Hapa pakiguswa vizuri, iko wazi patapunguzia elimu kero shuleni

06Apr 2021
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hapa pakiguswa vizuri, iko wazi patapunguzia elimu kero shuleni

UAMUZI wa serikali kuwapo elimu bure, umeleta unafuu kwa wazazi na walezi hasa kulingana na hali ya kiuchumi ya baadhi ya Watanzania, hatua inayochangia kuwapo tija katika sekta ya elimu, kwa kuwa inatoa fursa kwa kila mtoto kusoma.

Kimsingi, sera hiyo inamaanisha kufutwa kwa ada zote kuanzia elimu ya msingi hadi shule ya sekondari, ngazi ya kidato cha kwanza hadi cha nne. Wazazi wanakuwa huru kusomesha watoto wao katika ngazi hizo.

Pamoja na sera hiyo kuleta unafuu kwa wazazi na walezi, pia inatoa fursa kwa kila mtoto wa Kitanzania kupata elimu na imesababisha kero mbalimbali zinazochangiwa na baadhi kutafsiri vibaya sera hiyo.

Ni hali inayotokana na baadhi ya wazazi na walezi kuchagizwa na maneno ya baadhi ya wanasiasa majukwaani na hata wanaharakati ama kwa kudhania au kwa makusudi ya dhana zao, kwamba kupatikana elimu bora hakuna uhusiano na muungano wa majukumu na ushirikiano kati ya wazazi, serikali na wanafunzi.

Wapo wanaodhani kuwa, jukumu la kupata elimu kwa watoto wao ni la serikali peke yake, huku wao wakiwa na wajibu wa kufanya sehemu yao, kwamba ni njia ya kuboresha elimu nchini.

Hata ikiangaliwa kitaaluma na kiutawala, inapokuja suala la elimu bora, ni wazi linahitaji ushirikiano kati ya serikali, wazazi, wazazi na jamii kwa ujumla, pasipo kuisahau wadau wa elimu kitaifa.

Hivyo, inapendeza kushuhudiwa umma unaposhiriki kwa ujumla, kuwawezesha watoto wapate elimu bora.

Mfano hai, ni pale tangu sera ya elimu bila malipo ni mwongozo wa kisera ambao ulianza kutumika rasmi mwaka 2016, katika awamu ya pili ya uongozi wa nchi.

Sasa katika nyendo za utekelezaji na tafsiri yake ndiko kuna utata. Wako baadhi ya wazazi na walezi wanadiriki hata kugoma kuchangia chakula kwa ajili ya watoto shuleni, wakidai serikali ilishatangaza kutoa elimu bure.

Ni vyema tukakumbuka, serikali imeshatimiza wajibu wake wa kisera, ili kuwapa unafuu wazazi na walezi, pia wao wazazi na jamii hawana budi kutambua kuwa wana sehemu ya kufanya ikiwamo kuchangia chakula, ni njia mojawapo ya kuboresha elimu.

Binafsi ninaamini kuwa, iwapo kila mzazi atafanya sehemu yake, kero kwenye sekta ya elimu zinaweza kupungua, kwani pamoja na hatua ya serikali kuwa na sera ya elimu bila malipo, bado shule zinakabiliwa na kero mbalimbali.

Shule mbalimbali zimekuwa zikikabiliwa na uhaba wa madarasa, madawati, vyoo na miundombinu mingine muhimu, hali inayosababisha kila mwaka baadhi ya wanafunzi kutoanza masomo kwa wakati.

Kutokana na kuwapo uhaba wa miundombinu hiyo katika shule mbalimbali nchini, ingekuwa vyema serikali ikaruhusu kuwapo michango midogo itakayoridhiwa na wazazi na walezi.

Yawekwe mazingira ambayo yatafanyika michango hiyo, isiwe ya lazima kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, bali ifanywe kwa utaratibu utakaoridhiwa na wadau wa elimu, wakiwamo wazazi wenyewe.

Wakuu wa shule, kamati na bodi wanaweza kuibua hoja hiyo na kuwashawishi wazazi na wadau wengine wa elimu, ili kuona umuhimu wa kuwapo kwa michango shuleni ambayo haiwaumizi.

Njia hiyo inaweza kuwasaidia wazazi na walezi kutambua na kutimiza wajibu wao kuwa wana sehemu ya kufanya wakati huu wa elimu bila malipo, ili kupunguza kero mbalimbali zinazozikabili shule za msingi na sekondari.

Iwapo hali itaendelea kuwa kama ilivyo sasa, si vibaya serikali ikaboresha sera hiyo ili kutatua kero zinazozikabili shule za msingi na sekondari wakati huu ambao elimu bila malipo inaendelea kutolewa,

Serikali inaweza kuelekeza fedha katika ujenzi wa madarasa, utengenezaji madawati ya kutosha na uboreshaji wa miundombinu mengine ya shule.

Ikumbukwe kuwa, hadi sasa wanafunzi wanaochaguliwa kuanza elimu ya kidato cha kwanza wamekuwa wakianza masomo kwa awamu kutokana na uhaba wa madarasa na wengine wanajikuta wakikaa chini kutokana na uhaba wa madawati.

Hivyo, kwa mazingira kama hayo, ni wazi kwamba, ipo haja ya kuangalia upya sera ya elimu bila malipo ili ikiwezekana, fedha nyingi zielekezwe katika kuboresha miundombinu ya shule kwa ajili kumaliza kero hiyo.

Upo mfano kwamba, jumla ya wanafunzi 759,706 sawa na asilimia 91.1 ya wanafunzi waliofaulu wakiwamo wavulana 368,174 na wasichana 391,532 walichaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2021.

Hata hivyo, kuna wanafunzi 74,166 sawa na asilimia 8.9 wakiwamo wavulana 34,861 na wasichana 39,305 hawakupangiwa shule katika awamu ya kwanza, kutokana na uhaba wa madarasa.

Muungwana anaamini kwamba, iwapo fedha nyingi zitaelekezwa kwenye uboreshaji wa miundombonu ya shule, hakutakuwa na wanafunzi wanaosubiri kupangiwa shule awamu ya pili, badala yake wataanza masomo kwa pamoja.