Hatari kuendekeza imani za kutaka kuwaua wazee

07Feb 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hatari kuendekeza imani za kutaka kuwaua wazee

SERIKALI imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuhakikisha wazee wanaishi maisha bora, yenye staha kwa kutekeleza Sera ya Taifa ya Afya ya Mwaka 2007.

Hiyo ni pamoja na kuanzisha Mpango wa Utambuzi wa Wazee katika Halmashauri na kuwapatia vitambulisho vya matibabu bila ya malipo.

Pamoja na utekelezaji sera hiyo, serikali ina mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee, utakaozinduliwa Juni mwaka huu, kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya Mwaka 2003, ili iendane na hali halisi ya maisha yao.

Ni kauli iliyotolewa Septemba mwaka jana na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. John Jingu, kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee jijini Arusha.

"Kutokana na umuhimu wa uwepo wa wazee katika familia, jamii na taifa letu, hatuna budi kuitumia Siku ya Wazee Duniani kuhamasishana, kuelimisha na kukumbushana wajibu wetu kwa wazee wetu, ili kuwawezesha kuishi maisha bora yenye staha," anasema Dk. John Jingu.

Anafafanua kwamba tayari kuna wazee 576,370 walionufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini, tangu Februari mwaka jana, chini ya Mpango wa Taifa wa Kusaidia Kaya Masikini (TASAF).

Kutokana na idadi hiyo, wapo wanaume 217,947 na wanawake 358,423.

Pamoja na juhudi zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwamo asasi ya HelpAge Tanzania, ikinuia kuboresha maisha ya wazee, bado kuna changamoto kadhaa zinazowakabili.

Miongoni mwake ni mauaji ya wazee kutokana na imani za kishirikina, Kuna baadhi ya watu, wanaoendelea kuzikumbatia.

Watu wanaoendekeza imani hizo wanasababisha kukatisha maisha ya wazee au kufanya waishi kwa hofu badala ya kuishi maisha ya heshima, hadhi na kuthaminiwa utu wao.

Mwaka 2003, serikali ilitunga Sera ya Taifa ya Wazee, ambayo ililenga kutoa ulinzi wa kisheria, kwa kundi hilo maalum, pia kuwaboreshea huduma zote za msingi, ili waishi kwa usalama na heshima.

Ikumbukwe , sera hiyo inazitaka serikali za mitaa kutoa ulinzi na matunzo kwa wazee katika jamii kwa kushirikiana na familia. Kwa bahati mbaya, mauaji dhidi yao yameendelea katika baadhi ya mikoa nchini.

Shirika la Kutetea Haki za Wazee na Watu Wenye Ualbino (Tawlae), liliwahi kutoa ripoti ikionyesha kuwa wazee 50 waliuawa mkoani Shinyanga ndani ya kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.

Mbali na shirika hilo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi nayo iliwahi kutoa takwimu kuwa kuanzia Julai mwaka 2017 hadi Machi 2018, wazee 117 waliuawa nchini, huku watuhumiwa 100 wakiwa wamefikishwa mahakamani.

Inasemekana kuwa, wazee wamekuwa wakiponzwa na macho makundi ambayo baadhi ya watu wanaoamini ushirika, hudhani kwamba wenye macho ya rangi inayotokana na moshi wa majiko ya kuni ni wachawi.

Anna Rose Nyamubi, aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga vijijini, alishatamka kwamba kupatikana kwa nishati ya umeme katika wilaya hiyo, kutapunguza mauaji ya vikongwe, ambao wamekuwa wakiuawa kutokana na kuwa na macho mekundu yanayosababishwa na moshi wa majiko ya kuni.

Alitamka hayo kwenye uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini, unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vjjijini (REA) Awamu ya Pili uliofanyika katika Kata ya Lyabusalu, Shinyanga Vijijini.

Kwa mazingira hayo, ni wazi kuna haja ya watu waendelea kuelimishwa, ili waachane na mila hizo potofu, huku wakitambua kwamba wao ni wazee watarajiwa, hivi na wao wakiwa na macho mekundi wauawe?

Inasemekana kwamba, ifikapo mwaka 2050 idadi ya wazee nchini itakuwa imefikia asilimia 11 ya watu wote, kutokana na kile kinachoelezwa, ni uboreshaji wa huduma za afya za wananchi na idai yao inaongezeka

Mratibu wa Huduma za Afya kwa Wazee kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Edward Mung’ong’o, alishawahi kutamka kwenye Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, mwaka jana.

Wakati serikali ikijitahidi kuboresha afya za wananchi wake ili waweze kuishi miaka mingi, jamii nayo haina budi kutambua na kuwalinda wazee, ili wasiendelee kuwa katika hatari ya kuuawa kwasababu ya imani za kishirikina.