Hili la Asukile na tuhuma za rushwa Yanga limulikwe zaidi

03May 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Hili la Asukile na tuhuma za rushwa Yanga limulikwe zaidi

AKIWA na hasira ya kufungwa, nahodha wa timu ya Prisons, Benjamin Asukile, baada ya mechi dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga, aliongea maneno ambayo yamekuwa gumzo kubwa kwa mashabiki wa soka nchini.

Alisema mengi, akianzia kunyimwa penalti na walipokwenda kumuuliza mwamuzi akadai kuwa haoni. Mtangazaji aliyemhoji alimkatisha kidogo, lakini Asukile alionekana kutopendezwa na kitendo hicho.

Mwishoni akasema anashangaa kwa baadhi ya timu kutumia gharama kubwa kusajili wachezaji kutoka nje, lakini wachezaji hao wanashindwa kucheza mpira, badala yake wanalazimisha kushinda kwa kutumia hila.

Ukiisikiliza na kuangalia mahojiano yale, ni kwamba mtangazaji hakutaka mchezaji kutoa tuhuma zile kwa sababu hazikuwa na ushahidi. Lakini pia ukiangalia ni kwamba, mtangazaji alitaka mchezaji huyo kuendelea kumtuhumu mwamuzi na ilionekana hakuwa na shida na hilo.

Tatizo lake lilikuwa ni tuhuma za rushwa tu dhidi ya timu pinzani na Prisons. Kwa maoni yangu, wote walikuwa sahihi. Mtangazaji alichoamini ni hicho. Hakutaka kituo chake kiwe ndiyo chanzo cha tuhuma zile nzito za rushwa.

Asukile naye alikuwa sahihi. Aliwasilisha kile ambacho anakijua na anakiamini. Tatizo lake labda alikuwa na hasira aliyotoka nayo uwanjani. Sina tatizo na mtangazaji wala mchezaji. Kila mtu ametekeleza kile ambacho anaamini.

Nilichoshangaa ni kuona baadhi ya wachambuzi wakimuona Asukile kwamba hakuwa na uhakika, wala ushahidi na kile alichokisema zaidi ya jazba tu ya kufungwa. Inawezekani ni kweli, lakini utafiti au uchunguzi umefanyika?

Nilitegemea sasa waandishi wa habari kusaka ukweli wa hilo. Waandishi wa Habari za Uchunguzi wanaweza kuingia mzigoni na kutuletea habari iliyo sahihi. anaweza kutueleza wazi kuwa matokeo ya uchunguzi wao ni kweli au Asukile hakuwa mkweli.

Navyoona ni kwamba waandishi wa michezo wanadhani kwamba jambo hili haliwahusu na linahusu mamlaka husika pekee kama Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) pekee.

Asukile kwa sasa ametulia, hana jazba tena na inawezekana kabisa kwenda kumuuliza taratibu, atasema kwamba ilikuwa ni hasira tua au ni kweli. Anaweza kutoa namba za watu ambao wamepiga. Zinaweza kuwa siyo namba za watu husika, labda zimetumiwa tu.

Je wanaomiliki namba hizo wana nasaba na watu wanaotuhumiwa? Na mengi yanayofanana na hayo. Kwenye habari kama hizi ni lazima mwandishi awe kama mpelelezi halisi. Ukiangalia kila kitu au kila unachokitafuta kwa jicho la tatu.

Wakati mwingine hata serikali hutumia uchunguzi uliofanywa na waandishi kutatua tatizo, au kulishughulikia. Si kwenye siasa, au kijamii tu, bali hata kwenye michezo.

Mwandishi Sanula Athanas wa Nipashe, aliwahi kupata tuzo tatu za Mwandishi Bora wa Michezo kwa habari tatu za uchunguzi za michezo kwa nyakati tofauti. Moja ni ya upangaji wa matokeo kwenye Ligi Kuu.

Nyingine ni ubebwaji wa pesa za milangoni kwenye viroba na pia habari ya uchunguzi ya pesa za wachezaji na makocha kwenye soka kutokatwa kodi. Serikali ilifanyia kazi hili kwa kuleta tiketi za kieletroniki na pia sasa wachezaji na makocha wote wanakatwa kodi.

Hata hili, waandishi wachunguze na kuja na majibu, vyombo vya serikali navyo vinaweza kuingia walipoishia na wao kujidhihirisha, kama walivyofanya huko nyuma.

Kama tunataka kusaidia mpira wetu kwa sasa, ni wakati wa kutofumbia macho kero kama hizi zinazoibuliwa na wachezaji na mashabiki.