Hiki ndicho kiasi cha nyama nyekundu tunachopaswa kula

26Nov 2020
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hiki ndicho kiasi cha nyama nyekundu tunachopaswa kula

KWA muda mrefu, kumekuwapo na mjadala kutoka kwa watu wa kada mbalimbali unaohusu faida na madhara ya ulaji nyama nyekundu, ambayo ninaamini Watanzania wengi ni watumiaji.

Hiyo nyama nyekundu, ni ile yenye rangi nyekundu kabla ya kupikwa. Hapo kuna wanyama kama nguruwe, ng’ombe, mbuzi, kondoo na wanyama wengine, wote wanatembea kwa kutumia miguu minne.

Wapo wanaoshauri nyama hiyo iachwe na badala yake watu watumie mboga za majani na matunda kwa ajili ya kuendelea kulinda afya zao, ili kuepuka maradhi yatokanayo na ulaji wa nyama hiyo.

Mboga zinazoshauriwa kuliwa ni kama dengu, njugu na vyakula vyenye protini ya mimea ikiwamo mikate ya ngano isiyokobolewa, nafaka zisizokobolewa, karanga, maharage ya soya, kunde na vingine vingi.

Pamoja na hayo, inashauriwa kuwa mtu anatakiwa kula gramu 14 tu ya nyama nyekundu kwa siku, gramu 29 ya vyakula vitokanavyo na kuku, na gramu 13 ya mayai ama yai moja na nusu kwa wiki.

Kwamba, kwa kutumia kiasi hicho cha nyama nyekundu na kuendelea kula vyakula vya mboga, itasaidia kumuepusha mtu na maradhi yanatokana na nyama hiyo, na hivyo kuwa salama zaidi.

Ushauri huo umo katika utafiti uliochapishwa kwenye Jarida la Sayansi la Lancet mwaka jana, kuhusu mabadiliko yanayohitajika kwenye uzalishaji na ulaji wa chakula ili kuepusha vifo vya mamilioni ya watu.

Utafiti huo ulitangazwa na redio moja ya kimataifa, kwamba ni muhimu kufanya mabadiliko katika lishe ili kupunguza ulaji wa nyama hiyo na kugeukia zaidi vyakula vya mboga kwa usalama wa afya ya binadamu.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, nyama nyekundu huchangia hatari kwa mtu kupata ugonjwa wa moyo na saratani ya tumbo, kwa kuwa baadhi ya nyama hiyo huwa na kiwango kikubwa mafuta.

Mafuta hayo yanatajwa kuongeza lehemu mwilini, na kwamba mtu mwenye kiwango kikubwa cha lehemu, huwa hatarini kupatwa na ugonjwa wa moyo, hivyo ni muhimu kuwa makini katika ulaji wa nyama hiyo.

Vilevile, inaelezwa kuwa nyama nyekundu ina kemikali iitwayo 'carnitine' inayofanya mishipa ya damu kukakamaa na kusababisha kuzeeka kwa ngozi. Hivyo, inajenga maana ya umuhimu na kuwapo msisitizo wa kupunguza ulaji wa nyama aina hiyo.

Pia, Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FA0) katika taarifa yake, inasema nyama ya nguruwe inaongoza kuliwa kwa wingi duniani kwa asilimia 36, ikifuatiwa na kuku asilimia 35 na nyama ya ng'ombe asilimia 22.

Kwa kuwa nyama ya nguruwe nayo ni nyekundu na nyingine za aina hiyo, umefika wakati watu kuangalia uwezekano wa kuangukia ulaji wa kuku na kushusha nyama zote nyekundu kwa ajili ya kulinda afya.

Ni kweli, miili yetu inahitaji protini kwa ajili ya kujijengea kinga ya mwili kuanzia nyama, samaki, kuku, kunde, maziwa na vingine, lakini wataalamu wa afya wanasema, inawezekana mtu akapata kinga bila kula nyama.

Kwa hali hiyo, bado kuna haja ya kubadili mfumo wa ulaji kwa kuzingatia kile kinachoelekezwa na wataalamu hao, ikiwamo kuachana na nyama hiyo, ama kula kiasi kidogo wanachoshauri.

Inawezekana watu wengi wamekuwa wakikutana na utata kuhusu nyama nyekundu, lakini ni vyema kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuendelea kulinda afya kuliko kubaki kwenye mashaka.

Utata huo unakuwapo kutokana na maelezo mbalimbali yakiwamo kwamba, mtu anatakiwa kuchagua nyama ya ng’ombe anayepelekwa malishoni kula nyasi, na si anayelishwa mashudu ya mahindi ama nafaka mbalimbali.

Kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya ng’ombe anayechunga nyasi na yule anayelishwa kwa kufugwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, kwa kuwa nyama yake si salama, kama ilivyo ya yule anayepelekwa malishoni kula nyasi.

Jambo muhimu ni katika kulinda afya, hivyo kila Mtanzania hana budi kutafakari kwa kina kuhusu ulaji nyama nyekundu na kisha kuchukua hatua sahihi za kunusuru afya yake.