Hakuna wa kumlaumu nafasi Stars Kombe la Dunia 2022

15Nov 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hakuna wa kumlaumu nafasi Stars Kombe la Dunia 2022

ILIIBUKA tu ghafla kama kumbikumbi wanavyoibuka wakati wa mvua juu na ndivyo ilivyo timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuweza kwenda kucheza fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar.

Sijui ilitokana na nini, lakini mashabiki wengi wa Tanzania waliibuka tu na kuamini kuwa timu yao inaweza kwenda kucheza fainali hizo. Ilionekana kama rahisi vile, lakini kumbe sivyo.

Ndiyo maana kwa sasa kila mtu analaumu, kuna wanaomlaumu kocha kwa upangaji wake na wapo wanaowalaumu wachezaji, wengine wanachagua wachezaji wa kuwalaumu ili mradi kila mmoja anaona Stars haikupaswa kupoteza mechi ya Alhamisi iliyopita dhidi ya DR Congo.

Mwanzoni kabisa wakati makundi yakipangwa, Stars ikipangwa Kundi J, Watanzania wengi walikuwa kwenye uhalisia wao, kwa kuona kuwa kundi hilo ni gumu kwa Taifa Stars.

Mbali na Stars kulikuwa na Benin, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Madagascar, ugumu wake ulitokana na ukweli kwamba Benin ni nchi ambayo kisoka iko juu kwa sasa, DR Congo hakuna Mtanzania ambaye hajui hili na hata Madagascar hawakuichukulia poa kutokana na historia yake kwa ilichofanya kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Misri 2019.

Ilifanya maajabu ikafika hatua ya nusu fainali kabla ya kutwangwa mabao 3-0 dhidi ya Tunisia.

Kila mtu alijua kundi ni gumu, lakini michuano ilipoanza ndipo kama Watanzania walipoanza kuichukulia poa.

Nadhani hali ya kujiamini ilianza baada ya Stars kulazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya DR Congo.

Baada ya hapo, ikaichapa Madagascar mabao 3-2 nyumbani. Wakaibuka mashabiki wengi sasa ambao waliamini kuwa njia ya kwenda kucheza Kombe la Dunia nchini Qatar ni nyeupe. Tena kuna wengine walidhani kuwa atakayeongoza kundi ndiye anakwenda moja kwa moja.

Kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Benin, kukawanyong'onyesha kidogo, lakini ushindi wa ugenini wa bao 1-0, uliwaaminisha Watanzania kuwa safari ya Qatar ni rahisi mno.

Cha ajabu ilionekana kama safari ya kwenda kucheza Kombe la Dunia ni rahisi kuliko hata kusaka tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON). Haijawahi kuwa rahisi kiasi hicho.

Hata kama Stars ingeongoza kundi bado ingekwenda kukumbana na vigogo vingine kwenye soka la Afrika kama Misri, Cameroon, Senegal, Ghana, Tunisia, Morocco ama Nigeria.

Huko nako kusingekuwa na urahisi wowote kwenye mechi za mtoano. Ni kwamba ilipofika Stars ndipo uwezo wa wachezaji ulipoishia.

Hakukuwa na mkakati wowote uliokuwa unaonyesha kuwa Stars inataka kwenda kucheza fainali za Kombe la Dunia, badala yake mazingira ya mechi ilizokuwa inacheza ndiyo yaliyokuwa yakiwaonyesha watu kuwa inawezekana hivyo. Ina maana Watanzania walisubiri zaidi bahati kuliko uwezo halisi wa timu na mipango mikakati.

Badala ya kuwatupia lawama 'madongo' wachezaji na makocha, inabidi kuwapongeza kwa hatua waliofikia, kwani kwenye michuano hii kuna kitu wamekitengeneza.

Ilikuwa ni nadra sana kwa timu ya taifa kwenda kushinda ugenini au kulazimisha sare na timu za mataifa hata madogo kisoka, achilia mbali makubwa kama Benin na DR Congo.

Leo hii wachezaji wa Stars wanauwezo wa kupambana kwenda kushinda ugenini, ni jambo ambalo linaonekana limefanyiwa kazi na benchi la ufundi, kwani hilo ni jambo ya kiufundi na kisaikolojia zaidi.

Kilichowaangusha ni mechi ya za nyumbani. Na hata mechi iliyoshinda dhidi ya Madagascar ilipata ushindi kwa mbinde wa mabao 3-2, inaonekana kuna tatizo kwa Stars inapocheza nyumbani.

Unaweza kusema ni kutokana na presha mashabiki wao, lakini kuna mechi ambazo Stars ilicheza bila mashabiki.

Hata Watanzania waseme vipi, lakini uwezo wa wachezaji wao ndiyo ule na umeishia pale. Haiwezekani tukaona tofauti baada ya hapo.

Kama Watanzania wanacheza na timu ya taifa ambayo Fiston Mayele wanaomuimba kila kukicha, lakini kwenye kikosi chao cha taifa hana namba na haitwi, unategemea kuwa hiyo ni timu ya mchezo?

Nina uhakika kama Mayele, Jesus Moloko, Henock Inonga, Yannick Bangala, wangekuwa Watanzania, basi wangekuwapo kwenye kikosi cha Taifa Stars tena wale wanaoanza, lakini timu ya Taifa DR Congo hawapo.

Hapo pata picha ya uwezo wa wachezaji wa DR Congo na wa Kitanzania. Itoshe tu kusema Wachezaji wamepambana, lakini ubora wa timu walizocheza nazo umekuwa mkubwa zaidi kuliko wao.

Haiwezekani nchi inayokusanya wachezaji kutoka nje ya nchi ambayo haiwategemei TP Mazembe, wala AS Vita kutoa wachezaji kwenye timu ya taifa, kucheza na taifa ambalo hadi leo baadhi ya mashabiki wake wanataka wachezaji wa kigeni wapunguzwe ili Simba na Yanga viwe vitalu vya kutoa wachezaji wa timu ya taifa, badala ya kuwahamasisha kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, na kuacha kuwategemea Mbwana Samatta na Simon Msuva tu miaka nenda rudi.