Hatuna mbadala, safari ya nishati ndio ahueni misitu

13Feb 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hatuna mbadala, safari ya nishati ndio ahueni misitu

MAZINGIRA ni jumla ya mambo na vitu vyote vinavyomzunguka viumbe hai na kwa kawaida, vinategemea mazingira, hata viumbe visivyo hai pia hutegemea mazingira, yanajumuisha ardhi, maji, hewa uoto, na vingine ambavyo kwa ujumla wake husababisha kuwapo kwa uhai.

Kutokana na umuhimu huo, kuna haja ya kupambana kwa kila njia ili kuhakikisha mazingira yanalindwa mazingira, kwa vile binadamu na viumbe vingine wa pamoja wanahitaji kuishi, hivyo jamii haina budi kushiriki kikamilifu kwenye kutunza nna kulinda mazingira hata kwa ajili ya maendeleo ya viwanda.

Bila ya kufaya hivyo, madhara yake yatakuwa ni makubwa, kwani athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira zinaweza kusababisha jamii kupata athari zikiwamo za ukame ambazo mwisho wake siku ni kukosa mazao ya chakula na biashara na hivyo kuathirika kiuchumi.

Nimegusia hilo kwa kifupi, ili kujadili kidogo suala la ukataji wa mitu kwa ajili ya biashara mkaa, ambayo imekuwa ikifanyika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu wa mazingira, ambayo mwisho wake nchi inaweza kugeuka jangwa kama kasi ya kukomesha biashara hiyo haitakuwa kubwa.

Inawezekana, kuna sababu zinazowafanya Watanzania kutumia nishati ya mkaa na baadhi ikiwamo utamaduni na mazoea, kwa kuamini kwamba mkaa unaivisha chakula vizuri, tofauti na nishati nyingine na pia gharama yake siyo kubwa sana kama ilivyo kwa matumizi ya umeme, lakini ukweli unabaki palepale kwamba matumizi ya mkaa yanaharibu mazingira.

Hebu fikiria, magunia ya mkaa yanayoingizwa jijini Dar es Salaam kila siku, ni wastani wa 400,000 hadi 500,000 huku matumizi ya kuni nchini yakiwa ni zaidi ya asilimia 71 ya watu wote. Hapa maana yake ni kwamba, miti mingi inakatwa kwa ya nishati na kusababisha uharibifu wa mazingira.

Hivyo ndivyo, Bunge limeelezwa juzi huku serikali ikisema kuwa inaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha gesi asilia inatumika majumbani, ili kupunguza uharibifu wa mazingira, watu 600 wameshanza kutumia gesi hiyo.

Ni jibu la Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, kwa swali la nyongeza la bungeni, alipohojiwa jitihada za serikali katika kulinda misitu na mikakati ya haraka wa matumizi ya gesi, ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Dk. Kalemani anasema, wiki iliyopita ameunganisha gesi kwa wafanyakazi 110 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na ni mkakati mzuri wa kupunguza uharibifu huo na kwamba ya pili, itakuwa ni kwa mikoa yote ya Tanzania Bara, kwa kuanza kusambaza mitungi iliyoshindiliwa gesi na kujenga mabomba kwenye mikoa hiyo kuanza kusambaza katika vijiji vyote ikiwa ni mkakati wa kupunguza uharibifu wa mazingira.

Ninaweza kusema kuwa hii ni habari njema na kama mkakati huo utakamilika, basi kwa kiasi fulani utapunguza matumizi ya mkaa ambayo kwa kweli yanachangia katika uharibifu wa mazingira ambao mwisho wake ni nchi kuwa jangwa, kutokana na miti mingi kukatwa.

Wafanyabiashara wa mkaa nao hawana budi kuliona hilo badala ya kujali pesa tu huku wakiharibu mazingira, kwani kama Dar es Salaam tu inapokea magunia ya mkaa kiasi hicho, ina matumizi ya mkaa kwa nchi nzima ni makubwa, kwani sidhani kwamba hakuna mkoa usiotumia nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constatine Kanyasu, Tanzania ina rasilimali za misitu zinazokadiriwa kufikia hekta milioni 48.1, ambapo asilimia 34.5 inasimamiwa na Serikali Kuu, asilimia 6.5 inasimamiwa na halmashauri na pia asilimia 45.7 inasimamiwa na vijiji, asilimia 7.3 inasimamiwa na sekta binafsi.

Asilimia sita ya misitu iko katika ardhi huria.

Anasema, kulingana na taratibu za serikali, misitu ya Tanzania inasimamiwa na Sheria ya Misitu ya Mwaka 2002.

Katika mamlaka za usimamizi wa misitu nchini, zipo wizara kuu mbili, ambazo ni Maliasili na Utalii, ambayo imekasimu mamlaka kwa Wakala wa Misitu (TFS), ambayo ina jukumu la kusimamia misitu ya hifadhi ya serikali kuu na misitu mingine yote ambayo haijahifadhiwa kisheria.

Naibu Waziri Kanyasu anabainisha utafiti uliopo, misitu ya Tanzania inakabiliwa na matatizo makubwa mawili, mojawapo ikiwa ni uharibifu mkubwa unaofikia kiasi cha hekta 372,000 kwa mwaka na mahitaji ya mazao ya misitu kwa mwaka yanayozidi uwezo wa misitu kwa zaidi ya mita za ujazo milioni 19.5.