo na badala yake inaruhusu magari yanayokwenda mabibo ukipita ikiwa hivyo ni sawa, lakini iwapo utapita wakati magari yanayotoka Tabata kwenda Mabibo yanakatiza, linahesabiwa ni kosa na faini inamhusu dereva.

Eneo jingine ni Mwenge kwa anayetokea Coca Cola kuelekea Posta, akikatiza wakati magari yaliyotokea uelekeo wa Bagamoyo yanakatiza, inaonekana ni kosa au wakati yaliyotokea Ubungo yanakatiza, ni kosa bali anatakiwa kusubiri yanayotoka upande aliyopo kuelekea Ubungo, ndiyo akatize.

Katika eneo hilo hali ni ileile kwa aliyetokea uelekeo wa ITV anakwenda Ubungo, akikatiza wakati magari mengine yanapishana, anakutana na askari waliojificha kwenye vituo wakiwawinda watu wa namna hiyo.

Pia madereva wanaotokea uelekeo wa Tegeta na kwenda Coca Cola nao wanasubiriwa kukamatwa na wale wanaotokea Ubungo wanataka kuingia barabara ya Bagamoyo.

Kwa ujumla, alama za barabarani hususani ‘pundamilia’ zimefutika kwenye maeneo mengi, kiasi cha kuwafanya madereva kutaabika na kushindwa kufanya maamuzi na kukutwa na mkono wa sheria.