Hakuna kapa isiyokuwa na usubi

11May 2019
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hakuna kapa isiyokuwa na usubi

‘USUBI’ ni wadudu wadogo wanaofanana na mbu. ‘Kapa’ ni sehemu ya pwani inayoota mikoko na ambayo huwa na tope na haikosi usubi. Maana yake hakuna msitu wa mikoko usiokuwa na usubi.

Methali hii yatufunza kuwa hakuna kitu kisichokuwa na kasoro au hitilafu zake. Kila kitu kina faida na hasara zake.

Tangu viongozi waliokuwa madarakani katika utawala uliopita kutangaza kujiuzulu, wanachama na mashabiki wa Yanga walionekana wameshindwa kukubaliana na uamuzi huo. Jambo hilo lilisababisha klabu ya Yanga ishindwe kujiendesha yenyewe hata kuitwa ‘ombaomba’ (hali duni inayohitaji msaada kutoka kwa wengine).

Watani zetu (Simba) wakawa wanatutania kwa kutuita ‘Yanga bakuli’ yaani tunaopita na bakuli mitaani na viwanjani kuomba msaada. Hata Yanga ilipokuwa inapambana na timu zingine, wapiga picha za runinga hawakukosa kuonesha picha za watu waliokuwa wakichangisha fedha kwa ajili ya Yanga.

Ilikuwa fedheha ya aina yake kwa klabu kongwe kuomba msaada viwanjani. Ni jambo lililokera wengi, lakini hatukuwa na jinsi ila kukubaliana na hali halisi.

Hata hivyo wahenga walisema: “Hakuna kubwa lisilo ukomo.” Maana yake kila jambo lina mwisho wake kwani hata maisha ya binadamu hufikia kikomo chake.

Jumapili iliyopita, wanachama wa Yanga walifanya uchaguzi na kumchagua Dk. Mshindo Msolla kuwa Mwenyekiti kwa kupata kura 1,276 huku mgombea mwenzake wa nafasi hiyo, Dk. Jonas Tiboroha akiambulia kura 60 tu.

Aliyeshinda nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Fredrick Mwakalebela aliyewashinda wagombea wengine watano kwa kupata kura 1,206. Mwakalebela alipata kuwa Katibu Mkuu wa TFF zamani. Walioshinda nafasi za ujumbe ni: Frank Kamugisha, Arafat Haji, Salum Rupia, Bahati Mwaseba, Saad Kimji, Rodgers Gumbo, Ahmad Islam na Dominic Kata.

Viongozi hawa wameitwaa Yanga ikiwa na matatizo mengi yanayohitaji hekima, maarifa na juhudi kubwa kuirejesha pale ilipokuwa zamani. Kama kuna kiongozi aliyechaguliwa kwa lengo la kujinufaisha badala ya kuinufaisha Yanga, ni vema ajiondoe mapema na kuwaachia wenye uchungu na Yanga, wenye lengo la kuitoa kwenye umasikini uliokithiri.

Viongozi wapya wanapaswa kuzingatia mambo makubwa manne.  Wahakikishe wanapata hatimiliki (waraka wa kisheria unaompa mhusika haki ya kumiliki ardhi au mali nyingine) iliyo mikononi mwa mtu asiyetaka kuipa klabu. Kama atakataa kuitoa kwa viongozi, ashitakiwe mahakamani ili haki itendeke ili hatimiliki irejeshwe klabuni.

Hatimiliki hiyo itumiwe na viongozi kawa dhamana ya kupata mkopo wa Benki itakayokubali kujenga ile nyumba iliyokuwa makao makuu ya Yanga zamani kwenye makutano ya mitaa ya Mafia/Nyamwezi jijini Dar es Salaam. Jengo hilo laweza kuwa la ghorofa 10 au zaidi, maalum kwa biashara kama hoteli na maduka, likiwemo duka la klabu litakalouza jezi, skafu, vikombe vya chai, glasi na vifaa mbalimbali vya michezo vyenye nembo ya Yanga.

Pili lile ghorofa linalotumika sasa kule Jangwani, lifanyiwe ukarabati mkubwa ili liwe maalum kwa ofisi za viongozi wa klabu na pia malazi ya wachezaji wanapokuwa kambini badala ya kukodi hoteli za watu binafsi kama ilivyozoeleka.

Tatu, viongozi wapya wafute kabisa mpango wa ujenzi wa uwanja wa mpira pale Jangwani kwani ni eneo linalofurika maji wakati wa mvua za masika na vuli. Ni eneo ambalo chini yake kuna bomba kubwa la maji yanayokwenda kwenye Hospitali Kuu ya Rufani Muhimbili. Kwa ufupi wakubaliane na maelezo ya Serikali kuwa eneo lile halifai kujengwa uwanja wa mpira.   

Jambo la nne: Viongozi wapya wawaondoe ‘makomandoo’ kwani ndiwo wanaotumiwa na viongozi ‘wachumia tumbo’ wanaojitafutia shibe kwa kuinyonya Yanga. ‘Makomandoo’ hujifanya ndiwo wanaoijua Yanga na kuipenda sana kumbe ndiko wanakoshibia!

Viongozi wapya wasikubali kupokea taarifa za maneno kutoka kwa watangulizi wao bali kila kitu kifanyike kwa maandishi. Ikiwezekana, vitabu vya hesabu vipelekwe kwa wakaguzi ili vikaguliwe kujua fedha zilizoingia, na kazi zilizofanyia. Endapo kutakuwa na shaka, wahusika washitakiwe ili sheria ifuate mkondo wake.

Dk. Msolla na wenzake wafanye juhudi kuifanya Yanga iwe kampuni na kuwa klabu yenye hisa kwani “Hakuna kubwa lisiloshindwa.” Maana yake hakuna jambo lisilowezekana. Hutumiwa kumhimiza mtu anayekabiliana na hali ngumu kuwa lazima atafanikiwa hatimaye.

[email protected]

0784  334 096