Familia ya mke imechangia ndoa yangu kuvunjika!

14Feb 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Familia ya mke imechangia ndoa yangu kuvunjika!

MPENZI msomaji, safu hii haiishiwi vituko. Wiki iliyopita kituko chetu kilibeba kichwa cha maneno ‘Nilimsomesha, amepata kazi akanitosa! Nifanyeje?’ Jamaa bado anashangaa imekuwaje mwenzake amgeuke.
Lakini yawezekana ipo sababu kama msomaji wetu mmoja alivyotoa ushauri ufuatao:

Kijana wangu kwa uwezo wa Mungu utapata mke mwema ambaye atakuliwaza kama nilivyopata mimi baada ya kumkosa niliyedhania atanifaa katika maisha yangu. Hakuna anayejua siri ya Mungu, tulizana fanya kazi zako kwa utulivu, na jitahidi kuwafanyia wema watu wote,hata yule anayekufanyia ubaya.

Jitahidi kuyahifadhi maneno yangu haya na kuyafuata, naamini siku moja utakumbuka baada ya kuona matokeo yake. Ahsante. Wenu mzee Salim.

Naam. Mambo ndio mambo. Hebu leo tuangalie kingine. Kwa ujumla watu wengi wanayo mitihani ya kimaisha hadi basi! Hakika, Maisha ndivyo Yalivyo. Msikilize naye huyu yaliyomsibu kama anavyosimulia.

Anasema hivi; Dada mimi nilikuwa na mpenzi toka mwaka 2001. Tukajaliwa kupata mtoto wa kwanza mwaka 2003. Ilipofika mwaka 2006 tukafunga ndoa na baada ya miaka miwili tukapata mtoto mwingine.

Nikapata safari kwenda mkoani Kilimanjaro ambako nilikaa miezi sita kisha nikarejea nyumbani Pangani. Nilimkuta mke wangu na watoto wakiwa salama, maisha yakaendelea huku tukifurahia vyema ndoa yetu.

Miaka miwili mbele dada yangu ndoa ikaanza misukosuko, ugomvi, fujo, makelele, huku familia ya mke ikionekana kuchangia kwa kiwango kikubwa fujo ya ndoa yetu. Hali hiyo ilipelekea hata mke wangu kunikimbia na kuniachia watoto.

Kibaya zaidi aliondoka na pesa yote iliyokuwa kama akiba yetu nyumbani bila ya kujali ameacha watoto. Nilijaribu kuwasiliana naye baada ya miezi mitatu akarudi nyumbani. Akakaa mwezi mmoja tu akaondoka tena.

Nikambembeleza tena akarudi, tukakaa miezi miwili familia yake ikaanza taabu tena naye akaondoka. Ndipo nilipoamua nitulie miaka mitatu huku nikilea watoto wangu. Lakini mke wangu bado nampenda sana.

Ndipo nilipoamua kutafuta mke mwingine kwa ajili ya kunisaidia malezi ya watoto kwani shughuli zangu zilikuwa zinakwama. Aliposikia nimeoa akaja na kutaka kufanya fujo lakini nilifanikiwa kuzuia fujo hiyo akaenda kunishitaki.

Nikaletewa barua ya wito na nilipokwenda nikaikuta familia yake wamejazana pale ofisini kwa Mtendaji. Shauri lilipoanza kusikilizwa nikajikuta naingiwa na hasira na kuondoka eneo lile.

Baadaye yule mke wangu aliamua kwenda kwa dada yangu kutaka suluhu. Dada aliniita tukaongea lakini nilihisi kama alitaka kunivurugia nyumba na mke wangu wa sasa. Napo pia nikaondoka, yule binti naye akaolewa.

Baada ya miezi sita akaachika, akapata bwana mwingine naye pia ndoa yake haikudumu. Mimi nimemhurumia sana nikiangalia ni mzazi mwenzangu. Pia bado nampenda sana ila hataki kabisa hata kuwasiliana na mimi, ila kiukweli bado nampenda.

Nasema hivi ikizingatiwa kuwa mapenzi yetu hatukuyakatisha kwa kuchokana bali yalikatishwa na watu wa upande wa kwao, ila familia ya upande wangu tunampenda sana.

Sasa dada yangu naomba ushauri wako, natumai utanisaidia na kunifanya niwe mpya kimaamuzi. Ni BK wa Pangani, Tanga.(0717765114).

Mpenzi msomaji, bila shaka umempata vema mwenzetu huyo kuhusu misukosuko ndani ya ndoa yake. Ukiangalia kwa undani, wawili hawa bado wanapendana. Ndio maana mume amekuwa akimtafuta mkewe arudi pale anapokuwa ametimkia kwao.

Bibie naye anapotafutwa na mumewe hurudi lakini baada ya muda hutimka tena. Ona ilifikia hatua akaenda kuolewa, japokuwa akaachika mara mbili, huku mume akioa mwingine ambaye wanaishi hadi sasa. Ila bado mume huyu anampenda mkewe wa awali (mama watoto) na kumhurumia mapito anayopitia.

Lakini hapa ninachokiona ndoa hii ilivurugwa na ndugu za familia ya mke ambao ndio wamekuwa wakimlisha maneno, ukiwemo unafiki hata kutokea yote yaliyotokea. Lipo tatizo hapa ambalo limejificha na chanzo kikubwa ni ndugu za mke.

Ipo roho ambayo imesimama ikiapa kwamba wawili hawa hawataishi kwa amani. Nitaieleza katika uchambuzi wa wiki ijayo, hivyo msomaji wangu usikose nakala yako kwani utaweza kujifunza Mungu anasema nini kuhusu roho hiyo!

Nini maoni na ushauri wako kuhusu sekeseke la kimaisha la kijana wetu tuliyemzungumzia hapo leo? Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; _HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected].com_ au _HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected]