Fursa ndio hizo shambani, wenye taaluma kazi kwenu

09Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Fursa ndio hizo shambani, wenye taaluma kazi kwenu

WAHITIMU wa vyuo vya kilimo kote nchini, wamekuwa wakihimizwa kutumia fursa ya uhaba wa maofisa ugani ulioko nchini, kwa kwenda kutoa elimu kwa wakulima na kuanzisha mashamba ya mfano kwa wakulima.

Lengo la kufanya hivyo ni kufungua mashamba ya mfano na watoe huduma kwa wakulima, pia ikiwa sehemu ya kujiajiri, kwa vile hivi kwa sasa nchi imebadilika. Wapo wakulima wanaotafuta wataalamu wa kilimo.

Wakulima wanafanya hivyo ili waweze kupata huduma kwenye shughuli zao za kilimo na wapo tayari kulipia wataalamu. Ni bahati mbaya, wataalamu wa ugani hawapatikani kwa ajili ya kazi hiyo.

Fursa hii inatajwa na Naibu Waziri Kilimo, Omari Mgumba, kwamba inapaswa kuchangamkiwa na vijana waliohitimu vyuo, ili waweze kujikwamua kiuchumi, badala ya kukaa kusubiri ajira za serikalini.

Ni kweli kilimo kimebadilika na kinahitaji ushauri wa watalaamu, hivyo kama kuna wakulima wanaohitaji ushauri wa wataalamu hao, basi ni vyema wakachangamkia fursa inayotokana na uchache wa maofisa ugani.

Si kutoa ushauri wa kitaalamu tu, bali vijana hao pia wanatakiwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu bora za mazao, kwa vile kuna uhitaji mkubwa wa mbegu nchini.

Kwa maelezo hayo ya naibu waziri, ni wazi kwamba hakuna haja ya kuzunguka na vyeti katika ofisi mbalimbali wakitafuta ajira badala yake wachangamkie fursa hiyo ya kufuata wakulima vijijini.

Haina mjadala kuna vijana wengi wanapohitimu shule na vyuo, mawazo yao ni kuhamia mijini kutafuta ajira. Hilo linaweza kuwa sawa, lakini kuna haja ya kujiongeza zaidi kwa kubadili mwelekeo.

Ndiyo maana serikali imekuwa ikiwahimiza wahitimu kuchangamkia fursa mbalimbali, badala ya kubweteka wakisubiri ajira, kwa sababu wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa njia nyingine tofauti na taaluma yao.

Hivyo, hao waliohitimu kutoka vyuo vya kilimo, rai yangu kwao wasiendelee kusubiri ajira kwa kukwepa kwenda vijijini. Waangalie fursa, ikiwamo ya kukodishwa kwa ajili ya utalaamu wao, kwenda kufunza mbinu bora za kilimo.

Inawezekana wasipate malipo makubwa, lakini bado kuna unafuu kuliko kukaa kusubiri ajira, wakati kuna tosha za kuwawezesha kupiga hatua moja ya kusonga mbele, katika harakati za kujiletea maendeleo.

Naibu Waziri huyo, ametaja kuwapo jumla ya vijana milioni 16.1 nchini, sawa na asilimia 35 ya idadi ya watu wote. Utafiti wa Nguvu Kazi ya Taifa wa mwaka 2014, ulioonyesha asilimia 67.1 ndio nguvukazi yote ya Taifa na kiwango cha ukosefu ajira ulioko sasa ni asilimia 11.7.

Hali inapokuwa hivyo, vijana hawana budi kubadilisha mwelekeo kwa kuchangamkia fursa zinazowawezesha kuendesha maisha yao, ikiwamo kuungana na kukopa fedha katika benki na wakajitosa katika biashara.

Takwimu hizo zinaonyesha umuhimu wa nguvukazi ya vijana na sekta ya kilimo kwa maendeleo ya nchi, ambayo kimsingi, kilimo bado ni uti wa mgongo wa taifa.

Naibu Waziri Mgumba kwenye wito wake ndani ya kongamano la vijana wakulima mkoani Arusha, anasema vijana wote waliohitimu vyou mbalimbali na kukaa kusubiri ajira bila kuangalia njia nyingine ya kujiajiri, ni hatari kwao.

Wametakiwa waanze kufikiria kujiajiri kwa kuishi na kutumia fursa ya mkopo wa asilimia nne unaotolewa katika halmashauri kwa vijana, ili wawe chachu ya mabadiliko katika jamii kupatikana ajira.

Kufikiria kujiajiri kunaweza kuongeza ajira kwa vijana wengine, kwani kuna uwezekano mkubwa wa kupata mkopo na kuanzisha biashara, ambayo wakati mwingine inamlazimu mkopaji aajiri wafanyakazi.

Baadhi yao wamekuwa wakilalamika kwamba, taasisi za fedha zimekuwa zikiwanyima mikopo, Niseme tu, ni vyema wakawekewa mazingira rafiki yanayowawezesha kuipata bila usumbufu.

Ni hatua itakayokuwa msaada mkubwa kwao, wakiachana na mazoea ya kusubiri kuajiriwa na badala yake watajiajiri kwani ninaamini wapo ambao wangependa kuona wanaendesha biashara zao na kuitwa ‘mabosi.’