Hatutegemei kelele za mwongozo, taarifa

20Apr 2016
Restuta James
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hatutegemei kelele za mwongozo, taarifa

KAMA nchi bado tunakabiliwa na matatizo lukuki, ndio maana hata kasi ya Rais John Magufuli, inawashangaza na kuwafurahisha wananchi kila siku kutokana na namna ‘madudu’ mapya yanavyoibuliwa.

Kuanzia kwenye utumbuaji majipu ya wakwepa kodi, wanaojinufaisha kupitia ofisi za umma hadi watumishi hewa, kote ni matatizo matupu.

Jana Bunge la Bajeti limeanza mjini Dodoma ambalo litajadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano.

Imekuwa kama desturi kwa wabunge wa upinzani kuibua kasoro zilizopo kwenye baadhi ya vipengele vya bajeti za wizara kadha wa kadha na wakati mwingine hutumia lugha kali kueleza kasoro wanazoziona.

Vivyo hivyo, wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekuwa na tabia ya kusifia bajeti na wakikaribia kuhitimisha wanataja matatizo ‘machache’ yaliyopo jimboni kwao.

Kasumba hii ya uchangiaji bungeni imekuwa ikiibua msuguano usio na sababu kwa pande zote mbili kurushiana kejeli na vijembe visivyolisaidia kabisa Taifa.

Tulishuhudia katika Bunge la Kumi kelele za kila upande kutaka mwongozo wa kiti cha Spika na kutoa taarifa kwa mbunge anayekuwa anachangia.

Yaani imejengeka tabia ya kila anapochangia mbunge wa upinzani, akiinuka wa CCM anamkejeli na kugeuka kuwa msemaji wa serikali kwa kusifia kila jambo linalowasilishwa na serikali!

Kusifia siyo kubaya, lakini kusifia hata pale panapohitaji marekebisho ya dhahiri, hakuisainii serikali bali kuididimiza.

Wakati wabunge wakifanya mipasho bungeni, kuna Watanzania wenzao hawajapata hata uji leo hii.

Ni wabunge hawa ambao baadhi yao walikuwa wakiamkia hadi watoto wakati wa kampeni na kuwaita wananchi ‘waheshimiwa’ leo thamani ya mwananchi imekuwa kujengewa ukuta kati yake na mwakilishi. Kwamba mbunge anauwezo wa kula vizuri, kulala pazuri na kumpatia mwanawe elimu nzuri lakini sio ‘waheshimiwa wananchi’ aliokuwa akiwalilia Oktoba mwaka jana.

Ni katika muktadha huo nasema kwamba wabunge lazima watambue kuwa kuna watu hawana maji, kuna Kata zisizo kabisa na zahanati; na wananchi wanahangaika usiku na mchana kusaka elimu.

Wakati mwingine, ukiangalia mjadala wa Bunge unaweza usiamini kinachoendelea kana kwamba wabunge hawaishi Tanzania!

Ni unafiki huu wa kutoona matatizo yanayowakabili wananchi ambao umekuwa ukiwagawa wabunge hadi wanaamua kupinga hoja ya Kambi ya Upinzani kwa sababu tu imewasilishwa na wabunge hao, si vinginevyo.

Wakati wabunge wakichangia bajeti ya mwaka huu, wakumbuke kwamba kuna kada nyingine tena muhimu zinaishia kupata tone la mapato ya mbunge kama mshahara wa mwezi mzima.

Angalia walimu, watafiti, madaktari na akina bwana shamba; uliza mishahara yao halafu jumlisha na misiba, kuuguliwa, harusi na ada za watoto, ndipo wabunge wanaweza kuthubutu kupiga mipasho.

Wakumbuke pia kuwa mtu yeyote anaweza kuishi bila mbunge, lakini hawezi kuishi bila daktari ambaye anaweza kumtibu pindi atakapougua.

Mijadala ya Bunge kutawaliwa na unafiki wa kiitikadi hata kwenye hoja za msingi; inadhihirisha kwamba baadhi ya wabunge wameingia bungeni kwa ajili tu ya kulinda maslahi ya chama badala ya Taifa.

Makofi yanayopigwa na wabunge wa CCM pindi mbunge wa upande huo anapochangia hata kama anachozungumza ni pumba, hayana faida zaidi ya kupoteza tu muda wa umma.

Binafsi sikubaliani na hoja ya kupinga kila hoja ya serikali au kuisifia, nia yangu ni kupima hoja na kuijadili kwa uzito stahili kwa kuangalia utaifa badala ya chama au ushabiki.