Habari njema Tehama isiishie shule za mijini

07Jul 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Habari njema Tehama isiishie shule za mijini

ILI kuwawezesha wanafunzi kufahamu matumizi ya taarifa mbalimbali, kumudu vyombo vya mawasiliano na kujifunza kupitia maktaba, serikali ilianzisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) shuleni.

Kozi hiyo ilianza kufundishwa mwaka 2005 katika mtalaa mpya wa Elimu ya Msingi.

Hii inatokana na ukweli kwamba katika dunia ya sasa ya utandawazi, matumizi ya Tehama hususani kompyuta yamechangia kuendeleza na kusambaza matumizi ya sayansi na teknolojia.

Kwa hapa Tanzania, Kiswahili kinatumika kama lugha rasmi ya kufundishia somo hilo, shule za msingi kama nyenzo ya kuwasilisha elimu ya sayansi na teknolojia ya kisasa kwa wanafunzi.

Pamoja na juhudi hizo za kuanzisha kwa somo hilo, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine, zinazoweza kukwamisha ufundishaji na ujifunzaji wa Tehama.

Baadhi ya changamoto hizo ambazo zimewahi kutajwa na wizara husika ni uhaba wa walimu, ukosefu wa umeme hususani maeneo ya vijijini na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Kwa upande wa serikali, inajitahidi kutatua changamoto ya nishati kwa kupeleka umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili kuhakikisha somo hilo linafundishwa katika ngazi zote linapohitajika.

Lengo la kufanya hivyo, ni kuwaandaa walimu watakaofundisha somo hilo shuleni, huku ikishirikiana na kampuni ya Microsoft kwa ajili ya kupata vifaa hasa kompyuta.

Huo ni mpango wa muda mrefu wa serikali wa kuimarisha matumizi ya somo hilo katika ufundishaji shuleni, lakini kwa sasa linafundishwa kwa baadhi ya shule na hasa za mijini ambazo zina mazingira rafiki ikiwamo umeme.

Kwa sehemu hizo ni wazi kwamba kuna umuhimu wa kuwaandaa walimu na pia kuhakikisha shule zote zinakuwa na umeme ili iwe rahisi kwa walimu kufundisha na pia iwe rahisi kwa wanafunzi kuelewa.

Ukisoma kitabu cha Tehama darasa la saba, kuna mada kama vile mtandao wa ndani wa kompyuta, mtandao wa intaneti, kutumia tovuti, maana ya baruapepe, hayo yote walimu na wanafunzi wanatakiwa kuyaelewa.

Sidhani kwamba walimu na wanafunzi wa shule za vijijini wanaweza kuyaelewa, hivyo kuna haja ya kuhakikisha shule zote zinakuwa na walimu wanaojua matumizi ya Tehama ili iwe rahisi kufundisha somo hilo.

Walimu itawawia rahisi kufundisha iwapo pia shule zitakuwa na umeme kwa ajili ya kompyuta, hivyo ni vyema kasi ya kusambaza umeme ya REA ikaongezwa ili shule zote ziwe na nishati ya umeme.

Shule za vijijini zisionekane kama zinabaguliwa kwenye somo la Tehama, kwa sababu ya kukosa nishati ya umeme, kwani huko nako kuna wataalam wa baadaye ambao wanahitaji kusoma somo hilo.

Hayo yakifanyika, wanafunzi wa shule za vijijini hawatakuwa nyuma kwenye somo hilo, hivyo umeme usambae kote, wizara husika iandae mafunzo ya muda mfupi kwa walimu wa vijijini ambao watafundisha Tehema.

Kama umeme unaweza kuchukua muda mrefu, basi uangaliwe uwezekano wa kuhakikisha shule zote zinakuwa na umeme jua ili kurahisisha ufundishaji wa somo hilo.

Siyo vibaya kushirikisha wadau wote wa elimu kwa ajili ya kufanikisha somo hilo kwa shule zote nchini, kwani wanaweza kusaidia upatikanaji wa kompyuta mpakato, sola na huduma nyingine muhimu.

Wakati hilo likifanyika, wizara nayo iwajengee walimu uwezo katika somo hilo, kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya mawasiliano duniani, ambayo kimsingi huathiri nyanja mbalimbali za maisha.

Hayo yakifanyika, kutakuwa na mazingira rafiki ya ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo nchini, bila kujali kwamba ni za vijijini au mijini, kwani kila moja itakuwa na mahitaji yote muhimu.

Pamoja na hayo, ninaamini kwamba kuna manufaa mengi katika ufundishaji wa somo hilo kwa lugha ya Kiswahili, kwani kunasaidia kujenga saikolojia ya kujiamini na kujithamini miongoni mwa wanafunzi.

Vilevile kutumia lugha hiyo ni hatua muhimu ya kukabiliana na mahitaji mapya katika medani za sayansi na teknolojia, tofauti na sura yake ya kuwa lugha ya kwenye majukwaa ya kisiasa, nyumbani na maeneo mengine.