Hatari ya kutojua ukuu ulio ndani ya mwanao!

20Mar 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Hatari ya kutojua ukuu ulio ndani ya mwanao!

MPENZI msomaji, leo tuzungumzie watoto wetu. Nitazama zaidi kukuelimisha ujue kuwa mtoto wako anacho kitu kikubwa sana ndani yake pasipo wewe kujua na kumwona wa kawaida tu. Hii ni hatari sana!

Nitajaribu kugusa maeneo ambayo Mungu ameyaainisha kwenye maandiko yake kudhihirisha kuwa kabla mtoto hazaliwa, alishawekewa kitu cha thamani/ukuu ndani yake lakini kikaharibiwa aidha na mzazi mwenyewe au shetani na maajenti zake.

Naam. Mzazi kutojua ukuu ulio ndani ya mtoto wake ni hatari sana. Mtoto anapoharibika kitabia, mzazi ni wa kwanza kulaumiwa. Na ukweli unabakia pale pale kwamba usipojua ndani ya mtoto wako kuna nini, waweza kumwacha akaangamia au ukijua, ukamuokoa.

Watoto wamebebeshwa vitu vingi vizuri, na ajabu ni kwamba maajenti wa shetani( wachawi, waganga wa kienyeji n.k) wanajua mtoto fulani ana nini ndani yake cha thamani. Yaweza kuwa ni nyota nzuri ya elimu, utajiri, udaktari, uinjinia, mfanyabiashara, rubani, mkurugenzi, rais wa nchi na kadhalika).

Wazazi mara nyingi kabla hawajajua, maajenti wwa shetani wao walishajua na kuondoa kitu fylani ndani ya mwanao- utukufu, kitu kizuri, heshima- kile ulichozaliwa nacho.

Mtoto akiwa tumboni, shetani(aweza kuwa jirani yako mchawi, ndugu yako, rafiki yako) huhisi ukuu wake. Unajua “maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake”, yaani wale ulio karibu nao sana. Mathayo 10:36. Na pindi mtoto anapozaliwa, maajenti hao humfuatilia kwa karibu. Yupo atakayekuletea zawadi ya nguo kumbe imenuwizwa jambo fulani.

Yupo atakayempakata mwanao na kutamka maneno ya sifa kumbe kuna kitu anachukua toka kwa mtoto pasipo wewe kujua. Zote hizo ni mbinu za maajenti wa shetani kuiba ukuu wa mwanao.

Mungu katika maandiko yake ameweka wazi tahadhari zote kwa wazazi akionyesha mifano ya watu waliosikia maagizo ya kuokoa watoto wao na kufanikiwa. Na hiyo ilitokana na ukuu uliokuwa ndani ya watoto husika ambao baadaye walikuja kuwa watu wakuu ikiwemo wafalme.

Hebu tizama maandiko haya yaweze kujenga imani yako mzazi wa leo. Biblia Takatifu kitabu cha Waebrania 11:23 imeandikwa; ” kwa imani Musa, alipozaliwa, akafichwa miezi mitatu na wazazi wake, kwa sababu waliona kuwa ni mtoto mzuri; wala hawakuiogopa amri ya mfalme”.

Wazazi wengi leo hawajui nini kilicho ndani ya watoto wao. Heri kutozaa kuliko uzae mtoto awe jambazi, kahaba. Lazima umuombe Mungu akufunulie nini kilichoko ndani ya mtoto wako.

Andiko lingine; Kutoka 2:2-3, imeandikwa; “Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu. Na alipokuwa hawezi kumficha tena, akampatia kisafina cha manyasi akakipaka na lami, akamtia mtoto ndani yake, akakiweka katika majani kando ya mto “. Mtoto huyu ndiye baadaye alikuja kuitwa Musa.

Mwanamke huyo alijua kuwa baada ya vuguvugu la agizo la Farao la kuuawa kwa wazao wote wa kwanza wa kiume kuisha, mwanae atakuwa salama. Kutoka 1: 22, “kisha huyo Farao akawaagiza watu wake akisema, kila mtoto mwanaume atakayezaliwa mtamtupa mtoni, na kila mtoto mwanamke mtamhifadhi hai”.

Andiko lingine; Mathayo 2:13-14, imeandikwa; “Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize.

Akaondoka, akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; akakaa huko hata alipokufa Herode; ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, kutoka Misri nalimwita mwanangu.

Maandiko haya yanatufundisha kwamba mtoto kama umemzaa, hupaswi kumuacha. Hatma ya mtoto yaweza kupigwa kwa sababu tu mzazi hakujua ana nini ndani yake. Fuatilia nyendo za mwanao, anakuwa wapi na akina nani, ana marafiki gani, anaingia nyumba gani. Mtenge na marafiki wa ajabu ajabu wasio na maadili mema.

Mpenzi msomaji, mzazi kama hatakuwa makini, maajenti wa shetani wanaweza kuangamiza watoto wake, huku akidhani pengine ni laana au akachukulia kawaida kumbe ni matatizo makubwa.

Yupo mfanyakazi mwenzangu hivi majuzi aliniambia kuwa aliamka asubuhi akakuta mwanae miaka mitano ameng’olewa jino. Wakati bado anatafakari, baada ya siku mbili jino la pili halipo sehemu ya chini. Ni yale meno ambayo huanza kuota.

Anaye jirani ambaye hupenda sana kumwita mwanae huyo nyumbani kwake, akiwa na historia ya ushirikina. Swali;
kama unamjua mtu wa aina hii, kwanini usidhibiti wanao kwenda kwake? Ukiona kitu kimechukuliwa ndani ya mwanao, tayari hatma yake iko shakani . Wachawi huandama zaidi mtoto wa kwanza na wa mwisho kuzaliwa, wakiamini kuwa hao wana vitu vizuri sana ndani yao.

Somo hili tutaendelea nalo siku zijazo. Je, una maoni, kisa? Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; [email protected] au [email protected]
.