Fursa kuchangamkia kilimo cha Bonde Bugwema, Musoma Vijijini

17May 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Fursa kuchangamkia kilimo cha Bonde Bugwema, Musoma Vijijini

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imeingia mkataba na Halmashauri ya Musoma, kwa ajili kuboresha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji, katika bonde la Bugwema.

Mbali na kilimo hicho, bonde hilo lenye zaidi ya ekari 800 limegawanywa pia kwa ajili ya malisho ya mifugo, kujenga shule, zahanati na ofisi ya serikali ya kijiji na taasisi nyingine za serikali.

Mkataba huo ulifanyika hivi karibuni mbele ya viongozi mbalimbali, akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na wengine. Benki hiyo itatoa vifaa vya kilimo kwa wananchi.

Utaratibu wa kurejesha mkopo unalenga kuhakikisha unawanufaisha wakulima wa vijiji vya Kata ya Bugwema, watakaokuwa ndani ya mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji.

Pembejeo zitakazotolewa na mwekezaji ni zana za kisasa za kilimo, mbegu, mbolea na huduma nyingine pale zitakapokuwa zinahitajika, huku mazao ya kuanzia yakiwa ni mpunga, mahindi na vitunguu.

Inaelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Musoma, John Kayombo, kuwa katika awamu ya kwanza, wanufaika watakuwa wakazi wa Bugwema na kwamba kadri mradi utakavyokuwa unaendelea, wakazi nje ya Bugwema watakaribishwa.

Kwa utaratibu uliopo ni kwamba mwekezaji akisharudisha gharama zake, mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji utakabidhiwa kwa wananchi, chini ya usimamizi wa halmashauri yao.

Inaelezwa, kuwa gharama kamili za mwekezaji zitajulikana baadhi ya miezi michache ijayo na kwamba, kwa sasa anaendelea na kukamilisha mambo kadhaa yatakayomwezesha kufanikisha mradi huo.

Nimeanza kueleza kwa kirefu kile ambacho kinaendelea katika bonde hilo, lengo ni kutaka kuwaambia wakazi wa Bugwema kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kunufaika na kilimo hicho.

Bugwema ipo jimbo la Musoma Vijijini, ambalo kwa sasa limejikita kwenye mambo matatu, ambayo ni kuboresha elimu, huduma ya afya na kilimo cha umwagiliaji kikiwamo cha bustani.

Kazi hiyo inafanyika kwenye kata vijiji 68, huku mbunge wa jimbo hilo, akigawa bure mbegu za mazao mbalimbali zikiwamo za alizeti ambalo, ni zao jipya katika jimbo hilo na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mwekezaji katika bonde hilo ni moja ya mikakati ya kuinua kilimo, ili kiweze kuwa na tija jimbo humo, kwa wananchi kupata mazao ya chakula na biashara, hivyo wananchi hawana budi kuchangamkia fursa hiyo.

Kupata mbegu bure, pia kupata mwekezaji ni hatua nzuri inayoweza kuwafanya wakulima wakainuka kiuchumi iwapo watachangamkia fursa hiyo, hasa vijana ambao hukimbilia mijini badala ya kujikita katika kilimo.

Vijana ni nguvukazi katika nyanja zote, lakini kwenye kilimo wamekuwa ni wazito, baadhi yao wamekuwa wakikwepa kukimbilia mjini kutafuta vibarua, kama vile kilimo hakina tija.

Musoma Vijjini mmepata mwekezaji katika bonde la Bugwema. Bahati nzuri mbunge wenu amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Hivyo, njia pekee ya kufanikisha kilimo hicho ni wakulima wa maeneo husika kushiriki kikamilifu na hatimaye mradi huo kuwa mkubwa zaidi wa kuweza kunufaisha jimbo zima badala ya Bugwema pekee.

Ikumbukwe kuwa maendeleo ya uhakika kwenye kilimo hayawezi kupatikana, kama wakulima hawatazingatia kile ambacho wanaelekezwa na wataalam wa kilimo.

Najua kwamba, kwa muda mrefu wataalamu wa kilimo wa Halmashauri ya Musoma Vijijini, wamekuwa wakihamasisha kuhusu mbinu za kisasa kwenye kilimo ili kupata mazao mengi.

Mbinu hizo ambazo wameelekezwa ndizo wanapaswa kuzitumia kwenye kilimo cha umwagiliaji katika bonde hilo la Bugwema lililoanzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere katika miaka ya 70.