Heko wadau wa umma, binafsi kuboresha taaluma

07Sep 2017
Yasmine Protace
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Heko wadau wa umma, binafsi kuboresha taaluma

KUNA msemo wa wahenga kuwa elimu haina mwisho, hivyo hata kama unajiona umeelimika bado una wajibu wa kujifunza kwa wale walio na mafanikio zaidi.

Hiki ndicho anachokisisitiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga mkoa wa Pwani, Mshamu Munde, katika jitihada za kutaka kujifunza na kurekebisha makosa, anashauri shule za umma na binafsi zishirikiane, ili kuboresha elimu katika halmashauri hiyo.

Anataka walimu na wataalamu wa elimu wa halmashauri kukutana na wenzao wa shule binafsi kubadilishana ujuzi na zaidi wale wa serikali wapate mbinu za ufundishaji zinazosaidia wanafunzi katika shule za umma kufaulu.

Munde anahimizi walimu na viongozi wa shule binafsi kujadili na wenzao wa shule za serikali upungufu, changamoto na fursa zilizoko na kuweka mikakati itakayowezesha wanafunzi wa serikali wafaulu.

Anataka wapate mawazo na mikakati inayowawezesha wanafunzi wa shule binafsi kufanya vizuri na kufaulu kila wakati, huku wale wanaosoma shule za umma wakifanya vibaya.

Anatambua mchango ambao unafanywa na shule binafsi na kuwapa changamoto viongozi wa elimu wa halmashauri kushirikiana kuleta mahusiano mazuri katika kuinua elimu wilayani humo.

Shule za binafsi mara nyingi zinazofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kila miaka hivyo, wadau watambue mchango wao katika taaluma na kuutumia kusaidia maendeleo ya elimu.

Niupongeze uongozi wa Wilaya ya Mkuranga, kwa kutambua mchango wa elimu unaotolewa na shule za binafsi unaoleta matokeo mazuri kutoka kwa shule binafsi japo sekondari za serikali zinafanya vibaya.

Ikumbuke kuwa, shule za binafsi zikifanya vizuri au vibaya eneo liliko sekondari hizo ndilo hubeba sifa au lawama kutokana na ufaulu duni au wa viwango vya juu.

Hivyo basi kama shule za binafsi zinafanya vizuri, kuna haja ya kushirikiana nazo katika kuinua elimu katika shule za serikali, kama anavyosisitiza Munde.

Munde akizungumza katika mahafali ya 16 ya Shule ya Sekondari Ujenzi, iliyopo Mkuranga anasema shule binafsi zifanye juhudu za kiushirikiano, ili kuisaidia kujirekebisha na kufanya vizuri katika mitihani ya kila mwaka.

Anasema shule za binafsi zimekuwa zikifanya vizuri katika mitihani ya kila mwaka na hali hiyo, kuisaidia wilaya kuonekana iko juu kitaaluma japo shule za umma zenye idadi kubwa ya wanafunzi hazifanyi vizuri.

Anasema kutokana na shule za binafsi kufanya vizuri katika wilaya hiyo, anachotaka kuona ni ushirikiano baina ya shule hizo, ili kuinua elimu wilayani humo.

Kuomba msaada na ushauri si vibaya na hasa ukizingatia kuwa ushauri huo utawanufaisha wanafunzi wote kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya taifa.

Shule zikiungana na kupeana mikakati ni mbinu bora katika kujua siri na kuendeleza mikakati ya ufaulu.

Pamoja na shule za serikali kufanya vibaya, lakini haimaanishi kuwa hakuna cha kujifunza kutoka kwao, kwani umoja na nguvu na wanapoungana kwa pamoja watajifunza vile vitu ambavyo walikuwa hawavijui licha ya kufanya vizuri kitaaluma.

Mkurugenzi huyo pia, amemuomba mmiliki wa shule tatu za binafsi zilizopo katika Wilaya hiyo, Thadei Mutembei, ambazo shule zake zinafanya vizuri, kusimamia ushirikiano huo na kuwa na umoja, ili kuziwezesha shule za serikali nazo kufanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne na sita.

Anasema shule za serikali zijifunze kupitia shule hizo kutokana na kila mwaka kufanya vizuri katika mitihani yao.

Pia anasema mikakati ya wilaya katika kuboresha elimu ni pamoja na kusimamia taaluma, ili kuinua elimu katika kiwango cha ufaulu.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 matokeo hayakuwa mazuri, ambapo shule 10 zilifanya vibaya.

Anasema kuwa wanafuatilia ni kitu gani ambacho kimesababisha shule hizo kufanya vibaya, ikiwamo kuangalia uwiano wa walimu na wanafunzi Wilaya ya Mkuranga.

Pia mkakati mwingine ambao umewekwa na halmashauri hiyo, kuacha kuibua miradi ya maendeleo na nguvu zote kuzielekeza katika ujenzi wa maabara.