Halmashauri zitenge bajeti ya kliniki tembezi za madaktari bingwa nchi

07Sep 2017
Raphael Kibiriti
Nipashe
Mjadala
Halmashauri zitenge bajeti ya kliniki tembezi za madaktari bingwa nchi

NIMEKUWA mmoja wa watu walio na mtazamo wa upande unaoikubali dhana ya maendeleo kuwa na maana pale inapohusisha maendeleo ya watu na siyo ya vitu.

Kwamba maendeleo halisi ni yale yanayojikita kwenye ustawi wa watu na siyo wingi wa vitu.

Unapokuwa kwa mfano na jiji kama la Dar es Salaam ambalo limepambwa na maghorofa marefu karibu kila eneo na mtu akaita hali hiyo kama maendeleo wakati wakazi wake wanakabiliwa na magonjwa, njaa na umasikini anakuwa anatofautiana na mimi moja kwa moja kimtazamo.

Kumbe mtazamo wangu ni kwamba hata kama jiji hili lingekosa maghorofa marefu ya kuvutia, lakini wakazi wake wakapata kwa ufanisi huduma za kijamii kama vile afya, elimu, maji, yumkini watakuwa wamepiga hatua za kimaendeleo.

Suala la mtu kuwa na afya bora ni la msingi kwa maendeleo yake na ya taifa kwa ujumla.

Si ajabu kusikia mtu akimshukuru Mungu kwa kumjalia afya bora.

Katika mantiki ya kawaida anamaanisha kuwa mtu anapokuwa na afya bora, anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kukabiliana na mazingira yanayomzunguka kujiletea maendeleo yake.

Mjadala unakubaliana na msemo huo kwa sababu bila ya afya, hakuna shughuli yoyote inayowezekana kufanikiwa.

Mtu anapokuwa mgonjwa hawezi kufanya chochote cha maendeleo zaidi ya kuwa tegemezi kwa ndugu, jamaa na marafiki na mwisho wa siku anaweza kuiingiza familia yake katika lindi la umaskini kutokana na kutumia rasilimali za familia kwa ajili ya matibabu.

Sasa sekta ya afya nchini ambayo ni moja ya nguzo za maendeleo ya taifa bado ina changamoto ya kuwafikia wananchi wote, pamoja na serikali kufanya vyema katika kushughulikia changamoto zilizopo.

Ni dhahiri serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa sekta hii imeweza kujenga zahanati na vituo vya afya nchini, na hasa baada ya kuweka dhamira ya kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata nchini.

Kwa hivi sasa utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali.

Hata hivyo, pamoja na hatua hiyo kubwa ya serikali, lakini tatizo la ukosefu wa madaktari bingwa limekuwa ni kikwazo cha kuhakikisha wananchi na hasa wa vijijini wananufaika na huduma ya watalaamu wa kada hiyo muhimu ya afya.

Bado kuna upungufu mkubwa wa madaktari bingwa nchini na ndiyo maana sasa wanapatikana walau kuanzia ngazi ya hospitali za mikoa na kuendelea, yaani katika hospitali za rufani na ya taifa.

Tatizo hili limesababisha wananchi, wengi wakiwa wa vijijini kukosa huduma za wataalamu hawa na hivyo kujikuta wakisumbuliwa na magonjwa ambayo yangeweza kupona iwapo tu wangefikiwa na huduma ya wataalamu hawa.

Changamoto ya umbali kutoka vijijini kuzifikia hospitali za mikoa, changamoto ya kiuchumi kwa maana ya nauli na gharama ya matibabu, zote hizi zimesababisha wananchi wengi wasio na uwezo kukosa huduma ya wataalamu hawa.

Ndiyo maana basi mjadala unapongeza hatua ya kuzinduliwa kwa huduma ya kliniki tembezi za madaktari bingwa ambazo zimekuwa zikiendeshwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Baadhi ya kliniki hizo ni kama zile zilizoendeshwa na Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na karibuni mkoani Rukwa.

Kwa mujibu wa takwimu, tayari kliniki hizo tembezi zimeweza kuwafikia wananchi wa vijijini zaidi ya 30,000, kiasi ambacho ni haba.

Ni kwa mtazamo huo mjadala unaona kuna umuhimu mkubwa kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikasimamia agizo lake lililotolewa kupitia kwa Naibu Waziri Dk. Hamis Kigwangalla la kuhakikisha kliniki hizi zinafanyika nchi nzima.

Zinafanyika nchi nzima, ili watu wengi wa vijijini waweze kufikiwa na huduma hii ya madaktari bingwa ambayo hawaipati kwa sasa.

Mjadala unaona basi, ili kliniki hizi za madaktari bingwa ziweze kupenya hata katika ngazi ya vituo vya afya waliko wananchi wengi, kuna umuhimu basi halmashauri zikatenga bajeti kila mwaka ya kugharimia kliniki hizi.

Hii ni kwa sababu, historia ya kliniki hizi inaonyesha kuwa rasilimali fedha imekuwa ni kikwazo cha madaktari bingwa kuwafikia wananchi wanaohitaji huduma zao hadi ngazi ya vituo vya afya, kwani safari nyingi huko nyuma zimewezeshwa na ufadhili wa wadau mbalimbali.

Hivyo ni muhimu kwa halmashauri za wilaya, mji, manispaa na majiji uonavyo mjadala huu zikabeba jukumu hili muhimu kwa afya za wananchi, ili liweze kufanyika kwa ufanisi.