Hakuna 'mchawi' Simba, Yanga kufungwa Ligi Kuu

13May 2019
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hakuna 'mchawi' Simba, Yanga kufungwa Ligi Kuu

SOKA la Bongo kwa miaka ya sasa timu za Simba na Yanga zikifungwa ni kama 'msiba wa mswahili' ambao haukosi sababu.

Watoto wa mjini wanasema kuwa uswahilini mtu akifa, basi itatafutwa sababu ambayo si ya kitaalamu ambayo itaeleza sababu ya kifo cha marehemu.

'Aligombana na bibi kizee mmoja jirani.', mwingine atasema 'Alitembea na mume au mke wa mtu.', wapo watakaosema 'Alipandishwa cheo kazini wenzake wakamuonea kijicho.', vile vile kuna wengine watasema 'Alioa au kuolewa na mtu mwingine, kwa hiyo yule aliyeahidiwa na kuachwa ndiye aliyesababisha.'

Nikiandika hapa sababu naweza kufikisha hata 500 na zisiishe. Soka la Tanzania nalo linafanana na hayo, hasa kwa mashabiki wake ambao wengi wao wanazipenda sana Simba na Yanga.

Mashabiki wengi wa timu hizi hasa wa kizazi cha sasa, hawaamini kama timu zao zinaweza kufungwa na timu nyingine za Bongo kwa kawaida tu kuzidiwa kimbinu kwa siku hiyo na makocha wa timu zingine.

Ndiyo maana zinapofungwa hawakosi sababu. Inakuwa ni balaa moja kwa moja, lawama kwa wachezaji wao, lawama kwa kocha wao, lawama kwa waamuzi, ilimradi tu tafrani.

Ijumaa iliyopita Simba ilichapwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, huku watani zao wa jadi Yanga wakidungwa bao 1-0 dhidi ya Biashara ya Mara. Kwenye mitandao ya kijamii na mitaani imekuwa balaa.

Wenye kuwatupia lawama wachezaji wao wapo, makocha wapo, waamuzi wapo na hata ukitazama mechi ambazo Simba au Yanga zinapoteza zinakuwa na vurumai kubwa uwanjani na nje ya uwanja.

Ukisikiliza au kusoma maoni ya mashabiki wengi utagundua kuwa tuna safari ndefu sana kwenye soka.

Ni kama Simba na Yanga ndizo zina haki miliki ya kushinda na timu zingine hazina, badala yake zenyewe zipo kwa ajili ya kuzipa pointi tatu tu timu hizo.

Wakati mwingine sifa zinazotolewa kwa timu hizo haziakisi kile ambacho kinaonekana uwanjani, lakini mashabiki wanakuwa wameaminishwa kuwa timu hizo zina uwezo wa hali ya juu.

Inawezekana ni kweli, zina wachezaji wenye uwezo mkubwa kuliko zingine, lakini hilo halitoshi kufanya timu ishinde kila mechi, hasa kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Hata Barcelona, pamoja na kuwa na wachezaji bora kabisa duniani, hufungwa na hakuna maneno, sembuse Simba na Yanga?

Na hii imekuja miaka ya hivi karibuni baada ya timu nyingi za Ligi Kuu kuwa dhaifu, huku Simba na Yanga zikijipigia.

Ni tofauti na mashabiki wa miaka ya '80 ambako pamoja na Simba na Yanga kuwa na wachezaji wenye vipaji na uwezo wa hali ya juu, lakini hazikuwa na uhakika kabisa zinapoenda kucheza na Pamba ya Mwanza, Tukuyu Stars, Sigara, Nyota Nyekundu, Pilsner, Mecco, Ushirika ya Moshi, Bandari Mtwara na nyingine.

Yanga kufungwa mabao 3-0 na Pamba wala haikuwa ajabu na wala hakukuwafanya mashabiki kuhamaki na kutafuta mchawi, bali kuzidiwa tu na wapinzani wao ndicho walichokiamini wakati huo.

Simba kuchapwa na Coastal Union au Mecco lilikuwa ni suala ya kawaida tu  haikuwa ajabu kiasi watu waweke mijadala. Ni kwamba timu zinafungwa zinajindaa na mechi ijayo.

Mashabiki wa sasa wao wanachoona ni kwamba hizi timu kufungwa labda na timu za nje tu, lakini hapa nchini zikifungwa, basi kuna 'mkono wa mtu', kitu ambacho si kweli.

Hizi timu za Simba na Yanga pamoja na kuwa na mashabiki wengi kila kona nchini ni timu kama zote za Ligi Kuu, ambazo pia zina baadhi wachezaji kutoka timu hizo hizo zinazocheza nao, hivyo zinaweza kushinda, kufungwa au kutoka sare, na hazina maajabu sana kushinda zingine.

Mashabiki wa soka nchini sasa wanapaswa kuanza kujiandaa kisaikolojia, kwani huko tunakokwenda na Ligi Kuu ikipata udhamini mnono na timu zikajiandaa sawa sawa zikiwa na pesa, ushindani utazidi kuongezeka na Simba na Yanga zinaweza kuzidi kupoteza mechi nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu zaidi ya sasa.

Mashabiki wasiwe wanafiki wa kulilia soka la Bongo likue wakati wao wanachotaka timu zao za Simba na Yanga ziwe zinashinda tu. Ili soka likue kwanza inabidi Ligi Kuu iwe na ushindani na moja wapo ni hili la timu yoyote hata kama ni kubwa, kutokuwa na uhakika wa kushinda, kama vile tunavyoona kwenye Ligi Kuu ya England.