Haki ya dhamana maana yake ni nini?

08Jun 2019
John Juma
Nipashe
Mionzi ya Sheria
Haki ya dhamana maana yake ni nini?

NI kawaida kusikia mtu anakwenda katika kituo cha polisi , akiwa na mahitaji muhimu ya kisheria kumuwekea dhamana mtu wake wa karibu.

Ni mustakabali unaosababisha mtu kudodosa haja ya tafsiri neno dhamana na nafasi yake kisheria. Hapo ndipo inapofungua mlango katika kutolewa ufafanuzi wake, ndani ya mustakabali wake kisheria.

Inaelezwa kisheria, dhamana ni ruhusa ya uhuru anaoweza kupewa mtuhumiwa wakati ama uchunguzi wa kosa lake unaendelea au shauri lake likiendelea kusikilizwa mahakamani au akisubiri uamuzi wa rufani yake.

Hiyo ni haki inayopatikana kuptia msingi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo ina dhana inayotamka kwamba mtu hatochukuliwa kuwa mwenye hatia mpaka tuhuma zithibitishwe dhidi yake, kupitia Ibara ya13 (6) (b).

Ili kuzingatia dhana hiyo, ni muhimu kumruhusu mtuhumiwa kwa kumpa dhamana apate kuwa nje ya kizuizi mpaka hapo tuhuma zake zitakapothibitishwa na mahakama. Kwa mantiki hiyo, dhamana ni haki ya mtuhumiwa na wala sio upendeleo au zawadi.

Dhamana huweza kutolewa na jaji au hakimu, hali kadhalika, Mkuu wa Kituo cha Polisi ambako mtuhumiwa ameshikiliwa.

Hata hivyo, yapo baadhi ya makosa ambayo kisheria hayaruhusu dhamana, nayo ni: Mauaji ya kukusudia; uhaini; unyang’anyi wa kutumia silaha; ugaidi; sanjari na kosa la kunajisi; Kifungo cha 148(5) (a)  (e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, 1985.

Hali kadhalika, mtuhumiwa anaweza kukosa dhamana kutokana na mazingira yafuatayo. Endapo:

Mtuhumiwa alishapewa dhamana akaikiuka; Kwa minajili ya usalama wa mtuhumiwa mwenyewe; usalama wa jamii; Kwa kuchelea kumwachia nafasi ya kuvuruga/kuharibu upelelezi; na sababu nyingine, yoyote ya msingi, kama atakavyoona Mkuu wa kituo.

Dhamana zipo za aina tofauti, na zenyewe ni kama vile: Dhamana ya mkataba wa Maandishi. Huo ni mkataba kati ya mtuhumiwa au mdhamini kujifunga kwamba mtuhumiwa atahudhuria Baraza la mahakama siku iliyotajwa. Iwapo mtuhumiwa asipotokea pasipo sababu muhimu, atalazimika kutekeleza masharti fulani au hata kifungo.

Dhamana ya Mali: Iwapo mtu hana kiasi cha fedha, anaweza kuweka dhamana kwa kukabidhi mali zake zinazohamishika.

Dhamana ya kutambuliwa: Aina hii ya dhamana humtaka mtuhumiwa au mdhamini kuweka sahihi ikiwa masharti ya mkataba wa dhamana yamevunjwa.  Aina hii huonekana kama yenye unafuu kidogo.

Dhamana ya kuweka fedha: Hii ni aina ya dhamana ambapo, mtuhumiwa, rafiki au ndugu hutakiwa kutoa kiwango fulani cha fedha na iwapo hatahudhuria mahakamani fedha hiyo hutaifishwa na serikali.

Anayeweza kuomba dhamana? Mshitakiwa au rafiki wa mshitakiwa na wakili wa mshtakiwa.

Muda wowote wakati kesi inaendelea na wakati rufaa ikisubiriwa; Wakati mashitaka yanaandaliwa na polisi au kabla ya hukumu kutolewa au rufaa kuamuliwa.

Kifungu cha 67 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mwaka 1985 kinaeleza kwamba, mtuhumiwa aliye chini ya ulinzi wa polisi anaweza kukataliwa maombi yake ya kutaka apewe dhamana.

 Hii ni kwa kuzingatia masuala kama vile, polisi kujiridhisha kwamba mtuhumiwa atatimiza masharti ya dhamana atakayopewa, ikiwa kufika siku na saa atakayoamriwa.

Zaidi, kujua makazi, ndugu na jamaa, ajira na hata ikibidi hali ya maisha ya mtuhumiwa na familia yake, kumbukumbu za kihalifu kama zipo.

Baada ya mtuhumiwa kupewa dhamana ya polisi na kuwa huru dhamana hiyo inaweza kufutwa na mkuu wa kituo, chini ya Kifungu cha 68 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mwaka 1985. Baadhi ya sababu zinazoweza kusababisha uamuzi wakufuta dhamana ni: Kubainika kwamba mtuhumiwa anapanga mipango kutoroka au makusudi anakiuka au yuko karibu kukiuka masharti ya dhamana

Adhabu kwa Kukiuka Masharti ya Dhamana; dhamana inayotolewa na polisi kwa mtuhumiwa anayekabiliwa na kosa la jinai inapaswa kuheshimiwa. Kifungu cha 69 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Mwaka 1985 kinaelekeza adhabu kali kwa mtuhumiwa na mdhamini au wadhamini wanapokiuka masharti ya dhamana waliopewa.

Dhamana inatolewa bure, hakuna malipo yoyote yanayotakiwa kutolewa ili mtuhumiwa au mshtakiwa akubaliwe dhamana.

Jambo la msingi ni mtuhumiwa kuomba apewe dhamana na kutimiza taratibu kwa mujibu wa sheria.

Ni muhimu  mtuhumiwa kuwa nje kwa dhamana, ili aweze kujiandaa kukabiliana na tuhuma zinazomkabili kabla ya hajafikishwa mahakamani, mfano kupata msaada wa kisheria

Mwisho kabisa, dhamana ni haki ya kikatiba ya kila mtuhumiwa, kwa hiyo mtuhumiwa ana haki ya kuomba dhamana wakati wowote kabla hajapatikana na hatia au baada ya kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yake. Pia dhamana ya polisi haihusishi fedha taslimu, hutolewa bure. Ni kosa kwa askari polisi kupokea fedha/rushwa katika zoezi la utoaji wa dhamana na katika utendaji kazi wake.