Hayati Karume akumbukwa kwa orodha ya mema kwa Taifa

08Apr 2021
Maulid Mmbaga
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hayati Karume akumbukwa kwa orodha ya mema kwa Taifa

KILA ifikapo April 7, siku kama ya jana, Watanzania wanaadhimisha kumbukumbu ya kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar. Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, aliyezaliwa mwaka 1905 na kufariki mwaka 1972.

Rais Sheikh Karume, aliongoza nchi baada ya mapinduzi yaliyomwangusha Sultani aliyekuwa akitawala Zanzibar, hadi mwaka 1964.

Baada ya miezi mitatu tu, Zanzibar iliungana na Tanganyika ilipokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Julius Nyerere na kufanya Muungano wa nchi hizo mbili, kukazaa taifa la Tanzania.

Katika maadhimisho hayo, Wazanzibari pamoja na jamii ya Wtanzania kwa ujumla, wanatakiwa kuitumia siku kama ya jana, kutafakari mambo muhimu yatakayoleta mshikamano katika Muungano na yatakayoleta maendeleo ya pande zote mbili.

Watanzania wanapaswa kuulinda na kuuenzi Muungano huo ulioasisiwa uendelee kuleta umoja na ushirikiano katika kutekeleza mambo mbalimbali ya maendeleo yatakayokuza uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kwa mwaka huu uliopo ni  mara ya kwanza taifa kuidhinisha siku hiyo chini ya marais wapya, Hussein Ali Mwinyi Zanzibar na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye ameingia katika wadhifa huo kikatiba, baada ya kufariki kwa aliyekuwa Rais, Dk. John Magufuli.

Sasa kilichopo mbele ya jamii ni kwamba, kila Mtanzania anapaswa kuenzi na kuulinda Muungano wenyewe usitetereke, kwa manufaa ya taifa kwa jumla, kama ambavyo viongozi wakuu wa nchi wanavyosisitiza umuhumu huo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Philip Mpango, juzi wakati alipozungumza katika hafla ya kuapisha makatibu wakuu, manaibu wao na wakuu wa taasisi za umma kadhaa, pamoja na viongozi mbalimbali wa umma alisisitiza haja ya ulinzi wa Muungano.

Dk. Mpango aliwataka wanaosimamia shughuli za muungano waweze kusimamia ipasavyo wakishirikiana pande zote mbili, ili kupunguza au kumaliza kabisa changamoto zinazotokeza.

“Wale wote wanaoshughulika na Muungano muhakikishe kwamba tunapiga hatua kubwa zaidi ya hapa tulipofika kwa manufaa ya taifa letu,” anasema.

Kimsingi, Ofisi ya Makamu wa Rais ndio inawajibika na maendeleo ya Muungano huo na miongoni mwa ufafanuzi katika mustakabali huo, umejumuisha ushirikiano wa kibiashara na miradi ya mkakati na kimaendeleo, itakayobaki kuwa sehemu ya nguzo itakayoendelea kuimarisha mshikamano kwa Watanzania kwa faida ya Taifa kwa ujumla.

Siku hiyo itumike kutafakari mambo mbalimbali ya kimkakati yatakayoisaidia nchi kupiga hatua kimaendeleo, kutoka hapo ilipo aidha kwa kubuni miradi na njia mbalimbali zitakazotupeleka mbele kiuchumi.

Hayati Sheikh Karume, alikuwa miongoni mwa waasisi watakaokumbukwa, si tu kwa historia ya kuongoza nchi pekee, bali inajumuisha mambo mbalimbali aliyolifanyia taifa lake, ambayo bado yadamu kubeba haiba ya faida.

Hapo kunatajwa mengi ya msimamo wa taifa na hadi sasa ikiwamo kushiriki katika suala la kuasisi Muungano.

Kila Mtanzania awajibike kuyakumbuka na kuyaenzi mambo ya msingi yaliyokuwa yanasisitizwa na waasisi wa taifa katika kujenga na kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania Bara na Visiwani kwa faida ya taifa kwa ujumla.