Hakika Rais Samia yu ‘Mchungaji Mwema’ kwa vitendo, jamani tumfuate

29Jul 2021
Mashaka Mgeta
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hakika Rais Samia yu ‘Mchungaji Mwema’ kwa vitendo, jamani tumfuate

ALIPOKUWA anazindua Mpango wa Chanjo ya Uviko 19 kwa Watanzania jana, Rais Samia Suluhu, amezungumzia mambo kadhaa yanayouaminisha umma kuhusu usalama uliopo kwenye chanjo hiyo.

Kauli ya Rais Samia, imekuja kutokana na kauli za baadhi ya watu, wanaoonyesha wasiwasi juu ya usalama wa chanjo hiyo, pengine kutokana na ama ukosefu au upungufu wa taarifa sahihi, walizo nazo hasa zinazotokana na kuenezwa kupitia mitandao ya kijamii.

Ni uzinduzi uliofanyika Ikulu ya Magogoni, jijini Dar es Salaam, Rais Samia akiweka wazi kwamba ana majukumu makuu yanayomkabili akiwa mama wa familia, mke, mlezi wa wajukuu.

Pia kiserikali ana wasifu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa na dhamana ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Anajitambulisha kuwa na watoto na wajukuu anaowapenda sana, kama vile nao wanavyompenda na kumtegemea katika maisha yao. Ameyasema hayo huku ‘lugha ya picha’ ikionyesha jinsi Rais Samia anamaanisha kuhusu jambo hilo.

Upande mwingine, Rais Samia akasema anayatambua majukumu yake katika ngazi hizo, ikiwamo ya urais ambayo inamfanya kuwa mfano wa mchungaji anayewaongoza Watanzania, hivyo hawezi kuruhusu jambo lisilokuwa na tija liwafikie Watanzania.

Hotuba fupi ya Rais Samia kuhusu chanjo hiyo, imebeba ujumbe mzito unaopaswa kuwatoa hofu wananchi, badala yake wanapaswa kuunga mkono ili Tanzania iwe sehemu ya dunia inayolenga kudhibiti kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Rais Samia akijitaja kuwa ‘Mchungaji’ wa Watanzania, nami ninawiwa kumtaja kuwa ‘Mchungaji Mwema’. Kwanini? Niseme, anatimiza vyema wajibu wake katika kutambua ‘kiu’ ya watu anaowachunga, kisha akawaonea huruma wasiendelee kuteseka katika kadhia inayowakabili. Hapa inamaanisha madhara ya Uviko 19.

Ni wazi kwamba, Watanzania wengi wameguswa kwa namna tofauti kutokana na athari za Uviko 19. Lakini, kwa walioguswa moja kwa moja, wanatambua umuhimu wa kulidhibiti janga hilo. Udhibiti wa Uviko 19 ni miongoni mwa ‘kiu’ ya Watanzania ambayo Rais Samia aliye ‘Mchungaji Mwema’ ameitambua.

Utambuzi huo ndio unamsukuma Rais Samia, kuwaonea huruma Watanzania kwa kadhia zinazotokana na athari za Uviko 19, na hivyo kuruhusu matumizi ya chanjo hiyo, huku akiongoza uzinduzi wake uliofanyika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam jana.

Hiyo inachukua nafasi kuidhihirishia dunia kwamba, chanjo hiyo haina madhara pasipo shaka yoyote. Rais Samia kachanjwa hadharani, huku akiungwa mkono na watu mashuhuri, wakiwamo viongozi wakuu wa dini, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi waandamizi, wa kiserikali hadi ngazi ya wilaya, wasanii na engine wenye mapenzi mema.

Kwa namna yoyote ile, Watanzania wanapaswa kuondokana na taarifa potofu, badala yake wazipate na kuzitumia taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya uamuzi sahihi kwa maisha yao.

Taarifa sahihi ni zinazotoka kwenye vyanzo sahihi, kama zilivyotolewa kwenye hotuba ya Rais Samia kuhusu ukweli wa chanjo yenye kudhibiti maambukizi ya Uviko 19.

Kwa mukhtadha huo, Rais Samia ametimiza wajibu wake akiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu; ametimiza wajibu wake akiwa mama wa familia;. ametimiza wajibu wake akiwa mlezi wa wajukuu; ametimiza wajibu wake akiwa mke; na ametimiza wajibu wake kama Mchungaji aliyeshika fimbo mkononi, akiwaongoza Watanzania.

Ni hiari kwa kila Mtanzania kutumia akili na utashi kufanya uamuzi sahihi katika kushiriki mpango wa kupata chanjo ya Uviko 19, na kwa namna iwayo yote, uamuzi sahihi ni kushiriki chanjo hiyo pasipo hofu ama hisia hasi.

Wakati hamasa ikiwa katika kushiriki chanjo hiyo, Watanzania wanapaswa kuendelea kuchukua hatua zote zinazoshauriwa na watalaamu katia kudhibiti maambukizi ya Uviko 19, ikiwamo kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka, kutumia vitakasa mikono na kadhalika. Kwa pamoja tutashinda dhidi ya Uviko 19!

Mwandishi ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga na anapatikana kwa simu: 0754691540 au barua pepe: [email protected].