Hakika CCM kama nyani mzee!

08Nov 2020
Joseph Kulangwa
Nipashe Jumapili
FIKRA MBADALA
Hakika CCM kama nyani mzee!

SIKU hizi vijana au watoto hawana fursa ya kusomewa vitabu vya hadithi au hata kusimuliwa hadithi na wazee wao. Kusimuliwa na mababu na mabibi zao, wakiwa wanaota moto usiku wakisubiri chajio.

Badala yake wanakalia zaidi kusikiliza muziki wa kizazi kipya, wanakalia kuangalia bongomuvi, wanashindana mavazi na kurushana kwenye mitandao ya kijamii, bila kujua kuwapo kwa historia ya jamii zao.

Wangezingatia simulizi mbalimbali wanazopewa na hata kusoma vitabu kama vya Adili na Nduguze, Mashimo ya Mfalme Suleiman, Kisiwa cha Giningi, Rosa Mistika, Pepo ya Mabwege, na vingine vya aina hiyo, wangeshajifunza mengi wala wasingepata tabu, hasa katika nidhamu.

Wangesoma Mashimo ya Mfalme Suleiman, wangekumbana na usemi wa kujitambulisha wa Umsolopagaaz, wa kabila la Wazulu na damu ya Chaka, Mkuu wa Majeshi ya Nkomabakos, akiapa kutumia pigo moja lililonyooka la shoka na kumaliza mambo.

Kwa Umsolopagaaz kazi ilikuwa ni moja tu, ya kupiga na kusambaratisha maadui. Hicho ndicho nilichokiona katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani na hata uwakilishi mwaka huu katika Tanzania.

Pigo moja lililonyooka la shoka, hakika limesambaratisha upinzani nchini. Mpaka sasa ngumu kuamini kilichotokea, kwamba CCM imeweza kusambaratisha wapinzani kiasi hiki cha kutishia Bunge kurejea kuwa la chama kimoja!

Ukiuliza walioko upande wa washindi, watakwambia kirahisi sana, kwamba ni sera nzuri na yaliyofanywa na awamu hii ya tano katika muhula wake wa kwanza. Lakini wale wa upande wa pili nao haraka tu, watakwambia wameibiwa.

Mimi ambaye niko katikati, nitasema tu kwamba uchaguzi umemalizika, aliyeshinda kashinda na aliyeshindwa kashindwa. Nitakwambia tu kwamba kila ushindani na mbinu na ujanja wake, ukizubaa umeliwa.

Hata kwenye soka, tunajua, mbona Wabongo tunapenda sana soka, na ndiyo sababu tumegawanyika katika usimba na uyanga, na tunajua kuna magoli ya mkono. Ukizubaa limo.

Sijajua kama wapinzani walizubaa likawamo, au kama washindi ambao ni watawala kweli walilitumbukiza kwa mkono bila msimamizi, yaani mwamuzi, Waitu Kaijage na wenzake, wakashindwa kuona au wakaona wakauma filimbi!

Kwenye soka, tunajua ngoma ikimalizika wachezaji hukumbatiana na kuyaacha hapo, hata Malkia Sendiga alisema kwenye ngumi nako ni hivyo hivyo, mnatwangana mnatoana ngeu, lakini mwisho wa siku mnakumbatiana na maisha yanaendelea.

Kina Tundu wanaona ukakasi kabisa kukumbatiana na kina Pombe, pengine wanadhani wenzao waliweka mawe kwenye glovu, au walifunga magoli kwa mkono. Sasa sijui kamati ya saa 72 inaweza kufanya nini katika hilo!

Tatizo watu wanasahau kuwa hili lisisiemu ni nyani zee lililokwepa mishale, mikuki, magobori, mapanga na hata mawe lukuki, hivyo linajua mbinu zote za ushindi, sasa ukiingia kichwakichwa hujui mishale ya sumu na isiyo na sumu ni ipi, itakuua tu.

Hebu tazama sasa, Pombe katupa makonde kadhaa 12 yametua usoni mwa Tundu, huku Tundu akirusha ya kwake na ni moja tu lililotua, nani atashinda? Lazima Pombe amleweshe Tundu tu atake asitake.

Sasa watazamaji nao wana yao, wanajiuliza, hivi hii tofauti ya kura milioni 12 na milioni moja, si maajabu haya? Wanakumbuka 2015 ambako angalau tofauti ilikuwa ya milioni nane kwa milioni sita! Tena safari hiyo Edo hakuwa msemaji sana kama alivyokuwa Tundu kwenye kampeni za mwaka huu.

Kama ni nyomi mwaka huu, kila upande ulikuwa na nyomi yake, tena mmoja ukihanikiza wasanii wote uwajuao wa nji hii, huku mwingine ukichechemea, lakini bado nyomi zilikaribiana na kujiaminisha kuwa safari hii chuma kikoli moto.

Lakini wapi bwana, Mzee wa Chato akachukua 12 kati ya 14 na zilizobaki mbili akawaambia haya gawaneni huko, ili mbaki na ushahidi kuwa nanyi mlishiriki na kwamba kuna watu walikupigieni! Aisee, zereu duh! Wabongo tujiulize na tujifunze kwa kilichotokea uchaguzi huu huru na wa haki! Alamsiki!