Haki itawale chaguzi za marudio Ilala, Kinondoni

07Feb 2016
Salome Kitomari
Nipashe Jumapili
NAWAZA KWA SAUTI
Haki itawale chaguzi za marudio Ilala, Kinondoni

SARAKASI zinaendelea kwenye uchaguzi wa Meya wa Manispaa za Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam, huku kinachoangaliwa kikiwa siyo haki ya chama chenye madiwani wengi kuongoza, bali nguvu ya kisiasa.

Kila palipo na madiwani wengi wa vyama vya upinzani uchaguzi wa Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri umeingia dosari kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutumia nguvu na wakati mwingine kutumia vyombo vya dola na watendaji wa serikali ili kiongoze hata kama hesabu hazikubali. Kinachoonekana ni rafu ya kulazimisha kuongoza Halmashauri kwa nguvu, huku haki ikiwa kwa upinzani wenye wabunge na madiwani wengi katika eneo husika. Kabla ya kutangazwa kwa marudio ya uchaguzi katika Halmashauri hizo tatu kutokana na mgawanyo mpya wa wilaya, uchaguzi wa Ilala na Kinondoni uliingia dosari kwa wabunge wa viti maalumu wa CCM kutoka Zanzibar kuingia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kama wapiga kura halali. Waliposhtukiwa na wabunge wa mwamvuli wa upinzani wa Ukawa, kukatokea mvurugano na uchaguzi kushindwa kufanyika. Cha kujiuliza ni kwanini wabunge wa Zanzibar waje kupiga kura katika Manispaa ya Kinondoni au Ilala? Kwanini hawakwenda Temeke ambako madiwani wengi ni wa CCM? Wakurugenzi wa Manispaa hizo waliahairisha uchaguzi na kuutangaza upya, lakini sarakasi ziliendelea ikiwamo matumizi ya fedha na mwishowe Ukawa walipenya na kuongoza Ilala na Kinondoni kwa kuwa na wingi wa madiwani. Wiki iliyopita, Waziri wa Tamisemi ametangaza marudio ya uchaguzi huo baada ya kutangazwa wilaya mpya za Ubungo ambayo itamegwa kutoka Kinondoni na Kigamboni mbayo itamegwa kutoka Temeke ili kupata eneo jipya la utawala. Cha kujiuliza sheria inafanya kazi kwa kurudi nyuma au kunzia pale ilipoanzia na kuendelea? Kwanini sheria inafukua makaburi? Si mara ya kwanza kwa serikali kugawa maeneo ya utawala, na kila eneo kulipoundwa wilaya mpya iliendelea kuwa chini ya wilaya mama hadi uchaguzi mkuu mwingine na kupata madiwani. Iweje kwa Temeke na Kinondoni? Kulikuwa na haja gani kwa serikali ya awamu ya nne kutangaza mgawanyo huo kipindi cha mwisho na kuacha kufanya hivyo mapema ili uchaguzi utakapofanyika ibaki kuweka watendaji na majengo katika maeneo hayo? Awali uchaguzi wa Meya wa Jiji ulipanga kufanyika Januari 23, lakini ulihairishwa na tarehe mpya ikatangazwa kuwa ni leo. Lakini ukiangalia kiini cha mvutano na ucheleweshwaji unaofanyika katika hili ni CCM kutokubali ukweli wa mambo; kuwa tayari kuachia vyama vingine viongoze. Kila Halmashauri yenye wajumbe wengi wa Ukawa kuna sarakasi za kutaka kuwanyima haki yao. Mathalani uchaguzi wa Halmashauri ya Kilombero uliingia dosari baada ya Mbunge wa jimbo husika kuelezwa kuwa siyo mpiga kura halali, na nguvu kubwa ya askari zaidi ya saba kutumika kupambana na mbunge huyo. Halmashauri ya Tanga kulikuwa na figisufigisu kiasi cha kujiuliza yote haya yanatokea kwanini? Shida ni upinzani kuongoza? Kama chama kimoja kinataka kuendelea kutawala milele, kuna haja gani ya kuwa na uchaguzi na kujificha chini ya kivuli cha demokrasia? Sarakasi zinazojitokeza sasa hata ambaye siyo mjuzi wa siasa atakwambia CCM inalazimisha kuongoza katika eneo ambalo ukweli wa mambo kura zake hazikutosha. Ni vigumu kukubali matokeo hasa yanapokuwa kinyume na matarajio ya muhusika, lakini kwa kuwa taifa lipo kwenye mfumo wa vyama vingi ni lazima chama kimoja kifahamu kuwa kinaweza kushindwa na kingine. Kuendelea kung’angania uongozi ni kuonyesha udhaifu, kujishushia heshima na kudharaulika mbele ya wapiga kura. Mwenye haki yake apewe ushindi wake, sarakasi ziwekwe kando na kutoruhusu virugu na kurushiana maneno makali kwnai ni kujiabisha mbele ya umma kwa kuwa utawala wa sheria, demokrasia unashindwa kuheshimiwa na wenye jukumu la kusimamia. Hatutarajii uchaguzi wa marudio kutawaliwa na fujo, vituko na mengine mabaya ambayo hayastahili. Baada ya uchaguzi wa majimbo na kata za Jiji kumalizika Oktoba 25 mwaka jana, utangazaji wa matokeo ulichukua muda mrefu kiasi cha kujiuliza maswali mengi, ikiwemo kwa nini majimbo ya vijijini ambako miundombinu ni mibovu matokeo yaliwahi kutangazwa wakati ya Manispaa hizo yakichukua siku tatu hadi nne? Wananchi waliandamana na kukesha kwenye kituo cha kuhesabia kura kwa hofu ya uchakachuaji, hali hiyo hiyo inajirudia kwa sura ya kuwa na vurugu, matumizi ya serikali na vyombo vyake kuharibu uchaguzi wa Jiji na Manispaa hizo kwa kulazimisha ushindi kwa CCM. Mungu ibariki Tanzania. [email protected]