He! Simba, Yanga hufungwa kwa hujuma?

16Apr 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
He! Simba, Yanga hufungwa kwa hujuma?

NI timu gani ya kandanda duniani isiyofungika? Hebu nitajiwe moja tu ambayo tangu ilipoanzishwa haijapoteza mchezo wowote.

Hizo ziitwazo ‘kubwa’ hufungwa na timu zisizotarajiwa na kuwaacha mashabiki midomo wazi kwa kutoamini matokeo. Ndio, mpira unadunda na lolote laweza kutokea kwa sababu timu zote huingia uwanjani kwa lengo la kushinda.

Shindano ni tendo la kupimana uwezo katika jambo. Ni makabiliano yenye lengo la kuwania jambo baina ya pande mbili au zaidi. Hakuna upande unaocheza ili ushindwe. Kama lengo ni kushindwa, kwa nini timu inaingia mashindanoni?

Hivi majuzi Coastal Union ya Tanga iliifunga Simba 2-1 wakiwa uwanja wa nyumbani jijini Dar es Salaam. Kwa ushindi huo imeiondoa Simba kwenye harakati za kutwaa Kombe la FA.

Eti watu wanashangaa Simba kufungwa na Coastal Union. Kinachowashangaza ni nini? Katika msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom, Coastal Union wanashikilia mkia wakiwa na alama 19 baada ya michezo 26.

Ilibidi wacheze kufa au kupona, ili wacheze nusu fainali ya Kombe la FA na ikiwezekana walitwae. Hawakuja Dar es Salaam kushangaa ghorofa zinazochipuka kama uyoga. Walikuja kupambana. Kama kwenye Ligi Kuu wanashikilia mkia, basi hata Kombe la FA wasifanye vizuri?

Coastal Union ni timu pekee kwenye Ligi Kuu iliyozifunga Yanga (2-0) uwanja wa Mkwakwani, kisha Azam FC (1-0) kwenye uwanja huohuo jijini Tanga. Mcheza kwao hutuzwa.

Mara hii kwenye shindano la Kombe la FA, haohao Coastal Union wakaitoa Simba kwa kuifunga 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Kwa ufupi, ‘vigogo’ wote wa Dar es Salaam wameangushwa.

Miaka ya nyuma, kulikuwa na timu ya Reli mjini Morogoro iliyoitwa ‘kiboko ya vigogo’ kwa sababu ilizichachafya na kuzifunga Simba na Yanga mara kwa mara.

Angalau basi vijana wa Coastal Union waitwe ‘bakora ya vigogo’ kwa kuzifunga timu tatu za Bandari ya Salama – Yanga, Azam na Simba. Nani anathubutu kumcheka mwenziye kwa kipigo cha Coastal Union? Hakuna; na jiji limetuama kama maji mtungini.

Kuna madai kuwa eti Simba imefungwa kwa dhana mbili: kwamb,a kiwango chake kimeshuka! Walipumzika kwa muda mrefu bila kukuru kakara za Ligi Kuu.

Hawakuwa likizo ya starehe bali walifanya mazoezi kila siku wakijua wana mechi ya Kombe la FA dhidi ya Coastal Union.

‘Mapumziko’ ni kipindi cha kupumua baada ya kumaliza kazi. Lengo ni kupata fikra na nguvu mpya ili utakapoanza kazi uwe na ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya kama alivyosema Rais wa awamu ya nne, ingawa hakufanikisha azma yake.

Kwamba wachezaji walicheza chini ya kiwango ili kumhujumu (kumvurugia mipango) kocha kwa madai kuwa amekuwa na mgogoro wa ndani kwa ndani na wachezaji, nalo lanitia kichefuchefu (kuhisi kutapika).

Mchezo wowote una sehemu tatu: kushinda, sare/suluhu na kushindwa na ndio maana ya mashindano. Kwa nini Simba na Yanga zikishindwa mashabiki wao hutoa sababu za hujuma?

Mbona timu zao zinapobebwa na waamuzi (na mara nyingi huwa hivyo) hawasemi? Au ni ‘chongo kwa Mnyamwezi kwa Mswahili amri ya Mungu?’

Hebu nikumbushe mchezo kati ya Ndanda na Yanga uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kigi Makasi wa Ndanda alifunga bao zuri sana lakini kwa mshangao wa wanaojua kandanda, mshika kibendera alimwashiria mwamuzi wa kati kuwa eti mfungaji alikuwa ‘kaotea!’

Najaribu kuvuta hisia kama bao lile lingefungwa na Yanga kisha mshika kibendera alikatae, pangekuwa na songombingo (hali ya kutoelewana) pale uwanjani. Mashabiki wangerusha chupa na wengine wangeng’oa viti walivyokalia kuwa silaha.

Wakati hayo yakiendelea, upande mwingine wa watani, ungekuwa ukishangilia kwa sauti za juu na maneno ya kejeli.

Mwisho wa mchezo askari wangekuwa na kazi ya ziada kuwatoa waamuzi chini ya ulinzi ili wasishambuliwe na mashabiki wasiojua maana ya ushindani.

Ushabiki ni tabia ya kupenda au kupendelea sana jambo fulani. Hawa ndiwo wanaozusha tafrani za mara kwa mara kwenye klabu, ama kwa kutumiwa na viongozi wenye masilahi vilabuni au kwa kutojua wafanyalo!

Ni watu hatari sana. Ndio maana Simba na Yanga haziishi migogoro. Kukitulia Jangwani, kunaibuka Msimbazi na kukitulia Msimbazi kunawaka Jangwani.

Wengi wa mashabiki hawajali jinsi vilabu vyao vinavyoongozwa wala maendeleo yake. Wanachojua ni ushindi tu – uwe wa kununua na vinginevyo. Wenyewe husema “ushindi ni ushindi tu!” Watu wa aina hiyo utawaambia nini kuhusu kanuni na sheria za kandanda wakusikilize? Kwamba kandanda ni mchezo wa makosa na bahati, hawajui hilo.

Twasubiri kwa hamu maneno ya mashabiki wa timu zitakazotwaa Kombe la Ligi Kuu ya Vodacom na lile la FA; na ghamu (masikitiko) kwa mashabiki wa timu zitakazoshindwa. Halahala tusitoboane macho!

[email protected]
0715/0784 33 40 96