Funzo la mjinga taabu

04Jun 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Funzo la mjinga taabu

‘TAABU’ ni hali ya kuwa na shida, mashaka, kero au usumbufu.

Maana yake mtu mjinga huishia kujifunza kutokana na shida au taabu kwa sababu ya kupuuza ushauri. Methali hii hutumiwa kumwelezea mtu anayepuuza ushauri anaopewa.

 

Nimekuwa nikiwakosoa waandishi wanaotumia maneno ya kihuni au kuchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza kana kwamba maneno ya kigeni wanayotumia hayamo kwenye Kiswahili ilhali (jambo linaloelezwa ni kinyume cha ukweli ulivyo) yamo, ila ni uvivu wa waandishi kuyatafuta kwenye kamusi mbalimbali za Kiswahili.

Kutokana na umaarufu wa lugha ya Kiswahili, vituo vingi vya redio duniani hutangaza taarifa zao za habari kwa lugha ya Kiswahili: Redio za Umoja wa Mataifa, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Urusi, India, Japan na nchi kadhaa za Afrika. Kama hiyo haitoshi, sasa baadhi ya nchi za Afrika zinaiomba Tanzania kuzipelekea walimu wa kufundisha Kiswahili. Hii yadhihirisha jinsi lugha ya Kiswahili inavyopendwa duniani.

Baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika wameshauri Kiswahili kiwe lugha ya taifa ya Afrika yote. Ndo maana wahenga walijua hili mapema waliposema: “Usijivunie cha mwenzako.” Maana yake usijivunie kitu ambacho si chako. Methali hii yaweza kutumiwa kutukumbusha kuwa hatupaswi kuvionea fahari vitu vya wenzetu bali vitu vyetu wenyewe. 

Pamoja na mapenzi waliyonayo watu wa mataifa mbalimbali, sisi ambao ndiwo wenye asili ya lugha ya Kiswahili, ama hatujui thamani yake au tunaidharau lugha hii adhimu (iliyo na sifa na heshima kubwa) inayohusudiwa (kutamani mafanikio, kitu au uwezo mwingine; kitendo cha mtu kutamani kuwa kama alivyo mwingine) duniani kote.

Nimeandika mara kadhaa umuhimu wa kuienzi lugha ya Kiswahili lakini kadiri ninavyosisitiza ndivyo waandishi wenzangu wanavyozidi kuingiza maneno ya kihuni au kuchanganya Kiswahili na Kiingereza kwenye habari na makala za magazeti yao kama ilivyo redioni na kwenye runinga!

Takriban robotatu ya Watanzania hawajui ‘nasuri’ ni kitu gani ila wanajua ‘fistula’ ambalo ni neno la Kiingereza. ‘Nasuri’ (Kiswahili cha ‘fistula’) ndilo neno la Kiswahili linalopaswa kutumiwa badala ya lile la Kiingereza -- ‘fistula.’

‘Nasuri’ ni ugonjwa uwapatao wanawake ambapo tundu la mkojo limepasuka na kusababisha mkojo utoke mara kwa mara bila kukusudiwa; tundu linalotokea katika misuli kati ya uke na kibofu cha mkojo au kati ya uke na njia ya haja kubwa ama sehemu zote mbili.

Tukiacha hilo, baadhi ya maneno yatumiwayo vibaya ni: lakini, kwa niaba yangu, wakilisha, mwisho wa siku n.k. ‘Lakini’ ni tamko la kuonesha kasoro ya jambo; neno linaloonesha uwepo wa upungufu, au hitilafu.

Neno hili hutumiwa sana na wanasiasa wanapoeleza kazi zilizofanywa. Kwa mfano: “Serikali imejenga barabara nyingi nchini lakini pia inajenga njia ya reli ya kisasa kati ya Tanzania na Rwanda …” Neno ‘lakini’ halikutumika ipasavyo kwani ni neno linaloonesha upungufu, kasoro au hitilafu ya jambo. Ni sahihi kusema: “Serikali imejenga barabara nyingi nchini, pia reli ya kisasa kati ya Tanzania na Rwanda …” 

Wanasiasa wanapotoa hotuba husikika wakisema: “Kwa ‘niaba yangu’ namshukuru kiongozi wetu mpendwa kwa kutimiza ahadi yake ya kutupatia maji safi na salama baada ya miaka kadhaa.” Neno ‘niaba’ maana yake ni badala ya mtu au watu wengine. Isemwe: “Kwa niaba ya wananchi wa jimbo langu, namshukuru kiongozi wetu mpendwa kwa kutimiza ahadi yake ya kutupatia maji safi na salama …” Yaani unashukuru kwa niaba ya waliokutuma.

‘Mwisho’ maana yake ni hali ya kumalizika; tamati, ukomo wa jambo, hitimisho. Wengi wetu wamezoea kusema, kwa mfano: “Mwaka jana nililima sana lakini ‘mwisho wa siku’ sikuambulia kitu.”

Kilimo hakifanywi kwa siku moja hata isemwe ‘mwisho wa siku’ kwani hufanywa kwa msimu yaani kipindi maalum katika mwaka ambapo hali ya hewa mahsusi au jambo fulani hutokea. ‘Siku’ ni muda wa saa 24 kuanzia saa moja asubuhi hadi asubuhi inayofuata. Sijui mtu awezaje kulima na kuvuna kwa siku moja!

Vilevile kuna tofauti ya wakilisha na wasilisha. ‘Wakilisha’ kwa muktadha ninaoujadili ni neno lenye maana mbili: Kwanza ni kitendo cha kufanya jambo kwa niaba ya mtu mwingine. Kwa mfano, Rais, kiongozi au mtu yeyote aweza kumteua mwakilishi (mtu anayefanya jambo kwa niaba ya mwingine/wengine) ili amwakilishe kwenye tukio fulani.

‘Wasilisha’ (kitenzi elekezi) ni fikisha kitu au ujumbe mahala fulani; toa maelezo au mhadhara kwa kikundi cha watu au mbele ya watu.

Neno ‘chama’ lina maana zaidi ya moja. Kwanza ni kikundi cha watu wenye itikadi au lengo moja; kundi lenye kufuata kaida au silka fulani zenye kuegemea dini, siasa au misimamo ya jamii, uchumi au jambo lingine lolote lenye maazimio maalumu. Kwa ufupi ni muungano wa watu wenye lengo moja.

Ni upotoshaji wa lugha ya Kiswahili kusema au kuandika: ‘chama la wana’, ‘chama lao’, au ‘chama letu.’ Ufasaha wa Kiswahili ni ‘chama cha wana’, ‘chama chao’ na ‘chama chetu.’ Siku hizi klabu ya kandanda yaitwa  ‘chama letu’ au ‘chama lao’ na kushabikiwa sana na waandishi wa habari za michezo!

Neno lingine lililozoeleka sana kwenye magazeti ya michezo ni ‘mzuka’ na waandishi hudhani ni neno la sifa kumbe sivyo. Maana sahihi ya ‘mzuka’ ni kiumbe kisichoonekana ila hudhaniwa kuwa kinaishi na huweza kumtokea mtu; pepo. Pamoja na ukweli huu, twasoma kwenye magazeti ya michezo kuwa mchezaji fulani apandisha mzuka kumbe maana yake ni mchezaji kutokewa na pepo! Mchezaji wa aina hiyo hupungwa pepo?

Methali: Asiye na nadhari, siandamani naye.

[email protected]

0784 334 096